| Washiriki katika Kongamano la Wadau wa Hali ya Hewa linalofanyika nchini Tanzania, linalofadhiliwa na Shirika la Setelaiti za Hali ya Hewa la Ulaya (EUMETSAT). |
Na Joachim Mushi, Dar
KONGAMANO la Wadau wa Hali ya Hewa linalofanyika nchini Tanzania limekuja na neema kwa mataifa ya Bara la Afrika baada ya kubainika kuwa Shirika la Setelaiti za Hali ya Hewa la Ulaya (EUMETSAT) limepanga kurusha setelaiti mpya itakayoboresha taarifa za hali ya hewa kwa nchi za Afrika.
Akizungumza katika uzinduzi wa kongamano hilo kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atupele Fredy Mwakibete amelipongeza Shirika la Setelaiti za Hali ya Hewa la Ulaya (EUMETSAT) kwa uamuzi huo kwani unatarajia kuboresha zaidi taarifa za hali ya hewa kwa Bara la Afrika ikiwemo Tanzania.
Alisema Setelaiti itakayorushwa angani na Shirika la EUMETSAT inakwenda kuangalia taarifa za hali ya hewa na hasa kwa Bara la Afrika, hivyo kurahisisha sana upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa kiusahihi na kwa wakati, tofauti na hapo awali.
Akifafanua zaidi alisema Setelaiti iliyokuwa ikitumika awali ilikuwa ya kizazi cha pili (second generation) ilhali watakayorusha mpya kwa sasa itakuwa Setelaiti ya kizazi cha tatu (Third Generation) ikiwa imeboreshwa zaidi inayoweza kutoa taarifa za eneo kubwa kwa muda mfupi na uhakika zaidi.
"Kwa maana hiyo nchi za Afrika zote ikiwemo Tanzania tunakwenda kupata taarifa za usahihi zaidi na kwa wakati. Itakuwa ikitoa taarifa za eneo kubwa zaidi na kwa wakati mfupi.
Alisema kurushwa kwa chombo hicho cha kisasa kinachotoa taarifa za hali ya hewa kitasaidia mataifa ya Afrika hasa kwa sekta ambazo zimekuwa zikiathiriwa na hali ya hewa kama kilimo, uchimbaji madini, viwandani, sekta ya usafiri wa anga pamoja na maeneo mengine yanayotegemea taarifa za hali ya hewa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambaye pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dk. Agnes Kijazi aliishukuru EUMETSAT kwa msaada wa taarifa zake hasa kwa mataifa ya Afrika ikiwemo Tanzania.
Aliongeza kuwa taarifa za Shirika la EUMETSAT bado zinaumuhimu mkubwa kwa nchi za Afrika kwani zinaweza kutoa msaada wa taarifa za hali ya hewa hata kwa maeneo ambayo hayana mitambo ya kurekodia taarifa kwa wakati huo.
"...Kwa nchi za Afrika kutokana na kuwa na vifaa vichache vya kurekodia taarifa za hali ya hewa kuna maeneo mengine hayana kabisa vifaa hivi, lakini msaada mkubwa tunaupata kutoka katika taarifa za setelaiti iliyoko angani na kuweza kutoa utabiri katika maeneo hayo, hivyo unaweza kuona umuhimu wa setelaiti za EUMETSAT kwetu," alisema.
Alibainisha kuwa Kongamano hilo la watumiaji wa taarifa kutoka kwenye Shirika la EUMETSAT kwa Bara la Afrika, umejumuisha takribani mataifa 50 kutoka Bara la Afrika, wakiwemo Wakurugenzi wa Mamlaka za Hali ya Hewa za Afrika lengo likiwa ni kuangalia faida kwa taarifa za Hali ya Hewa zinazorushwa na EUMETSAT kwa nchi za Afrika pamoja na changamoto zake.

No comments:
Post a Comment