Na Eleuteri Mangi, Dodoma
NENO kumbukizi ni nomino lenye maana ya maadhimisho ya kukumbuka na kuenzi matendo au jambo lililofanywa na mtu enzi za uhai wake.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi Januari 21, 2021 aliwaongoza Wajumbe wa Menejimenti ya wizara pamoja na Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara kusimama mara baada ya kufungua kikao kwa heshima ya kumbukizi ya aliyekuwa Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Marehemu Godfrey Mngereza aliyefariki Desemba 24, 2020.
Marehemu Mngereza alikuwa mjumbe katika vikao vya Menejimenti ya Wizara kinachojumuisha watendaji wakuu wa wizara pamoja na wakuu wa taasisi ambao jukumu lao ni kujadili masuala mbalimbali ikiwemo utendaji na utekelezaji yao ya kila siku, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi pamoja na bajeti ya Wizara kwa kila mwaka wa fedha.
Katika ufunguzi wa kikao hicho Dkt. Abbasi alisema “Hiki ni kikao cha kwanza tangu amefariki mmoja wa wajumbe wa kikao hiki ndugu yetu Marehemu Godfrey Mngereza ni vema tusimame kwa dakika moja kumkumbuka mwenzetu, apumzike kwa Amani.”
Hakika kifo cha Marehemu Mngereza sio simanzi tu kwa familia, bali hata kwa taasisi aliyokuwa anaiongoza BASATA, Wizara yenye dhamana na tasnia ya Sanaa, wasanii na wadau wote wa tasnia ya Sanaa nchini, ndugu, jamaa na marafiki.
Kufuatia kifo chake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Wizara alisema alisema “Kwa muda mrefu tumekuwa mashuhuda wa namna Mngereza alivyosimamia maslahi ya kazi za Sanaa na wasanii, hakuwa mtu wa kukaa ofisini tu, alizunguka kwenye matukio yote muhimu yanayoihusu Sanaa yawe yameandaliwa na Serikali, taasisi kubwa au hata wasanii wa kawaida. Alikuwa mwepesi wa kutoa ushauri na nasaha mara kwa mara. Ni pigo tumepoteza mtu muhimu sana”.
Mwili wa marehemu Mngereza uliagwa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam Desemba 29, 2020 na kuzikwa kijiji cha Suji wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro Desemba 30, 2020.
Hakika Marehemu Mngereza atakumbukwa kwa umahiri wake mkubwa wa kuisimamia Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa ya mwaka 1984 na Kanuni zake na uwezo wake wa kusimia maadili katika kazi za Sanaa pamoja na kuifahamu sekta kwa mapana yake hatua iliyosaidia kukuza maendeleo na utengenezaji wa kazi za Sanaa nchini zenye kujali ubora na maadili.
No comments:
Post a Comment