Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wakati alipotembelea kiwanja cha ndege cha Njombe mkoani humo. |
NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuanza taratibu za kutafuta fedha za kujenga uzio katika kiwanja cha ndege cha Njombe ikiwa ni sehemu ya kuanza maboresho ya kiwanja hicho.
Akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanja hicho Naibu Waziri Mwakibete amesema kuwa uzalishaji wa mazao mbalimbali ikiwemo mboga mboga, mazao ya miti vinahitaji uwepo wa kiwanja cha kisasa kitakachokuwa kichocheo cha uchumi na kukuza biashara.
“Biashara hapa ni kubwa sana, kiwanja hiki kikiboreshwa kitakuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na kufanya biashara ziende kwa uharaka zaidi kwani wafanyabiashara watakuwa wana uwezo wa kuja na kufanya biashara na badae kuendelea na ratiba nyingine, amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu Waziri Mwakibete ameuomba uongozi wa Mkoa wa Njombe kuzungumza na taasisi za Serikali zilizo karibu na kiwanja hicho ili kuona uwezekano wa kupata eneo zaidi ambalo litatumika kwa kuongeza barabara ya kuruka na kutua ndege.
Kwa upande wake Mbunge wa Njombe Mjini, Deo Mwanyika ameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kiwanja hicho na kuanza taratibu za awali za kuboresha kiwanja hicho.
“Naipongeza sana Serikali kwani nimekuwa nikizungumzia sana kiwanja hiki, kwanini wenzetu Ruvuma, Mbeya na Iringa wana viwanja vyenye lami, ni wakati na sisi Njombe Serikali ituone kwa jicho la pekee sana, hivyo tunashukuru sana kupata lami kwenye kiwanja chetu’ amesisitiza Mbunge Mwanyika.
Naye Meneja wa Kiwanja hicho Lydia Mwenisongole amesema kwa sasa kiwanja hicho kinahudumia ndege ndogo za mashirika binafsi zenye uwezo wa kubeba abiria chini ya saba na ndege hizo huwa zinakuja mara chache kutokana na hali ya kiwanja kuwa cha nyasi.
Meneja Mwasongole ameongeza kuwa kwa sasa zoezi litakalofanyika ni kuzugumza na Uongozi wa Mkoa wakati TAA ikiendelea na taratibu za kuomba vibali husika ili kuendelea kutumika na kutoa huduma wakati Serikali ikitafuta fedha.
Kiwanja cha Ndege cha Njombe ni miongoni mwa viwanja vya ndege 59 vinavyosimamiwa na TAA na kiwanja hiki kina eneo la kuruka na kutua ndege la urefu wa mita 1800 na upana wa mita 30.
(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)
No comments:
Post a Comment