Mtafiti wa mradi huo, Profesa Ntengua Mdoe akifafanua kuhusu kilimo biashara cha mpunga, mifugo na hali maisha ya wakulima wadogo katika Bonde la Kilombero kwenye warsha hiyo.
Mtafiti wa mradi huo, Dk.Devotha Kilave akitoa mada kuhusu wanawake wanavyoshiriki shughuli za kilimo.
Mtafiti wa Mradi huo,Dk.Christopher Magomba akifafanua jambo kwenye warsha hiyo.
Mtafiti wa Mradi huo,Profesa Gilead Mlay akishiriki kufafanua mambo kwenye warsha hiyo.
Mtafiti Msaidizi wa mradi wa mradi huo, Gideon Boniface akitoa mada kuhusu athari walizopata wakulima kipindi cha ugonjwa wa Covid-19. |
Picha ya pamoja waandishi wa habari na watafiti wa mradi huo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).
Na Dotto Mwaibale, Morogoro
MABADILIKO ya Maisha na Uchumi wa Mkoa wa Singida imeelezwa hayatokani na kilimo cha alizeti pekee bali na mazao mengine pamoja na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Hayo yameelezwa na watafiti ambao walifanya utafiti katika Mkoa wa Singida kubaini ukweli wa nini kilichoufanya mkoa huo kuwa na maendeleo ya kiuchumi baada ya kuwepo kwa dhana ya wananchi kwamba kilimo cha alizeti ndicho kimeupaisha mkoa huo kimaendeleo.
Mtafiti Dk. Christopher Magomba akiwasilisha mada mkoani hapa juzi ya utafiti huo kwa waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kwenye warsha ya siku moja iliyoandaliwa na Mradi wa Utafiti wa Sera za Kilimo Barani afrika (APRA) iliyolenga kutoa matokea ya utafiti wao kwa jamii alisema kilimo cha mazao mengine na shunguli zingine za kiuchumi, vyanzo mbadala na miradi midogo midogo inayofanywa na kaya nayo imechangia kuinua uchumi wa mkoa huo.
Akitolea mfano kilimo cha mahindi ambacho ni asilimia 83.86 ni moja ya zao ambalo linaonesha kuchangia maendeleo mkoani humo ukilinganisha na alizeti ambalo katika utafiti wao walioufanya Wilaya ya Iramba na Mkalama lilionesha kuwa na asilimia 71 tu.
Magomba alitaja mazao mengine ambayo yameonesha kufanya vizuri na kuongeza kipato katika mkoa huo kuwa ni vitunguu, nyanya, mtama pamoja na pamba.
Katika hatua nyingine Watafiti hao kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA ) ambao wapo kwenye mradi wa APRA katika utafiti wao wamebaini kuwa vijana hasa wa kiume ndio wanaonufaika zaidi na Kilimo Biashara cha Mpunga Bonde la Kilombero ijapokuwa wanachangamoto ya mitaji na kukosa mashamba binafsi.
Akiwasilisha mada kuhusu matokeo ya utafiti wake uliohusu ushiriki wa vijana kwenye kilimo biashara cha mpunga kwenye Bonde la Kilombero Profesa Ntengua Mdoe alisema vijana wenye umri kati ya miaka 15-35 ambao ni sawa na asilimia 35.5% ya watu ndio wenye kunufaika zaidi katika bonde hilo ukilinganisha na makundi mengine.
"Utafiti wetu umebaini sio kweli vijana hawashiriki kwenye shughuli za kilimo wanashiriki na wanafanya vizuri kwenye kilimo biashara cha mpunga pamoja na kwenye mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo katika maeneo mbalimbali."alisema.
Alisema kwenye Utafiti huo wamebaini kuwa kipato wanachokiota vijana kwenye nguvu wanayowekeza kwenye kilimo ni kikubwa kuliko nguvu inayowekezwa na vijana wanaofanya kazi zingine hapa nchini.
“Ukiangalia kwenye Utafiti tumebaini kuwa nyumba nyingi zinazoongozwa na vijana zina uhakika mkubwa wa chakula kuliko kaya ambazo zinaongozwa na wazee na watu wenye umri mkubwa na hii ni kutokana na mafanikio makubwa wanayoyapata kutoka kwenye kilimo.” alisema Mdoe.
Katika mapendekezo ya utafiti huo wametoa ushauri kwa Halmashauri na Serikali za Mitaa kutenga ardhi ya kilimo kwa ajili ya vijana kama ambavyo imeelekezwa kwenye sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999 lakini pia kuwasaidia mikopo kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana wa asilimia 4% kwenye mapato ya halmashauri.
Mdoe alisema wanatoa ushauri kwa Halmashauri za Wilaya kwa kushirikiana na wadau wengine wa kilimo kuwawezesha vijana kupata elimu ya kilimo bora kupitia mafunzo ili kuongeza tija zaidi na kuachana na kilimo cha mazoea.
Akitoa ufafanuzi wa maswali mbalimbali ya wanahabari Mkuu wa Mradi huo wa APRA upande wa Tanzania Profesa Aida Isinika alisema vijana wengi wanapenda kilimo chenye tija na soko kama vile kilimo cha mpunga, vitunguu, nyanya na mazao mengine.
“ Vijana hawataki mazao ya muda mrefu maana sio wavumilivu sana wao wanahitaji matokeo ya muda mfupi ndio maana unaona wengi wanakimbilia mazao hayo ambayo wanatumia muda mfupi kupata fedha.” alisema Isinika.
Aidha Isinika alisema mitaji wanayohitaji vijana ni midogo midogo na sio mikubwa hivyo wakiwezeshwa kupata itawasaidia katika kufanya shughuli za kilimo kwa urahisi na kuongeza tija huku wakiboresha maisha yao.
Akizungumzia utoaji wa ajira katika mashamba hayo alisema kundi la wakulima wa kati ndio waliotoa ajira nyingi kwa vibarua ukilinganisha na wawekezaji wakubwa na kusema kuwepo kwa nishati ya umeme katika maeneo yalipo mashamba hayo kumechochea maendeleo.
No comments:
Post a Comment