Na Eleuteri Mangi na Jonas Kamaleki- MAELEZO, Dodoma
MAANDALIZI ya hafla ya
kumwapisha Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe
Magufuli itakayofanyika Novemba 5, 2020 katika Uwanja wa Jamhuri jijini
Dodoma yamekamilika.
Kauli hiyo imetolewa
leo jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na
Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi mara baada ya viongozi
kukagua uwanja huo utakaotumika kwa hafla ya kitaifa ya kumwapisha Rais Mteule
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa mara ya kwanza
kiapo cha Rais kinafanyika hapa Dodoma, ni jambo la kihistoria ambalo wananchi
wanapaswa kulifahamu. Uwanja wa Jamhuri Dodoma upo tayari kwa ajili ya shughuli
ya kesho maandalizi yote yamekamilika”, amesema Dkt. Abbasi.
Katika kufanikisha
shughuli hiyo, Dkt Abbasi amesema kuwa nchi yetu itapokea ugeni mkubwa ambao
utashiriki kwenye kiapo cha Mhe. Rais Mteule, Dkt. Magufuli ambapo watakuwepo
viongozi wakuu wa nchi au wawakilishi wa wakuu hao wapatao 20 ambao
wamethibitisha kushiriki.
Marais ambao
wamethibitisha kuwepo kwenye hafla hiyo ni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni,
Rais wa Comoro Azali Assoumani na Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa.
Viongozi wengine ambao
wamethibitisha kushiriki ni ni pamoja na
Mawaziri Wakuu, Makamu wa Rais wa nchi mbalimbali za Afrika, Waziri wa Mambo ya
Nje wa Qatar ambaye atamwakilisha Mfalme wa huko.
Aidha, Rais Mstaafu wa
Nigeria Olusegun Obasanjo na Nabii TB Joshua watashiriki pamoja na mabalozi
83 wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini
Katika hafla hiyo
watashiriki pia viongozi waandamizi wa Serikali wakiwemo Makatibu Wakuu,
Manaibu Katibu Wakuu, viongozi wa taasisi za umma na binafsi, viongozi wa siasa,
viongozi wa dini pamoja na Mawaziri na Manaibu Mawaziri wanaomaliza muda wao.
Fauka ya hayo, Dkt.
Abbasi amesema kuwa viongozi wote walioalikwa ambao wana kadi za mwaliko,
magari yao yatapaki Bustani ya Chinangali karibu na uwanja wa ndege wa Dodoma
ambapo watapanda mabasi kuwapeleka eneo la tukio.
Hafla hiyo itakuwa na
sehemu mbili ambapo kutakuwa na gwaride la kiapo litaongozwa na majeshi ya
ulinzi na usalama na sehemu ya burudani ambayo itawashirikisha wasanii
mbalimbali nchini ikizingatiwa Tanzania ni nchi ya amani na ni siku ya furaha.
No comments:
Post a Comment