Kuelekea mfungo wa Ramadhan, Mkurugenzi wa Benki ya CRDB, Abdulmajid
Nsekela leo ameambatana na familia yake pamoja na wafanyakazi wa benki
hiyo kotoa sadaka ya futari ya thamani ya shilingi milioni 10 kwa vituo 5
vya watoto yatima katika mkoa wa Dar es Salaam.
Hafla hiyo
ilifanyika katika viwanja vya Karimjee na kutanguliwa na ibada ya Ijumaa
iliyoongozwa na Imam, Haroub Khamis katika Masjid ya Karimjee.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Nsekela amesema sadaka hiyo ni
sehemu ya shukrani ya familia yake na muendelezo wa utamaduni wa Benki
ya CRDB kutoa sadaka kwa makundi yasiyojiweza na kuandaa futari maalum
kwa ajili ya wateja na wadau wake katika mfungo wa Mwezi Mtukufu wa
Ramadhan.
“Tukikaribia kuanza Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambapo mioyo na fikra
vipo katika kumnyenyekea Muumba tumeona ni jambo la faraja kujumuika kwa
pamoja na watoto yatima katika ibada hii ya funga kwa kuwapatia msaada
wa futari,” alisema Nsekela huku msaada huo pia utatolewa katika vituo
vya watoto yatima katika kanda zote nchini.
Akisisitiza juu ya
umuhimu wakuwasaidia watu wasiojiweza, Nsekela alisema katika kipindi
cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni vyema jamii ikafahamu wapo watu ambao
iliwaweze kutimiza funga yao kikamilifu wanahitaji msaada kutoka kwa
wale ambao wenye uwezo.
“Kutoa msaada kwa watu wasiojiweza ni kujitafutia thawabu, lakini pia
kunasaidia kudumisha upendo kwa ndugu, jamaa, marafiki na jamii kwa
ujumla wake. Hata katika Quran takatifu Surah Al-Baqarah aya ya 2:83,
Mwenyezi Mungu ametuamrisha kuwasaidia yatima na wasiojiweza,”
aliongozea Nsekela.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya vituo vya
watoto yatima, Sheikh Issa Othman Issa amemshukuru Nsekela na familia
yake pamoja na wafanyakazi wa Benki ya CRDB kwa msaada huo huku
akitanabaisha kuwa kusaidia wasiojiweza wakati wa mfungo wa Ramadhan ni
ibada na kunafungua milango ya baraka.
“Mafundisho ya Mtume SAW yanatuambia atakayemfuturisha aliye na
swaum atapata thawabu kama zake bila ya mwenye swaum kupungukiwa na
kitu. Kwa niaba ya vituo hivi na watoto hawa niwashukuru sana na
Mwenyezi Mungu aendelee kuibariki Benki yetu ya CRDB,” alimalizia Sheikh
Issa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Amani Foundation
for Orphans, Hajjaty-Zubeida Abdallah kilichopo Wilaya ya Kigamboni,
aliishukuru kwa msaada huo akisema umekuwa faraja kwa watoto hao na
utawasaidia kukamilisha funga yao ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan
kikamilifu.
“Mkurugenzi Mtendaji kwa niaba ya vituo hivi nikushukuru sana kwa
msaada huu, nichukue pia fursa hii kuwakaribisha katika vituo vyetu
ilituweze kujadiliana kwa pamoja namna bora ya kuwasaidia watoto wetu
hawa,” alisema Hajjaty-Zubeida.
Vituo vilivyopatiwa msaada huo ni pamoja na Kituo cha Tarbia kilichopo
Wilaya ya KinondonI, Kituo cha Irshad Islamic kilichopo Wilaya ya
Ubungo, Kituo cha Amani Foundation for Orphans kilichopo Wilaya ya
Kigamboni, Kituo cha Hiyari Orphans kilichopo Temeke, Kituo cha Busara
Orphans kilichopo Wilaya ya Ilala.
Kila kituo kimepatiwa Unga wa
Ngano kilo 50, Sukari kilo 50, Maharage kilo 50, Tambi pakiti 30, Tende
pakiti 20, Mafuta lita 20, Njugu kilo 20, Sabuni za Unga za Kufulia Ndoo
5 pamoja na maziwa ya unga makopo makubwa 5 sambamba na majani ya chai
pakiti 10.
No comments:
Post a Comment