Na Adeladius Makwega – DODOMA
KWA miaka mingi nilikuwa nikiufahamu mkoa wa Mbeya kwa kuusoma katika ramani, huku nikitambua kuwa kabila wenyeji wa Mbeya ni Wanyakyusa. Mwaka 2001-2003 nilipokuwa mwanachuo wa Chuo cha Ualimu Kasulu mkoani Kigoma nilijaliwa kuwa na marafiki zangu wakubwa wawili ambao wote walikuwa ni wenyeji wa Mbeya.
Mboka Mwambusi na Pendo Haule, wazaliwa wa Mbeya, urafiki wangu na wao hakika ulinivutia na mimi kufika Mbeya mara baada ya kuhitimu Chuo cha Ualimu Kasulu mapema 2003.
Mwambusi alikuwa mwalimu aliyekuwa akisimamia shule na Chuo cha Ualimu cha familia yao naye Haule alikuwa akisomesha shule ya Sekondari ya Mbalizi iliyopo njia ya kwenda Tunduma.
Safari kwa rafiki zangu hawa wawili zilinisaidia kuifahamu Mbeya na kuwa Wanyakyusa hawakuwa wakipatikana kwa wingi Mbeya Mjini bali Wasafwa ndiyo wenyeji wa Mbeya Mjini.
Nilipokuwa Mbalizi nilibaini kuwa eneo hilo alikuwa akizaliwa Jenerali Robert Mboma ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Majeshi ya Tanzania. Nikiwa Mbalizi nilikuwa na rafiki yangu aliyefahamika kama Wiliam Sikumile (Mzee Msafwa). Mzee Sikumile alinieleza kwa kina juu ya uenyeji wa Wasafwa kuwepo katika eneo la Mbeya zaidi ya Wanyakyusa.
“Baba yangu alifariki miaka mingi akiwa na wake wengi na huyu unayemuona anayekaa pale ni mama yangu mdogo kabisa anaitwa Bi Nandoda.” Aliniambia Mzee Sikumile.
Mwaka 2003-2005 nikiwa Mbalizi Bi Nandoda alikuwa anapika chakula muda ukifika anamuita mtoto wake kula chakula iwe asubuhi, iwe mchana au iwe jioni. Baadaye niliambiwa kuwa William Sikumile kumbe alimrithi mke wa baba yake kwa miaka mingi sana (mama yake mdogo-Bibi Nandoda).
“Makabila haya ni ya wachapa kazi sana, nina hakika hata binti Makwega yoyote akiolewa kutoka kwetu akaja hapa hawezi kulala na njaa.”
Niliandika katika kurasa ya shajara yangu siku ya Jumatatu Novemba 19, 2018 nikiwa katika kijiji cha Nanyara-Mbozi, nikiwa mtumishi wa umma wa wilaya hii, niliitumia fursa hiyo vizuri sana kuyafahamu zaidi makabila ya ukanda huu kama vile Wasafwa, Wanyakyusa, Wakinga, Wandali, Wanyiha, Wasangu na Wawanji.
“Hata mwanangu akipata mchumba wa kuoa au kuolewa eneo hili, sina shaka nalo nitafunga safari na kutoa mahari hiyo au kuipokea posa hiyo kwa moyo mkunjufu kwa maana nmevutiwa na juhudi zao katika kazi.” Niliendelea kuyaelezea makabila haya ya ukanda huu katika kurasa ya shajara yangu ya mwaka 2018. Natambua kuwa hata wewe msomaji wangu unaweza kuwa na mtazamo wowote dhidi ya kabila fulani japokuwa mtazamo huo unaweza kuonekana kuwa wa kibaguzi.
Maisha ya Mzee Sikumile na mkewe Bi Nandoda niliyakumbuka sana maana tangu 2003 na hiyo 2018 nilikuwa nalifuatlia kwa karibu kabila la Wasafwa na makabila mengine ya ukanda huu.Mzee Sikumile alifariki mapema kidogo lakini Bi Nandoda alifariki 2021.
“Kulingana na sensa ya idadi ya watu iliyofanyika nyuma ya mwaka 1975 ilibaini kuwa katika eneo la Mbeya wakati huo kabila la Wasafwa lilikuwa na watu wanaokaribia 70,000 Mbeya watu 53,478, Rungwe watu 5884, Mbozi watu 9777 na Chunya watu 856.”
Wasafwa wakiwa wamegawanyika katika makundi makubwa matatu nayo ni WAPOROTO hawa wanapatikana upande wa Kaskazini mwa Rungwe, ndugu hawa wanapatikana katika eneo linalofahamika kama Uporoto huku ndugu hao wakiitwa Waporoto.Nako ndani yake kuna makundi makubwa mawili Wasafwa kamili na Washibinde. Washibinde wanapatikana upande wa magharibi wa milima ya Uporoto. Ndugu hawa kinachowatafautisha ni jiografia ya eneo tu lakini watu ni wale wale tu.
Historia inadai kuwa ndugu hawa wawili walibakia katika maeneo hayo baada ya kubakizwa na Wanyakyusa katika safari zao za Wabantu. Kwani wanafanana mno kwa kila kitu. Ndiyo kusema kama Wanyakyusa wanatokea Morogoro basi hata hawa wanatokeo huko huko pia.
Aina ya pili ya Wasafwa ni WAMBIRWA hao wanapatika upande wa mashariki ya Mbeya sasa ni eneo la Lujewa hasa hasa maeneo ya Irambo na Usoha.
Aina ya mwisho ni ya Wasafwa wenyewe (Wasafwa Asilia) hawa wanakaa eneo kubwa la Mbeya Mjini Vijijini(Kwa Mzee Sikumile na Bi Nandoda), Mbozi na Chunya ambayo sasa ni eneo la mikoa ya Mbeya na Songwe
Mtafiti M, B Mwangole-UTANI RELATIONSHIP:THE SAFWA-UTANI RELATIONSHIP IN TANZANIA, VOLUME FIVE EDITED BY STEPHERN, A LUCAS(1975) ukurasa 40-56, anasema kuwa neno linalosimama badala ya utani kwa Wasafwa ni Ilonkwi/ Ilenga wakimaanisha kuwa ni kinyume cha neno Ukweli(Uwongo). Utani huo unafanyika katika shughuli kadhaa za maisha kama vile siasa, kilimo, misiba, ndoa, na biashara.
Utani mkubwa ni baina ya Wasafwa na Wanyakyusa, huu ulienea zaidi kutokana makabila haya kufanya biashara ya mazao mbalimbali yakiwamo ndizi na mahindi. Kwa hiyo Wanyakyusa walifunga safari hadi kwa Wasafwa kununua mazao na jambo hilo lilifanya Wasafwa kuwaita Wanyakyusa watembea pekupeku – WAHONDWA hadi sasa Wasafwa wanaitwa Wanyakyusa kama Wahondwa wakimaanisa watembea kwa miguuu.
Pia utani mkubwa mwingine ni wa Wasafwa na Wasangu ikidaiwa kuwa Wasangu waliungana na Wajerumani na Waarabu dhidi ya Wasafwa ambapo hilo liliibua vita kubwa wakati wa karne ya 19. Ikidaiwa kuwa Wasafwa wengi waliuwawa katika vita. Jambo hilo lilisababisha Wasafwa kuwaita Wasangu kama WATANGA hiyo ikimaanisha kuwa Wasangu ni watu wasiokuwa Wasafwa yaani wageni. Hata leo watu mgeni kwa Wasafwa ni WATANGA.
Mwanakwetu kwa siku ya leo nimeamua niwakumbuke rafiki zangu hawa wawili Mzee Sikumile na mama yake mdogo Bi Nandoda aliyekuja kuwa mkewe ambapo kwa sasa wote ni marehemu ikiwa ndoa ya Mwana na Mama Mdogo.
0717640257
No comments:
Post a Comment