Eleuteri Mangi, Dodoma
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha na kuidhinisha Bajeti ya Wizara Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya jumla ya Sh.Bilioni 54, 741,802,000 ambapo kiasi cha Sh. 19,146,653,000 zitatumika kwa ajili ya mishahara, kiasi cha Sh. 14,880,149,000 za matumizi mengineyo na kiasi cha Sh. 20,715,000,000 zitaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Bajeti hiyo imepitishwa Mei 31, 2021 Jijini Dodoma baada ya kuwasilishwa na Waziri mwenye dhamana ya Wizara hiyo Mhe. Innocent Bashungwa na kujadiliwa na Wabunge kwa mujibu wa ratiba ya Bunge ili kutekeleza majukumu ya Wizara hiyo kwa mwaka 2021/2022.
“Wizara na Taasisi zake kwa kushirikiana na wadau, itatekeleza majukumu yaliyopangwa kwa kuzingatia maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020-25, ahadi na maelekezo mbalimbali ya Viongozi wa Kitaifa na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 - 2025/26” amesema Waziri Bashungwa.
Aidha, Waziri Bashungwa ameongeza kuwa utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo yatazingatia malengo ya Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030 katika maeneo ambayo yanayohitaji kuchukuliwa hatua.
Kwa upande miradi ya maendeleo, Mhe. Bashungwa amebainisha kuwa Wizara itatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, Ujenzi wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, ujenzi wa eneo Changamani la Michezo Dodoma, ujenzi wa eneo Changamani la Michezo Dar es Salaam, ujenzi wa vituo vya mazoezi na kupumzika wananchi na ukarabati wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo.
Miradi mingine ni ukarabati wa Chuo Maendeleo ya Michezo Malya, Upanuzi wa Usikivu TBC, kufunga Mtambo Mpya wa Kisasa wa Uchapaji pamoja na Mradi wa Elimu kwa Umma.
Wakichangia hotuba hiyo, Wabunge Sophia Mwakagenda na Stanislaus Nyongo wamesema mradi wa usikivu wa TBC ni muhimu ufikie mwisho ili maeneo ya mikoa ya pembezoni mwa nchi yaweze kusikika hatua itakayowapa fursa Watanzania wanaishi katika maeneo hayo kupata haki yao ya msingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18 ya kupata taarifa.
No comments:
Post a Comment