TIGO YAUNGANA NA SAMSUNG KUZINDUA SIMU ZA SAMSUNG GALAXY 21 TANZANIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday 14 February 2021

TIGO YAUNGANA NA SAMSUNG KUZINDUA SIMU ZA SAMSUNG GALAXY 21 TANZANIA



Meneja wa bidhaa za intaneti wa Tigo, Mkumbo Muyonga Akiongea na  waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kuzindua simu mpya aina ya Samsung Galaxy S21+ na Samsung Galaxy S21 Ultra katika soko la Tanzania mapema leo katika makao makuu ya Tigo Jijini Dar es salaam.Kulia kwake ni Meneja wa Samsung Tanzania, Suleiman Mohamed.



Meneja wa Samsung Tanzania, Suleiman Mohamed Akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kuzindua simu mpya aina ya Samsung Galaxy S21+ na Samsung Galaxy S21 Ultra katika soko la Tanzania mapema leo katika makao makuu ya Tigo Jijini Dar es salaam.

  • Wateja kupata hadi GB 78 za intaneti bure mwaka mzima

KAMPUNI inayoongoza katika mageuzi ya kidigitali, Tigo Tanzania imeungana na Kampuni ya simu ya Samsung kuzindua simu mpya aina ya Samsung Galaxy S21+ na Samsung Galaxy S21 Ultra katika soko la Tanzania.Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kampuni kuongeza kasi ya matumizi ya mtandao wa 4G hapa nchini.

Meneja wa bidhaa za intaneti wa Tigo, Mkumbo Muyonga akizungumza wakati wa uzinduzi wa simu hizo alisema “Tunafuraha kuwa kampuni ya kwanza ya mawasiliano kupokea na kuuza Samsung Galaxy S21, Samsung Galaxy S21+ na Samsung Galaxy S21 Ultra katika soko la Tanzania.Huu ni uthibitisho wa imani kubwa ambayo wadau wetu wanayo juu yetu kama msambazaji mkubwa, mtandao mkubwa wa 4G, ofa mbalimbali pamoja na timu ya huduma kwa wateja amnbayo inahakikisha wateja wetu wanapata huduma za hali ya juu kila wakati.” 

Aliongeza “Lengo letu ni kuchochea maisha ya kidigitali hapa Tanzania na ndio maana tumeungana na Samsung kuongeza idadi ya watumiaji wa simu janja na mtandao hapa nchini.Tumejizatiti katika kuwawezesha watanzania kupata teknolojia za kisasa zaidi na ndiyo maana tunatoa zaidi ya GB 78 za intaneti kwa mwaka mzima kwa wateja wanaonunua simu za Samsung Galaxy S21+ na Samsung Galaxy S21 Ultra,” alisema Muyonga.

Tigo inaendelea kuchochea ueneaji na utumiaji wa simu janja hapa nchini kwa kuhakikisha wateja wake wanafurahia ulimwengu wa kidigitali kupitia mtandao wenye kasi zaidi wa 4G kutoka Tigo ambao ni mkubwa zaidi hapa nchini.

Akizungumzia muungano huo, Meneja wa Samsung Tanzania, Suleiman Mohamed alisema “Simu hii mpya ya Galaxy S21 5G series imetengenezwa mahususi kwaajili ya kumpa mtumiaji uzoefu wa kipekee zaidi ambao utafanya kila siku kuwa nzuri zaidi.  Galaxy S21 series imeundwa kwa teknolojia za kisasa zaidi zinayoipa uwezo wa kuwa na spidi zaidi pamoja na muonekano wa kipekee,” alisema.

 Kuhusu sifa za simu hizo, Mohammed alisema “Kwa wateja ambao wanahitaji kupata simu zenye ubora wa hali ya juu na camera yenye uwezo mkubwa zaidi kwa bei tofauti tofauti, Galaxy S21 na Galaxy S21+ zinauwezo wa kumpa yote hayo na zaidi. Galaxy S21 itapatikana katika muonekano wa kipekee zaidi kuanzia rangi hadi muonekano wake wa nje wenye kuvutia.

Samsung Galaxy 21 itauzwa kwa Tsh2,269,999 na Samsung Galaxy 21+ kwa Tsh 2,849,999 na Samsung Galaxy 21 Ultra kwa 3,489,000.

Mwisho


No comments:

Post a Comment