MBIO ZA MARATHONI DAR ZITAKUWA ZA KIPEKEE - UONGOZI SHULE ZA ATLAS - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday 17 September 2022

MBIO ZA MARATHONI DAR ZITAKUWA ZA KIPEKEE - UONGOZI SHULE ZA ATLAS

Washiriki wa Atlas Marathon yaliyopita wakiukimbilia ushindi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shule za Atlas Silvanus Rugambwa wa tatu kutoka kulia akiwaongoza viongozi waandamizi wa shule za Atlas katika Mahafali ya Kidato cha Nnne cha 2021 kilichoambatana na Atlas Marathon.

UONGOZI wa Shule za Atlas umesema mbio za Marathoni za mwaka huu zinazoendeshwa na shule hizo za jijini Dar es Salaam zitakuwa za kipekee zaidi ikilinganishwa na zilizo wahi kufanyika miaka mitatu iliyopita.

Akizungumza Ofisa Uhusiano wa Shule hizo zinazoongoza kitaaluma nchini, Calvin Obeid alisema zitakuwa za kipekee kwa kuwa kutakuwa na wazee ambao walishuhudia uongozi wa Mwalimu Nyerere wale wenye afya njema wakikimbia mbio za umbali mfupi na kisha kutunukiwa zawadi.

“Tunasema ni za kipekee kwakuwa kila mwaka tunafanya kwa wanafunzi wetu na watu mbalimbali lakini safari hii tunawashirikisha wazee kwakuwa Nyerere angelikuwa hai mwaka huu angetimiza miaka 100 na miaka yote kilele chake ni Oktoba 14,2022 kama sehemu ya kumuenzi Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere na Rais wa kwanza wa Tanzania,”alisema.

Obeid alisema kwa washiriki watakaohitaji kushiriki watalipia Sh 30,000 kwa ajili ya fulana na watapatiwa tuzo aina ya medali na zawadi mbalimbali kwa wazee na mbio hizo zitaanza kwa Km 5, 10 na 21.

Aidha kutakuwa na zawadi kwa Watoto watakaoshiriki tamasha hilo,kutakuwa na viburudisho mbalimbali ikiwemo nyama choma itakayotolewa bure.

Kwa upande wake Judith Audax kutoka Idara ya Fedha ya Shule hizo alisema ili kurudisha kile walichopata kwa jamii watatembelea kituo cha Afya cha Flamingo cha Madale na kutoa zawadi mbalimbali kwa mama na mtoto lakini kutakuwa na maonesho ya shughuli za walezi na wazazi.

“Kwanza ikumbukwe siku hii itaambatana na mahafali ya Kidato cha nne ambapo watatunukiwa vyeti na Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Serikali za Mitaa TAMISEMI, Innocent Bashungwa na wageni mashughuli wakiwemo wanasiasa na Mabalozi kutoka nchi mbalimbali," alisema Judith.

Aidha Judith aliwakaribisha wazazi, majirani na watanzania wote kuhudhuria tamasha na mahafali hayo na kujionea mazingira mazuri ya shule hiyo ambayo hufanya vizuri katika shule zake za awali, Msingi na Sekondari zilizopo Ubungo na Madale Dar es Salaam.

“Wakabie kwa wingi wajionee vipaji vya vijana wetu lakini pia mazingira rafiki ya kitaaluma na watakapoleta Watoto wao Atlas wajue wapo sehemu salama kuanzia chakula,malazi na kitaaluma pasipokusahau michezo”alisema Judith.

No comments:

Post a Comment