MKOA WA KAGERA KUFUNGULIWA KIMIUNDOMBINU-PROF. MBARAWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 21 January 2022

MKOA WA KAGERA KUFUNGULIWA KIMIUNDOMBINU-PROF. MBARAWA

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge akizungumza na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, mara baada ya kuwasili mkoani Kagera kwa ziara ya kukagua miundombinu ya sekta za Ujenzi na Uchukuzi.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, katika picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa wa Kagera na Watendaji wa taasisi za Ujenzi na Uchukuzi mkoani humo.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge (kushoto) na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Profesa Faustin Kamuzora. 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akizungumza jambo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge (kushoto) na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Profesa Faustin Kamuzora. 

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema Serikali itaendelea na mkakati wake wa kuhakikisha miundombinu yote ya usafiri na uchukuzi mkoani Kagera inajengwa kwa viwango vya juu ili kuchochea uchumi wa mkoa huo.


Akizungumza mara baada ya kuanza ziara ya siku tatu Mkoani humo Prof. Mbarawa amesema Mkoa wa Kagera ni mkoa muhimu kiuchumi kwa Taifa kwa kuwa uko pembezoni mwa nchi na unaiunganisha nchi ya Tanzania na Uganda, Rwanda na Burundi ambapo ni soko zuri kwa bidhaa mbalimbali toka nchini.


“Tumejipanga kuhakikisha kwamba usafiri wa majini, angani na barabarani katika mkoa huu hususani kwa njia zote zinazounganisha Tanzania na Nchi jirani unaimarishwa na matokeo yake mtaanza kuyaona siku za hivi karibuni’ amesisitiza Waziri Prof.  Mbarawa.


Waziri Prof. Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha mipango yote iliyopangwa na Serikali mwaka huu mkoani humo inatekelezwa kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha katika miradi yote.


Prof. Mbarawa amitaka TPA Mkoani Kagera kutowabugudhi wafanyakazi katika bandari hiyo (makuli) ili  waweze  kufanya kazi zao kwa weledi.


Aidha, amesema kwa sasa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba kitaendelea kutumika na kuboreshwa ili kiweze kutoa huduma wakati wote na kuitaka Serikali ya Mkoa wa Kagera kuhakikisha eneo lililotengwa kwa ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Omukajunguti linahifadhiwa kwa matumizi ya siku zijazo. 


Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kuhakikisha barabara nyingi mkoani humo zinapitika wakati wote wa mwaka na kuwahakikishia kuwa mkoa huo utatoa ushirikiano kwa Wizara ili kuhakikisha miradi yote iliyopangwa kutekelezwa inakamilika kwa wakati.


‘Mhe Waziri Mkoa wetu huu barabara  zake zikifunguka na meli ya MV Mwanza ikianza kutoa huduma uchumi wa Kagera utaimarika na kuchochea uzalishaji wa mazao ya kilimo amesema Meja Jenerali Mbuge.


Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof. Faustin Kamuzora amemuomba Waziri Prof. Mbarawa kuwa ujenzi wa barabara ya Omugakorongo-Murongo KM 110 unaotarajiwa kuanza hivi karibuni sehemu ya kwanza uanzie Kayanga ili kuleta urahisi katika utekelezaji wa mradi huo.


Prof. Mbarawa yuko Mkoani Kagera kukagua miradi ya sekta za Ujenzi na Uchukuzi inayoendelea mkoani humo.



Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. 


No comments:

Post a Comment