BARABARA YA CHUNYA-MAKONGOROSI YAFIKIA ASILIMIA 91 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday 29 May 2021

BARABARA YA CHUNYA-MAKONGOROSI YAFIKIA ASILIMIA 91

Muonekano wa Daraja Lupa katika barabara ya Chunya hadi Makongorosi mkoani Mbeya (KM 39), inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi kutoka Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group. Ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 91 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.



Muonekano wa barabara ya Chunya hadi Makongorosi mkoani Mbeya (KM 39), inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi kutoka Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group, Ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 91 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.


IMEELEZWA
kuwa mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya hadi Makongorosi, mkoani Mbeya inayojengwa kwa kiwango cha lami na Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation, uliofikia asilimia 91 unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu. 

Akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi huo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mwita Waitara amemtaka mkandarasi kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa viwango kama ilivyoainishwa kwenye mkataba. 


Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 39 inajumuisha ujenzi wa madaraja makubwa matatu ambayo yamekamilika kwa asilimia 100 pamoja na ujenzi wa jengo la wazazi katika mji mdogo wa Makongorosi ambalo ni utekelezaji wa ahadi ya Mkandarasi kwa Serikali.


“Tunaelewa kuwa mmekuwa mkipitia changamoto mbalimbali ikiwemo mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana, ila tumieni vema muda wa ziada mlioomba ili mradi huu ukamilike na wananchi wafaidi matunda ya Serikali yao kwa kuanza kutumia barabara ya lami” Amesema Waitara.


Aidha, Waitara amemtaka Mkandarasi huyo kurekebisha kasoro zote zilizobainishwa kwenye ujenzi wa jengo  la wazazi katika mji mdogo wa Makongorosi kabla ya kulikabidhi kwa Halmashauri.  


“Hili ni jambo jema kurudisha kwa jamii lakini hakikisheni kuwa jengo hili linakamilika kwa wakati ili hospitali ya mji mdogo wa Chunya itakapokamilika jengo hili pia lianze kutumika kama ilivyokusudiwa”, amesisitiza Waitara 


Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo Mhandisi Mshauri wa kampuni ya SMEC International na Mhandisi Consultancy alimueleza Naibu Waziri huyo kuwa kazi zinazoendelea ni ujenzi wa njia za waenda kwa miguu sehemu za makazi ya watu, kujenga kingo za madaraja matatu na kwenye matuta yenye kina kikubwa. 


Kazi nyingine ni kuweka mistari ya kutenganisha njia za magari ambapo kazi hiyo imefikia asilimia 84 pamoja na kujenga maingilio ya barabara ndogo kwenye barabara ya mradi. 


Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mbeya, Mhandisi Magesa Mwita amemuhakikishia Naibu Waziri Waitara kuwa wataendelea kusimamia kwa karibu kazi zilizobaki na kuhakikisha kuwa viwango vinazingatiwa kama ilivyo ainishwa kwenye mkataba.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya-Makongorosi unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.


Imetolewa na KItengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi


No comments:

Post a Comment