Na Prisca Ulomi, WMTH
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile ameiarifu Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuwa kiasi cha shilingi trilioni 18 zinapita kwenye mitandao kwa mwezi wakati wa kikao chake na kamati hiyo kilichohudhuriwa na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara hiyo na wakuu wa taasisi zake ikiwemo Shirika la Posta Tanzania (TPC), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA -CCC) na Tume ya TEHAMA (ICTC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa Bunge, Dodoma.
Dkt. Ndugulile amewaeleza wajumbe wa Kamati hiyo kuwa kiasi cha miamala milioni 300 inafanyika kwa mwezi mtandaoni na Serikali inapata shilingi bilioni 80 kwa mwezi za tozo kutokana na fedha zinazopita mtandaoni na mzunguko huo wa fedha mtandaoni kwa mwezi, miamala inayofanyika na tozo ambazo Serikali inapata ni kutokana na kuwepo kwa matumizi ya TEHAMA .
Amefafanua kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni njia kuu ya uchumi na inawezesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano yenye kasi, kufanikisha utendaji kazi wa mifumo ya TEHAMA na huduma za fedha mtandaoni ambapo Wizara imejipanga kuandaa ramani ya njia ya miundombinu huo ili kufanikisha mwingiliano wa ujenzi na upanuzi wake pale inapokutana na njia za miundombinu mingine kama vile ya barabara, maji, umeme na reli.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Moshi Kakoso ameitaka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuongeza udhibiti na usimamizi wa huduma za mawasiliano kwenye suala la fedha mtandao ili kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha na kuweza kuongeza mchango wa tozo Serikalini zaidi ya shilingi bilioni 80 kwa mwezi kwa kuwa miamala mingi ya fedha inafanyika na fedha nyingi zinapita kwenye mtandao ili TEHAMA iongeze mchango wake kwenye ukuaji wa uchumi na kuchangia zaidi pato la taifa .
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa Wizara itaipa ushirikiano wa kutosha Kamati hiyo ili kwa pamoja Serikali kupitia Wizara hii na Bunge kupitia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu waweze kutekeleza majukumu yao kwa kuwa wote kwa pamoja wanamhudumia mwananchi.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amewaeleza wajumbe wa Kamati hiyo kuwa Wizara itaendelea kusimamia na kuendesha vema Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kunufaika na huduma za mawasiliano na TEHAMA inatumika kurahisisha maisha yao ya kila siku katika nyanja ya kiuchumi na kijamii.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
No comments:
Post a Comment