Na Mbaraka Kambona, Dodoma
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka Wafugaji na Wavuvi
nchini kuhifadhi mazingira kama njia pekee ya kuziwezesha sekta hizo za mifugo
na uvuvi kuwa endelevu katika kujipatia kipato na kukuza pato la taifa.
Ndaki alitoa wito huo baada ya kutembelea mabanda katika kilele cha
maadhimisho ya wiki ya mazingira duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma
Mei 5, 2022.
Alisema shughuli za ufugaji na uvuvi zinauhusiano mkubwa na utunzaji na
uhifadhi mazingira na ndio maana wizara inawasisitiza wafugaji na wavuvi
kuendelea kuhifadhi mazingira ili kufanya malisho ya mifugo yaendelee kuwa
mengi na mazalia ya samaki yaweze kuwa endelevu na kutoa mazao ya kutosha.
“Sisi wizara tunazuia kabisa wavuvi kufanya uvuvi katika matumbawe ambayo
ndio kiwanda cha kuzalisha samaki ili tuendelee kuwa na uvuvi endelevu na wenye
tija kwa taifa”, alisema.
Aliongeza kwa kusema kuwa ili mifugo iwe na ustawi inategemea uwepo wa
malisho na maji ya kutosha na ndio maana wanahimiza wafugaji kutunza nyanda za
malisho na vyanzo vya maji ili ufugaji uwe na faida kwa wafugaji na taifa kwa
ujumla.
Mkuu wa Kitengo cha Mazingira, sekta ya Uvuvi, Melton Kalinga alisema
utunzaji wa mazalia ya samaki ni muhimu kwa uvuvi endelevu lakini pia ni moja
ya vivutio vikubwa kwenye sekta ya utalii nchini.
Naye, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mazingira, Sekta ya Mifugo, Yusuph Selenge
alisema kuwa ni muhimu kuhifadhi mazingira kwa kuvuna na kuhifadhi malisho
kwani kufanya hivyo kunasaidia kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji na
watumiaji wengine wa ardhi huku akiongeza kuwa ni muhimu wafugaji kuzuia mifugo
yao kuzagaa hovyo kwa sababu ni chanzo cha uhalibifu wa mazingira.
Kwa upande wake Balozi wa Mazingira nchini na Mwandishi wa Habari, Oliver
Nyariga alisema ni muhimu kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya afya ya jamii na
kuepusha magonjwa mbalimbali yanayoweza kusababishwa na uharibifu wa mazingira.
Naye, Miss Udom mshindi wa tatu, Agnes Budeba aliwaomba wavuvi hususan
wanaofanya shughuli zao katika ukanda wa ziwa Viktoria kuhakikisha wanafanya
uvuvi endelevu na kujiepusha na uvuvi haramu ili shughuli za uvuvi ziwe na tija
kwao na taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment