Meneja Mwandamizi Biashara za Serikali wa Benki ya NMB, Adelard Mang'ombo akizungumza wakati wa Mkutano wa Jumuia ya makampuni ya waongoza watalii Zanzibar. NMB ilidhamini mkutano mkuu wa mwaka. |
BENKI ya NMB imesema kuwa imejipanga na kukusudia kuhakikisha inashirikiana na serikali katika kuona sekta ya utalii inakidhi mahitaji ya uchumi wa taifa letu, ikiwa pamoja na kukuza Sekta ya Utalii ambayo imekuwa tegemeo kubwa la uchumi.
Benki hiyo imebainisha kuwa na mtaji wa kutosha na imejitolea kutumia Wataalamu wake kuona mfumo wa uendeshaji wa Sekta ya Utalii kupitia Teknolojia ya kisasa ya Mawasiliano unakwenda kwa kasi na kuleta matumaini makubwa hasa visiwani Zanzibar.
Hayo yamesemwa na Meneja Mwandamizi Biashara na Serikali wa NMB Adelard Mang'ombo katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Makampuni ya waongoza misafara ya Watalii Zanzibar (ZATO) uliofanyika Zanzibar. Adelard alisema kuwa, NMB inatambua kuwa uchumi wa Zanzibar unategemea sana shughuli za utalii, ambapo kama Benki kubwa nchini imejipanga kuhakikisha uchumi huo unaendelea kukua na kuwaletea wazazibar maendeleo.
“Benki yetu ina mtaji mkubwa, kupitia mafanikio haya, tunaona kuna umuhimu wa kuungana na Serikali na tumekusudia katika hilo, kuhakikisha tunashiriki na sisi katika kukuza uchumi wa nchi kupitia Sekta ya Utalii,” alisema Mang’ombo.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Biashara za Kadi Benki ya NMB - Philbert Casmir, alisema NMB imekusudia kutoa ushirikiano mkubwa kwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ili kuhakikisha inasaidia kukusanya mapato na kujenga uchumi. Alisema Benki hiyo inaamani kuwa uwezo wake katika kukusanya mapato yanayohusu Sekta ya Utalii, itasaidia kwa kiasi kikubwa kukusanya mapato na kupelekea kufikia lengo la uchumi wa buluu.
Kuhusu uchumi wa bluu, Casmir alisema kuwa Benki ya NMB imejipanga kushirikiana na serikali kutimiza maono yake kwenye uchumi wa bluu na tayari wameanza kwa vitendo kwa kuzindua jukwaa la biashara linalowezesha wafanyabiashara kufanya miamala kupitia tovuti zao (E-Commerce Platform).
Aidha alisema kuwa wamewezesha matumizi ya kadi za malipo za UnionPay na sasa inakubalika katika kufanyia miamala kwenye mashine za kutolea fedha (ATM) na zile za kufanyia manunuzi (POS) za NMB, lengo likiwa kuleta huduma bora kwa wafanyabiashara waliopo kwenye Sekta ya Utalii.
Maafisa wa Benki ya NMB Tawi la Zanzibar, wakimwelezea Kamishna wa Uhamiaji - Jecha Makame Issa kuhusu bidhaa na huduma za Benki hiyo. |
No comments:
Post a Comment