TARURA YA WAPONGEZA WANANCHI KIGOMA UJENZI WA MADARAJA YA MAWE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday 10 October 2021

TARURA YA WAPONGEZA WANANCHI KIGOMA UJENZI WA MADARAJA YA MAWE

Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina (mwenye suti), akiongozana na Wajumbe wa Bodi ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), katika ukaguzi wa daraja la mawe la Bukuba lenye urefu wa mita 21 lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, mkoani Kigoma. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TARURA Mhandisi Florian Kabaka.

Muonekano wa ujenzi wa daraja la mawe la Bukuba lenye urefu wa mita 21 linalounganisha Vijiji vya Bukuba na Malanga likiwa limefikia asilimia 60 kukamilika. Kulia ni daraja la miti linalotumiwa na wakazi hao katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, mkoani Kigoma.

Na Thereza Chimagu, Kigoma

MWENYEKITI wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Florian Kabaka, amewapongeza wananchi wa Kigoma kwa kujitolea kwa dhati katika mradi wa ujenzi wa madaraja ya mawe na kuwasisitiza kuendelea kujitolea katika mradi huo ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya barabara hasa maeneo ya vijijini.

Mhandisi Kabaka alisema hayo alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa Miradi ya Ujenzi wa Madaraja kwa kutumia tekinolojia ya mawe akiambatana na wajumbe wa bodi pamoja na mtendaji mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff.

“Nawashukuru sana wananchi mnavyoendelea kujitolea katika ujenzi wa madaraja haya ya mawe.  Ninaomba muendelee kuhamasishana katika ujenzi wa madaraja haya ya mawe ili tuweze kujenga madaraja mengi zaidina kufugua njia nyingi zaidi na kurahisisha usafirishaji wa mazao yetu katika maeneo yaliyokuwa hayafikiki, alisema Kabaka”.

Aidha alieleza kuwa ushiriki huo wa wananchi unatia moyo kwa TARURA kuendelea kutafuta fedha zaidi na kuunga mkono nguvu kubwa ya wananchi waliyoionesha katika ujenzi wa madaraja hayo ili kwapamoja kuleta ufanisi katika shughuli za maendeleo kwa kurahisisha usafirishaji.

Naye ndugu Reuben Mwemeli mkazi wa Kijiji cha Nyabigufa, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma aliishukuru Serikali kupitia TARURA kwa kushirikiana na mfadhili katika ujenzi wa daraja la Nyabigufa, ambapo awali ilikuwa kero kubwa sana kwao kuvuka katika eneo hilo la mto ambapo wlikuwa wakipoteza ndugu zao hasa nyakati za mvua.

“Baada ya kuhamasishwa tuliamua kuweka nguvu zetu kwa kushiriki katika kukusanya mawe ili tuweze kupata daraja bora la kudumu ili kuepukana na ajali za mara kwa mara zilizokuwa zikitokea kutokana na kutumia daraja la miti ambalo lilikuwa hatarishi kwa usalama wetu, alisema Mwemeli”.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff alisema kuwa teknolojia ya ujenzi wa madaraja ya mawe ni nzuri kwa kuwa inapunguza gharama kwa takribani asilimia 40 kwa kuhusisha wananchi kujitolea kukusanya mawe na kutumia malighafi yanayopatikana katika maneno husika ya ujenzi wa madaraja hayo.

“Teknolojia ya ujenzi wa madaraja ya mawe inapun guza gharama kwa kiasi kikubwa, kitu ambacho kitatuwezesha kujenga maharaja mengi zaidi na kufungua barabara mpya maeneo yasiyofikika. Hivyo tunatarajia kuisambaza katika maeneo yote ambayo mawe yanapatikana kwa urahisi kwa kuendelea kushirikiana na wananchi, alisema Seff”.

Naye Ndg. Steven Hollevoet mratibu wa Mradi wa Kilimo Endelevu katika Mkoa wa Kigoma (Sakrip - Enabel) akiwakilisha Serikali ya Ubeligiji alisema ujenzi huo madaraja ya mawe umelenga kuwasaidia wananchi kusafirisha mazao yao kutoka mashambani kwenda masokoni.

Alisema kuwa mpaka sasa wamejenga Madaraja 36 na malengo ya Mradi ni kujenga madaraja 70.

Ujenzi wa Madaraja ya Mawe unafadhiliwa na Serikali ya Ubelegiji chini ya Mradi wa Kilimo Endelevu katika Mkoa wa Kigoma (Sakrip - Enabel) na kusimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA. 

Katika Mkoa wa Kigoma kwa sasa unatekelezwa katika Halmashauri za Buhigwe, Kasulu, Kibondo, Uvinza na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma; na unatarajiwa kusambazwa katika halmashauri zote za Mkoa wa Kigoma.

No comments:

Post a Comment