Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi akizungumza na wanahabari juu ya utabiri wa mvua za msimu kwa miezi ya Novemba, 2020 hadi Aprili, 2021 kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka. |
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa mvua za msimu kwa miezi ya Novemba, 2020 hadi Aprili, 2021 kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, huku ikionesha mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Dodoma, Singida, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa, Lindi, Mtwara, kusini mwa mkoa wa Morogoro na mashariki mwa mikoa ya Tabora na Katavi.
Aidha, akitoa utabiri huo kwa wanahabari Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi amesema kwa maeneo ya mikoa ya Kigoma, Rukwa pamoja na magharibi mwa mikoa ya Tabora na Katavi yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, huku akibainisha uwepo wa vipindi vya mvua nyingi katika miezi ya Januari na Aprili 2021.
Aliongeza kuwa mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba, 2020 kwa maeneo ya mkoa wa Tabora na kutawanyika katika mikoa mingine inayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka katika wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2020.
"...Mvua zinatarajiwa kuisha katika maeneo mengi ya magharibi, kati, nyanda za juu kusini magharibi na pwani ya kusini katika wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2021, hata hivyo, kwa mkoa wa Ruvuma mvua zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Aprili, 2021.
Hata hivyo aliongeza kuwa, hali ya unyevunyevu ardhini inatarajiwa kuwa ya kuridhisha kwa ajili ya kilimo na malisho katika maeneo mengi hivyo kuwatoa wasiwasi wakulima na wafugaji.
Alieleza kuwa, pamoja na hali hiyo, kutakuwepo na matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza kusababisha mafuriko na kupelekea uharibifu wa miundombinu, upotevu wa maisha na mali. Magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na kutuama kwa maji machafu na uchafuzi wa maji safi hivyo kutoa tahadhari kwa jamii.
Aidha alisema msimu wa vuli kwa miezi ya Oktoba hadi Disemba 2020 katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani (ikijumuisha kisiwa cha Mafia) pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) unatarajiwa kuendelea kama ilivyotabiriwa hapo awali ambapo maeneo mengi yalitarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani.
Aidha, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa katika mwezi Januari 2021, huku mvua za wastani hadi juu ya wastani zikitarajiwa katika maeneo mengi ya nyanda za juu kusini magharibi, kanda ya kati pamoja na Pwani ya kusini. Aidha, maeneo ya magharibi yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Hata hivyo, mvua nyingi zinatarajiwa kunyesha katika nusu ya pili ya msimu.
Kwa Kanda ya Magharibi, Mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa kunyesha katika mkoa wa Kigoma pamoja na magharibi mwa mikoa ya Tabora na Katavi. Mashariki mwa mikoa ya Tabora na Katavi mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.
Mvua hizi zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba, 2020 katika mikoa ya Tabora na Katavi na kusambaa kusini mwa mkoa wa Kigoma katika wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2020. Mvua hizo zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2021.
No comments:
Post a Comment