ANCEFA YAZITAKA SERIKALI ZA AFRIKA KUONGEZA BAJETI YA ELIMU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 18 August 2022

ANCEFA YAZITAKA SERIKALI ZA AFRIKA KUONGEZA BAJETI YA ELIMU

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Francis Michael akizungumza kwenye Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Elimu Bora uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Afrika wa Kampeni ya Elimu kwa wote (ANCEFA), Dk. John Kalage akizungumza kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Ubora wa Elimu ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET).


Mratibu wa Taifa TEN/MET, Bw. Ochola Wayoga akizungumza kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Ubora wa Elimu ulioandaliwa na Mtandao wa TENMET.


Na Joachim Mushi, Dar es Salaam

MTANDAO wa Afrika wa Kampeni ya Elimu kwa wote (ANCEFA) umesishauri Serikali barani Afrika kuhakikisha zinaongeza bajeti za elimu kufikia asilimia 4 hadi 6 ya pato la ndani (GDP) na asilimia 15 hadi 20 ya bajeti hizo.

Ushauri huo umetolewa juzi na Mwenyekiti wa ANCEFA, John Kalage kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Ubora wa Elimu ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julias Nyerere jijini Dar es Salaam.

Dk. Kalage alisema ripoti ya Kimataifa ya kufuatilia elimu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utamaduni na Elimu (UNESCO) ya mwaka 2021/22, inabainisha kuwa nchi zenye kipato cha kati na chini zimekuwa zikitoa fedha kwenye sekta ya elimu kwa asilimia 4.3 pekee.

“Kwa Tanzania inatoa asilimia 3.5 ya GDP na asilimia 13 ya bajeti yake kwenye elimu, ikimaanisha kuwa tunapaswa kufanya kitu kama nchi kufikia lengo,” alisema Dk. Kalage ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Haki Elimu Tanzania.

Alizitaja nchi zingine kama Namibia, Sierra Leone, Lesotho, Africa Kusini, Swaziland na Kenya, kuwa angalau zimefanikiwa kufikisha asilimia 5 ya GDP kwenye bajeti zao za elimu.  

Hata hivyo, mdau huyo wa elimu aliwataka viongozi wa Serikali na wanasiasa kuweka mikakati ya ukusanyaji wa mapato kwa ajili ya kugharamia elimu kwa kufikia malengo.

“Ipo haya ya kuongeza ukusanyaji wa kodi na kuzuia misamaha ya kodi na kuhakikisha kodi kwa GDP inaongezeka kufikia angalau asilimia 14.4 kulingana na Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano,” alisisitiza.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dk. Francis Michael akizungumza kwenye mkutano huo, alisema Tanzania imefanya juhudi kubwa kufikia malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) na hasa lengo la 4 la utoaji wa elimu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Francis Michael akipata maelezo alipotembelea banda la Haki Elimu kwenye uzinduzi Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Elimu Bora.

Baadhi ya washiriki na wadau wa elimu wakiwa katika mkutano huo.

“...Mkutano huu unafanyika wakati nchi ikiwa inafanya mapitio Mpango wa maendeleo ya sekta ya elimu (ESDP). Tenmet na wadau wengine wamehusishwa kikamilifu,” alisema Dk. Michael 

Awali akizungumza katika mkutano huo wa pili, Mratibu wa Taifa TEN/MET, Bw. Ochola Wayoga  alisema jumla ya wadau takribani 300 kutoka nchi zaidi ya 13 wameshiriki wakijadili jinsi elimu inavyochangia katika mabadiliko duniani.

No comments:

Post a Comment