RTOs TUSAIDIENI KUFUNGIA LESENI ZA MADEREVA WENYE MAKOSA YA KUJIRUDIA RUDIA TUSIMSUBIRI MKUU WA KIKOSI AMA WAZIRI - THE HABARII

THE HABARII

HABARI | MATUKIO | MICHEZO.


ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 4 April 2021

RTOs TUSAIDIENI KUFUNGIA LESENI ZA MADEREVA WENYE MAKOSA YA KUJIRUDIA RUDIA TUSIMSUBIRI MKUU WA KIKOSI AMA WAZIRI



RTOs TUSAIDIENI KUFUNGIA LESENI ZA MADEREVA WENYE MAKOSA YA KUJIRUDIA RUDIA TUSIMSUBIRI MKUU WA KIKOSI AMA WAZIRI

Ni wazi kuwa juhudi zinafanyika sana katika kudhibiti makosa ya barabarani, hususani katika ngazi ya mikoa na Wilaya. Na pongezi za juhudi hizi bila shaka ni lazima ziwaendee Wakuu wa Trafiki katika ngazi za Mikoa maarufu kama RTOs. Hata hivyo, ni imani yangu na ya wengine kama mimi kuwa bado RTOs wanaweza kusaidia sana kuleta nidhamu barabarani kutokana na mamlaka na nyenzo walizonazo katika kudhibiti tabia hatarishi za madereva barabarani.

Mamlaka hayo ni yale yanayopatikana kwa mujibu wa sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168.

1. Mamlaka ya kukagua na kukamata

Mamlaka haya yanapatikana kifungu cha 73-89. Na kwa kweli yamekuwa yakitumika mara kwa mara.

2. Mamlaka ya Kufungua Mshataka

Mamlaka haya yanapatikana kifungu cha 72 na 73. Tumeona mamlaka haya yakitumika na kwa kiasi kikubwa maamuzi yake ya mwisho yanategemea mahakama.

3. Mamlaka ya Kufungia Leseni

Mamlaka haya yanapatikana katika kifungu cha 28(4) cha Sheria ya Usalama Barabarani. Na leo nataka kuzungumzia hasa matumizi ya mamlaka haya ambapo kama yatatumika vizuri na kwa ufanisi yanaweza kuleta nidhamu kubwa barabarani.

Licha ya Mamlaka haya tunafahamu mikoa inazo nyenzo kama vile tochi (speed radar na vipima ulevi), na zaidi ya hayo tumeambiwa kuwa RTOs wote sasa wanaweza kuona magari(mabasi) kwenye mfumo wa VTS unaomilikiwa na LATRA. Tunaamini hizi ni nyenzo muhimu sana za nyongeza.


Mamlaka ya Kufungia Leseni

Mara kwa mara tumekuwa tukishuhudia hatua za kufungia leseni za madereva, hasa wa mabasi makubwa, zikichukuliwa na Trafiki Makao makuu. Binafsi nimekuwa nikijiuliza kwa nini Trafiki Makao Makuu? Mbona hatusikii katika ngazi za mikoa madereva hawa hawa wamefungiwa leseni? Au RTOs wao wanahusika kufunga leseni za daladala tu na zile coaster zinazosafiri ndani ya mkoa? Ukisikia dereva kafungiwa leseni mkoani basi sana sana itakuwa sababu kafanya ajali. Lakini katika hali ya kawaida hatusikii. Lakini basi kama mnafanya hilo rai yangu ni tujuzeni kupitia vyombo vya habari walau kila mwezi au taarifa zenu za robo mwaka, inasaidia sisi madereva kuwa na woga Fulani huko barabarani. Lakini kama haifanyiki kabisa, basi tumieni mamlaka mlopewa chini ya kifungu cha 28(4) kuleta nidhamu barabarani.

Kwa mujibu wa kifungu cha 28(4)(b) Afisa wa Polisi wa cheo cha Mrakibu Msaidizi (Assistant Superintendent) au cheo cha juu yake, anayo mamlaka ya kufungia(suspend) kwa muda wa miezi sita (6) leseni ya dereva anayekiuka sheria za usalama barabarani. Kifungu cha 28(4) (a) kinampa afisa mwenye cheo tajwa hapo juu Mamlaka ya kutoa onyo kwa dereva anayekiuka sheria. RTOs wetu tulionao wana cheo cha kuanzia nyota 3 (ASP) na kuendelea. Hivyo kwa mujibu wa sheria hii wanahusika kabisa na wanayo hayo mamlaka.

Kutokana na usimamizi wao wa kila siku wa sheria barabarani wanao uwezo wa kutambua madereva wanaotenda makosa hatarishi na ya kujirudia rudia. Kwa upande wa mabasi VTS inawapa uwezo zaidi wa kutambua madereva wa mabasi wenye makosa hatarishi au tabia hatarishi na kuchukua hatua kabla hazijasababisha madhara. Hivyo ni rahisi kwao kutoa adhabu ya faini na onyo juu kwa mujibu wa kifungu cha 28(4)(a). Uzuri wake sasa hivi mfumo wa TMS unatunza rekodi za makosa. Hili linafanya iwe rahisi kwa RTO kufahamu dereva husika anatenda kosa la kujirudia na hivyo kuweza kutumia mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa kif.28 (4)(b) kufungia leseni. Madereva sisi tukijua huko mikoani mnafunga leseni sio lazima Dar es salaam, basi tutakuwa na woga.

Binafsi huwa nashindwa kuelewa, kwa nini dereva atende kosa TABORA halafu RTO aelekezwe kuituma leseni ya dereva huyo Dar es salaam ikafungiwe, au apeleke taarifa Dar es salaam ndipo dereva akafungiwe wakati yeye RTO mwenyewe anaweza kumfungia na kuwasilisha ripoti trafiki kuu na TRA.

TUKUMBUKE Sheria inasema note exceeding 6 months, hii maana yake kwamba RTO anaweza kufunga leseni ya dereva kwa kipindi chochote kuanzia mwezi mmoja hadi miezi 6. Miezi sita ndio maximum. Kwa hiyo dereva anaweza kufungiwa mwezi 1 au 2 au 3 au 4 kutegemeana na uzito wa kosa. 

Hebu pokeeni rai hii muifanyie kazi. Lakini pia trafiki kuu tunaomba muelekeze pia macho yenu katika kuboresha mfumo wa TMS. Kuwepo na ubunifu. Wenzenu TIRA walikuwa na TIRAMIS version 1 sasa wamekuja na TIRAMIS version 2 iliyoboreshwa na yenye ufanisi zaidi. Sisi tumebaki na TMS version ile ile. Nini kinashindikana kuboresha TMS ili:

1. Dereva aliyefungiwa leseni au kufutiwa taarifa zake zipate kuonekana kwenye POS na TMS?

2. Dereva aliyepewa onyo taarifa zake zipate kuonekana kwenye POS na TMS?

3.  RTO aweze kuona taarifa za makosa ya dereva hata kama alishalipa faini?

Haya ni kati ya mambo madogo sana yanayoweza kuboreshwa kwenye mfumo na ukawa na ufanisi zaidi.

Naomba kuwapa changamoto

RSA Tanzania

Usalama Barabarani ni Jukumu Letu Sote.

No comments:

Post a Comment