WAZIRI DKT. GWAJIMA AWATAKA WATOTO KUFICHUA VITENDO VYA KIKATILI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 6 June 2022

WAZIRI DKT. GWAJIMA AWATAKA WATOTO KUFICHUA VITENDO VYA KIKATILI

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari kuelekea Siku ya Mtoto wa Afrika katika Shule ya Msingi Mnadani jijini Dodoma.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari kuelekea Siku ya Mtoto wa Afrika katika Shule ya Msingi Mnadani jijini Dodoma.

Na WMJJWM, Dodoma

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka watoto kote nchini kufichua viashiria vya vitendo vya kikatili dhidi yao vinavyotokea hasa katika maeneo ya shule na nyumbani.

 

Waziri Dkt. Gwajima, ameyasema hayo jijini Dodoma Juni, 06, 2022, akiwa katika Shule ya Msingi Mnadani alipokuwa akiongea na Wanafunzi, Walimu pamoja na waandishi wa habari kuelekea kilele cha Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa Juni 16 ya kila mwaka.

 

Waziri Dkt. Gwajima, amewasisitiza watoto hao kutokuogopa na badala yake waonapo vitendo vya ukatili au viashiria watoe taarifa kwa watu wanao waamini ikiwepo dawati la jinsia linalopatikana kwenye vituo vya Polisi.

 

”Wanangu, Baba akikukatli mwambie Mama na kama ni Mama basi mwambie Baba, au kama unaona huwezi kumwambia Baba au Mama basi mwambie mtu unayemwamini alisema Dkt. Gwajima.

 

Akitoa hali ya takwimu ya hali ya matukio ya ukatili kwa watoto katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2021, Mhe. Dkt. Gwajima amesema, jumla ya matukio yaliyoripotiwa ndani ya Jeshi la Polisi ni 11,499 ikilinganishwa na matukio 15,870 katika kipindi kama hicho mwaka 2020, sawa na upungufu wa imatukio 4,371 ikiwa na asilimia 27.5.

 

“Mikoa iliyoongoza ilikuwa ni Arusha (808), Tanga (691), Shinyanga (505), Mwanza (500) na Mkoa wa Kipolisi Ilala (489). Akisema makosa yaliyoongoza kwa idadi kubwa ni ubakaji (5,899), mimba kwa wanafunzi (1,677) na ulawiti (1,114)” amesisi Waziri Dkt. Gwajima.

 

Serikali kupitia Wizara yenye dhamana na Watoto iliandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 ambayo imeainisha Haki tano (5) za Msingi za Mtoto ikiwepo Haki ya Kuishi, Kulindwa, Kuendelezwa, Kushiriki na haki ya Kutobaguliwa. 


Sambamba na kuratibu utungwaji wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009.Ameongeza kuwa Msingi wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ni utoaji wa Haki za Mtoto kama ilivyoelekezwa na Umoja wa Afrika katika Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto wa mwaka 1991. Umoja wa Afrika ulitohoa maazimio hayo kutoka katika Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto wa mwaka 1989” alisema Dkt. Gwajima.

 

Akizungumza kwenye Mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri, ameahidi kutekeleza yote yaliyoelekezwa na Waziri Gwajima huku akisema, kwa kuwa ndani ya Shule hiyo kuna Baraza ya Watoto, watatumia siku hiyo ya Juni 16, 2022 kufanya mdahalo unaoendana na kaulimbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika ili kuwashirikisha watoto katika kujifunza mbinu mbalimbali za kujilinda na kutoa taarifa dhidi ya vitendo vya ukatili dhidi yao.

 

Kaulimbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa Mwaka 2022 ni “Tuimarishe ulinzi wa Mtoto; Tokomeza Ukatili Dhidi Yake: Jiandae kuhesabiwa” Kaulimbiu hiyo inasisitiza umuhimu wa kuimarisha juhudi za kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili na hatimaye kuvitokomeza kabisa. Aidha, wananchi wote wanahimizwa kujiandaa na kujitokeza kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika tarehe 23 Agosti, 2022.

No comments:

Post a Comment