SHIRIKA LA HJFRI LAPONGEZWA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO-19 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 26 May 2022

SHIRIKA LA HJFRI LAPONGEZWA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO-19

 

Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma toka Wizara ya Afya Dkt. Amalberga Kasangala (katikati) akizumgumza jana mjini Sumbawanga kwenye kikao kazi cha kupitia taarifa za utoaji chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa mikoa ya Rukwa ,Katavi na Songwe ambapo amesema bado hali ya uchanjaji ipo chini.

Na OMM Rukwa

SERIKALI imelipongeza shirika la HJFRI (Walter Reed) kwa kuwa mstari mbele kusaidia jitihada za utoaji chanjo na vifaa tiba katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kudhibiti ugonjwa wa UVIKO-19.

Akifungua kikao kazi cha kupitia taarifa za utoaji chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa mikoa ya Rukwa, Songwe na Katavi jana (25 Mei,2022) mjini Sumbawanga, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa David Kilonzo alisema shirika hilo limekuwa mshirika mkubwa wa serikali kwenye mapambano ya UVIKO-19.

Kilonzo alieleza kuwa historia ya nchi imepitia kipindi kigumu kutokana na ugonjwa wa UVIKO-19 kutokana na uwepo wa mitazamo tofauti kuhusu chanjo lakini shirika la Walter Reed walisaidia kutoa elimu kwa wataalam wa afya pia vitendea kazi kufanikisha zoezi la chanjo.

“Tunashukuru Walter Reed kwa ushirikiano katika mapambano dhidi ya UVIKO-19 kupitia mafunzo, vifaa tiba na elimu iliyowezesha mikoa yetu kuwafikia wananchi na kutoa chanjo ya UVIKO-19 kwa ufanisi japo bado baadhi ya watu hawajapata chanjo hiyo”alisema Kilonzo.

Akizungumza kwenye kikao hicho Mkurugenzi Mkazi wa HJFRMI Sally Chalamila alisema shirika lake kwa kushirikiana na timu za Afya ya mikoa na halmashauri ipo mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wengi wanapata chanjo dhidi ya Uviko-19.

Chalamila alibainisha mafanikio yaliyofikiwa na HJFMRI ni pamoja na kuwezesha ununuzi wamesaini 70 za kuisaidia kupumua, mitungi ya gesi ya oxygen 368, ventileta 5 na konekta 400 kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Aidha, alisema shirika hilo limefanikiwa kutoa elimu kwa timu za mikoa na wilaya kuhusu kampeni ya UVIKO-19  na umuhimu wa chanjo pamoja na utoaji wa usimamizi shirikishi.

“Pia tumeiwezesha hospitali ya rufaa ya kanda ya Nyanda za Juu Kusini kuweza kufanya vipimo vya UVIKO-19, yaani PCR test kwa kuboresha mashine na kutoa mafunzo kwa wataalam wa maabara juu ya upimaji. Huduma hii ni kwa mikoa 7 ya Nyanda za Juu Kusini” alisema Chalamila.

Kwa upande wake Mwakilishi toka Wizara ya Afya ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma Dkt. Amalberga Kasangala alisema kasi ya uchanjaji katika mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe bado iko chini.

Dkt. Kasangala alibainisha kuwa mikoa na halmashauri inatakiwa kuongeza kasi ya uhamasishaji ili wananchi wengi waweze kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19 .

 “Lengo la serikali ni kuhakikisha zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wote wenye umri wa kuanzia miaka 18 na zaidi wanapatiwa chanjo dhidi ya UVIKO-19 ili kufikia kinga jamii (Herd Immunity) ifikapo Desemba 2022”alisisitiza Dkt. Kasangala.

Dkt. Kasangala alisema pia hadi kufikia tarehe 24 Mei 2022 zaidi ya dozi 13,400,000 za chanjo dhidi ya UVIKO-19 zimepokelewa na kuanza kutumika katika mikoa yote ambapo kati hizo dozi 5,586,508 zimetolewa kwa walengwa.

Akitoa taarifa ya hali ya utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 kwa mkoa wa Rukwa Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Godfrey Mapunda alisema mkoa ulianza utoaji chanjo hiyo Agosti 04 mwaka 2021 ambapo hadi Aprili mwaka huu jumla ya dozi 121,722 zimetumika kati ya dozi 199,463 zilizopokelewa sawa na asilimia 61.

“Hadi kufikia Aprili 30 mwaka huu asilimia 11 ya walengwa walikuwa wamechanja dozi ya kwanza ya UVIKO-19 kati ya lengo la kimkoa la asimilia 60 huku waliochanja dozi ya pili ni asilimia 6.7 ya lengo la watu kimkoa ambalo ni asilimia 60” alisema Mapunda.

Kikao kazi hicho cha siku tatu kinawaleta pamoja Waganga Wakuu wa Mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe, Waratibu wa chanjo wa wilaya hizo pamoja na wataalam wa Wizara ya Afya na shirika la HJMFRI kujadili namna ya kuongeza kasi ya uchanjaji pamoja na upatikanaji takwimu sahihi.

No comments:

Post a Comment