Ofisa Mipango Mwandamizi wa Internews, Victoria Rowan akiwasilisha mada katika mafunzo kwa wanahabari kuhusu usawa wa kijinsia. |
NA MWANDISHI WETU
MHADHIRI Msaidizi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) Zuhura Selemani, amesema vyombo vingi vya habari vinaandika na kutangaza habari zinazowahusu wanaume kuliko wanawake jambo ambalo si sawa.
Katika mada yake kwa wanahabari katika mafunzo ya siku moja kuhusu usawa wa kijinsia hususan katika siasa na uongozi pamoja na nafasi ya wanwake katika vyombo vya habari, Zuhura amenukuu utafiti uliofanywa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) mwaka 2019, akisema ingawa wanawake wengi huhitimu katika vyuo na vyuo vikuu vya uandishi wa habari kuliko wanaume, bado idadi ya wandishi wa habari wanawake katika vyombo vya habari na taasisi nyingine ni ndogo kuliko wanaume.
“Vyombo vingi vya habari pia havina sera kuhusu masuala ya jinsia na vingi kati ya vilivyo na sera hizo, havizitumii,” alisema.
Katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na taasisi ya Internews kupitia mradi wa Boresha Habari, Msimamizi wa Vyombo vya Habari wa Internews, Alakok Mayombo, alisema vyombo vya habari vinapaswa kuonesha mfano bora kwa kuandika na kutangaza habari kwa kuzingatia usawa wa kijinsia kwa kupaza sauti za watu walio katika makundi maalumu wakiwamo wanawake na wenye ulemavu.
Alisema ukosefu wa usawa wa kijinsia bado ni tatizo kubwa katika jamii katika nyanja mbalimbali zikiwamo za siasa, uwakilishi na uongozi sambamba na nafasi katika vyombo vya habari.
“Bado tatizo hili ni kubwa hivyo, lazima wanawake na wanaume washirikiane kuliondoa maana tunataka wote wasonge mbele hata katika shughuli zenye changamoto ili wapate uzoefu na nafasi ya kupanda juu hata katika vyombo vya habari hivyo, lazima hata wanaume waelimishwe na kushirikishwa katika juhudi hizi ili washiriki kuleta mabadiliko badala ya kuwa watazamaji,” alisema Alakok.
Mtaalamu huyo wa habari alisema lengo la kufikia uwiano wa 50 kwa 50 halipaswi kuwa katika siasa pekee, bali pia katika taaluma mbalimbali ikiwamo ya habari kwa kutoa nafasi sawa kwa wanawake na wanaume.
“Sauti za wanawake zisikike na pia, ni vema zioneshe mafanikio na uwezo wao badala ya wanawake kuoneshwa tu kwa matukio mabaya kama ya kubakwa na kupigwa,” alisema.
Katika mada yake iliyosisitiza tofauti baina ya jinsi na jinsia, Ofisa Mipango Mwandamizi wa Internews, Victoria Rowan, alisema ili kufikia usawa wa kijinsia, lazima wanawake na watu wenye ulemavu wapewe nyenzo na kusaidiwa kwa hali na mali ili kufikia uwiano.
“Si tu suala la wote kupata kwa usawa, bali walio pembezoni wapewe nguvu zaidi ili wafikie wenzao katika nyanja mbalimbali kama siasa, uongozi na kiuchumi kwa kuwa hakuna anayezaliwa akiwa kiongozi, bali wote huandaliwa,” alisema Rowan.
Alisema wanawake hawana budi kujengewa uwezo wa kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ukiwamo wa kisiasa huku kukiwa na mazingira wezeshi kama usalama, elimu na nguvu za kiuchumi.
Aliwataka wanawake kutojiweka nyuma zinapotokea fursa mbalimbali, bali wajitokeze na kuzichangamkia.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi isiyo ya kiserikali inayobadilisha maisha ya wanwake vijana na watoto (TIBA), Marcela Lungu, alisema elimu sahihi na endelevu inapaswa kutolewa kwa jamii ili kufikia usawa wa kijinsia.
Marcela alisema, “Vyombo vya habari vioneshe nguvu ya wanawake katika jamii ili jamii iwaone na kuwapa nafasi maana wapo wanawake wengi wenye uwezo mkubwa wa uongozi, lakini hawapati nafasi.
Akaongeza, “Tatizo hili linachangiwa pia na mtazamo hasi wa jamii, baadhi ya mila na desturi na baadhi yao wenyewe kutojiamini.”
Akijikita katika nadharia za uongozi katika mtazamo wa jinsia, mtaalamu wa masuala ya jinsia na maendeleo, Michael Marwa, alisema kitendo cha wanawake kujifunza majukumu yao mengi wakiwa katika umri mdogo, huathiri mitazamo yao na uchaguzi wa shughuli zao za kimaisha.
“Hili ndilo husababisha mtazamo kuwa jamii au kundi fulani ni viongozi bora kuliko wengine katika jamii jambo ambalo si kweli,” alisema.
Marwa ambaye pia ni Mkuu wa Mipango katika taasisi ya C-SEMA mkoani Dar es Salaam, alisema ukosefu wa uwakilishi wa kutosha wa wanawake katika uongozi si matokeo ya kinachodaiwa na baadhi ya watu kuwa uwezo mdogo au wanawake kutojiamini, bali imani potofu kuwa wanawake hawawezi kuwa viongozi bora.
“Jamii inapaswa kubadili mitazamo yao na kuweka usawa baina ya wanawake na wanaume,” alisema Marwa.
No comments:
Post a Comment