MAMBO YA NDANI WAIVUA IKULU UBINGWA KIBABE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 27 April 2022

MAMBO YA NDANI WAIVUA IKULU UBINGWA KIBABE

Timu ya Idara ya Mahakama (kushoto) ikiwavuta timu ya Shirika la  Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC) katika michuano ya kombe la Mei Mosi Taifa lililofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Mahakama wameshinda kwa mivuto 2-0.

Mchezaji Mariam Shabaan wa timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani  (aliyedaka mpira) akichuana na Chuki George wa Ofisi ya Rais Ikulu katika mchezo wa nusu fainali wa michuano ya Kombe la Mei Mosi Taifa, uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Mambo ya Ndani wameshinda kwa magoli 45-39.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

TIMU ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi imewavua kibabe ubingwa wa mchezo wa netiboli timu ya Ofisi ya Rais Ikulu kwa kuwafunga magoli 45-39 katika mchezo wa nusu fainali wa mashindano ya Kombe la Mei Mosi Taifa 2022, uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini hapa.

Mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua uliifanya Mambo ya Ndani kuongoza katika robo ya kwanza kwa magoli 8-7; lakini wakati wa mapumziko Ikulu waliongoza kwa magoli 27-21; huku robo ya tatu Mambo ya Ndani waliongoza kwa magoli 35-26.

Katika mchezo mwingine timu ya Uchukuzi SC imewachapa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa kuwafunga kwa magoli 48-36, hadi mapumziko washindi walikuwa mbele kwa magoli 22-18.

Kwa upande wa mchezo wa kuvuta kamba timu za wanawake zilizoingia fainali ni Uchukuzi SC na Idara ya Mahakama, ambapo nazo zimewaondoa wapinzani wao katika michezo ya nusu fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri jijini hapa.

Uchukuzi SC waliwavuta Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa mivuto 2-0; nayo Idara ya Mahakama waliwavuta kwa mbinde timu ya Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC) kwa mivuto 2-1, ambapo walimaliza sare ya mvuto 1-1, ndipo ilipoongezwa mvuto wa tatu wa kuamua mshindi.

Nazo timu za wanaume za Uchukuzi SC na Idara ya Mahakama wametingia fainali baada ya kuwavuta wapinzani wao katika mchezo wa nusu fainali.

Timu ya Uchukuzi SC waliwasambaratisha Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mivuto 2-0; nayo Idara ya Mahakama waliwaondosha Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC) kwa mivuto 2-0.

Katika mchezo wa soka timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii wameingia fainali kwa kuwafunga Ulinzi kwa goli 1-0 lililofungwa na Hafidh Mohamed.

Katika mchezo wa bao ubingwa kwa wanawake umechukuliwa na Martha Mwasumbi wa Wizara ya Mambo ya Ndani, huku Zamira Fundi wa Wizara ya Kilimo ameshika nafasi ya pili na Regina Mtinangi wa TPDC ameshika nafasi ya tatu.

Michuano hiyo inaendelea kesho kwa kutafuta mshindi wa tatu katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanawake watacheza TAMISEMI na TPDC; wakati kwa wanaume watavutana Mambo ya Ndani na TPDC; huku katika mchezo wa netiboli watacheza timu ya Ofisi ya Rais Ikulu dhidi ya TANESCO.


No comments:

Post a Comment