RC MAHENGE AKERWA NA MLUNDIKANO WA TAKA MANISPAA ATOA SIKU TATU ZIONDOSHWE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 27 June 2021

RC MAHENGE AKERWA NA MLUNDIKANO WA TAKA MANISPAA ATOA SIKU TATU ZIONDOSHWE

Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge alipofika kukagua  Ofisi za Manispaa ya Singida baada ya kuzungumza na watumishi na watendaji wa manispaa hiyo wakati akianza ziara yake ya kwanza ya kikazi kukagua miradi ya maendeleo, kuzungumza na wananchi,  kuhamasisha ukusanyaji wa mapato, ulipaji wa kodi na ushuru.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Singida (hawapo pichani) katika mkutano alioufanya jana  wakati wa ziara hiyo.

Watumishi na watendaji wa Manispaa ya Singida wakimsikiliza mkuu wa mkoa wakati alipokuwa akizungumza nao kwenye mkutano huo.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Deus Luziga akizungumza kwenye mkutano huo.

Mkutano ukiendelea.

Watumishi na watendaji wa Manispaa ya Singida wakimsikiliza mkuu wa mkoa wakati alipokuwa akizungumza nao kwenye mkutano huo.

Katibu Mwenezi na Itikadi wa Chama cha Mapinduzi (CCMMkoa wa SingidaAhmed Kaburu.akizungumza kwenye mkutano huo.

Naibu Meya wa Manispaa ya Singida Shabani Mkata akizungumza kwenye mkutano huo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akionesha uchakavu wa dari wakati akikagua ofisi za idara mbalimbali ndani ya Manispaa ya Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akiangalia takataka zilizorundikana katika moja ya maguba yaliyopo ndani ya manispaa hiyo.

Wananchi wakiangalia takataka zilizolundikana katika guba lililopo Soko Kuu la Manispaa ya Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge (katikati mwenye mvi) akiangalia gari la Halmashauri ya Manispaa hiyo ambalo lipo kwenye Karakana ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kwa ajili ya matengenezo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Kimataifa la Vitunguu.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akiangalia tenki maalumu la maji la mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika Kijiji cha Kisasida ambao uligharimu zaidi ya Sh.700 Milioni ambao haufanyi kazi kutokana na sababu mbalimbali.


Na Dotto Mwaibale, Singida


MKUU wa Mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge ametoa siku tatu kwa Manispaa ya Singida kuhakikisha inatoa takataka zote zilizojaa kwenye maguba ndani ya Manispaa hiyo.

Dkt.Mahenge alitoa agizo hilo jana wakati akiwa kwenye ziara yake ya kwanza ya kikazi ndani ya manispaa hiyo ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi baada ya kuhamishiwa mkoani hapa akitokea Dodoma.

Hatua hiyo ya kutoa siku tatu  kuondoa takataka hizo ilifikiwa na Mahenge baada ya kutoridhishwa na usafi wa mazingira ndani ya manispaa hiyo na uchakavu wa miundombinu ya barabara za mitaa hususani za eneo la Sabasaba.

" Kwa hali hii hatuwezi kabisa kufikia ndoto zetu za kuifanya Manispaa ya Singida kuwa jiji, hivyo naagiza kuanzia leo nataka kuona takataka zote hizi zilizo jaa kwenye maguba zinaondolewa" alisema Mahenge.

Alisema ratiba inayotakiwa kuanzia jana ni kufanya kazi ya kutoa takataka hizo kila siku kwa kutumia mapato ya fedha zao za ndani na kuwa usafi ndio unaowafanya wananchi wanaofanya biashara zao katika maeneo hayo kuzalisha zaidi wakiwa kwenye mazingira mazuri. 

Katika hatua nyingine Dkt.Mahenge aliagiza vikundi vyote vilivyokuwa vikifanya usafi ndani ya manispaa vilivyositisha kufanya kazi hiyo kutokana na kutolipwa fedha zao virudishwe mara moja na madeni yao yapangiwe namna ya kulipwa.

"Madeni yao myawekee ratiba ya kuyamaliza kuyalipa kwanza mtakuwa mmetoa ajira kwa vijana na kwa akina mama," alisema Mahenge. 

Aidha Mahenge aliwataka watu wote wanaohusika na usafi ndani ya manispaa hiyo kuhakikisha wanasimamia vizuri ukusanyaji wa mapato na kila mtu anayezalisha takataka anapaswa kuchangia kama wanavyochangia huduma za matumizi ya maji.

Mahenge aliitaka manispaa hiyo kuandaa mchanganuo na mpango mzima utakaoonesha jinsi ya kufanya usafi ambao watampa mkuu wa wilaya hiyo pamoja na yeye na kuonesha jinsi watakavyokuwa wakikusanya mapato.

Mkuu wa wilaya ya Singida   Mhandisi Paskas Muragili akizungumza katika ziara hiyo alisema wamekuwa wakipanga mikakati ya kufanya usafi lakini imekuwa haitekelezeki kutokana na kukosekana kwa ushirikiano mzuri na Menejimenti ya Manispaa hiyo. 

Dkt. Mahenge katika ziara hiyo alitembelea Soko la Kimataifa la Vitunguu na mradi wa kilimo cha umwagiliaji uliopo Kijiji cha Kisasida ambao uligharimu zaidi ya Sh.700 milioni lakini haufanyi kazi ambapo pia alizungumza na wananchi kujua changamoto zao na akatumia nafasi hiyo kuhamasisha ulipaji wa kodi na ushuru kutokana na biashara wanazozifanya ndani ya manispaa hiyo.

Leo Dkt. Mahenge ataendelea na ziara hiyo kwa kutembelea Kituo cha Afya  Sokoine na Mnada wa Mtamaa kwa lengo la kuona namna ya ukusanyaji mapato.

No comments:

Post a Comment