DK. JOHN POMBE MAGUFULI SEKONDARI YAZINDULIWA ZANZIBAR - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday 10 October 2020

DK. JOHN POMBE MAGUFULI SEKONDARI YAZINDULIWA ZANZIBAR

Rais Dk. John Pombe Magufuli.


Na Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

RAIS  wa Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wazee kuendelea kusimamia malezi ya watoto wao, wakati huu vitendo vya Unyanyasaji wa kijinsia vikiwa vimeshamiri hapa nchini. Dk. Shein ametoa wito huo katika hafla ya ufunguzi wa Skuli ya sekondari Mwanakwereke mpya, ambayo hivi sasa inatambulika kwa jina la ‘Skuli ya Sekondari ya Dk. John Pombe Magufuli.


Amesema vitendo  vya udhalilishaji wa kijinsia ambavyo hivi sasa vimeshamiri sio sifa ya Wazanzibari, hivyo akawataka wazee kote nchini kutoiachia serikali pekee jukumu la  kukabiliana na uhalifu huo na badala yake kushirikiana nayo.


“Hali hii ni lazima tushikamane katika kupambana na wahalihu hao…”,a lisema.


Alieleza kuwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto wadogo, ikiwemo wanafunzi vimekuwa vikifanywa  kwa makusudi, huku familia zinazoathirika zikiwaficha wahalifu wanaohusika na vitendo hivyo.


Dk. Shein alisema anaunga mkono kikamilifu azma ya Mgombea wa kiti cha Urais wa  Zanzibar kupitia CCM Dk. Hussein Mwinyi ya kuchukua hatua kali  katika kukabiliana na vitendo hivyo. Alibainisha kuwepo matatizo ya kibinadamu, kiutawala na katika hulka za Wazanzibari katika ushughulikiaji wa vitendo hivyo.


“Mambo yanayofanyika katika jamii yetu ni mabaya sana...kuna kaumu zilizopita zilipata hukumu mbali mbali kutokana na vitendo vyao viovu”, alisema.


Rais Dk. Shein alisema Serikali inaendelea na juhudi za kuweka mazingira bora ya kielimu ili kupata wataalamu wazalendo na ndio maana skuli zinazojengwa kama hiyo zimekuwa na  maabara za aina tofauti.


Alitowa wito kwa wanafunzi kusoma kwa bidii, huku serikali ikiendelea na jukumu lake la kuweka mazingira bora, ikiwemo kufanikisha dhana ya elimu bila malipo na kubainisha azma ya serikali ya kutoa elimu bure hadi kidato cha sita kadri uchumi utakavyoendelea kukua. Alisema Marehemu mzee Karume aliikomboa Zanzibar na hivi sasa mambo yote ya maendleeo yanafanywa na wananchi wenyewe.


“Nyinyi wanafunzi kazi yenu kusoma, serikali yenu iko pamoja nanyi na walimu nanyi somesheni kwa kutengeneza sio kuripua na wazee simamieni maendeleo ya elimu ya watoto wenu...”, alisema.


Katika hatua nyengine, Dk. Shein alipinga hoja zinazotolewa na baadhi ya watu kuwa kiwango cha elimu kimeshuka nchini, na badala yake akasema kumekuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu vizuri katika masomo yao, sambamba na kufahamu kuzungumza lugha za kigeni, hususan Kiingereza.


Alisema walimu wanasomesha vizuri na bila ubaguzi huku idadi ya wanafunzi wanaohitimu  idadi  imekuwa ikiongezeka kutokana na ongezeko kubwa la wananchi kuzaliana kwa wingi.


“Kipimo cha elimu Zanzibar hakijashuka kuna wanafunzi wapatao 124 wa kidato cha sita ambao wamepata Divisheni ya kwanza, huku divisheni ya nne ikipungua na divisheni zero kufutika kabisa….”, alisema.


Alisema mafanikio hayo yanachangiwa kutokana na mambo tofauti ikiwemo kiwango kikubwa cha Bajeti ya Fedha ya Wizara hiyo mwaka huu kinachofikia shilingi Bilioni 178, jambo ambalo kabla halikupata kutokea.


Aidha, Rais Dk. Shein kwa niaba ya ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  Dk. John Pombe Magufuli, alikubali ombi  la Uongozi wa Wizara Elimu na Mafunzo ya Amali na kubariki skuli hiyo kuitwa jina la kiongozi huyo  pamoja na kukubali skuli ya Sekondari Wingwi kuitwa jina lake (Dk. Ali Mohamed Shein).


Mapema, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, alisema Wizara hiyo itaendelea kusimamia maendeleo ya elimu nchini na kuhakikisha ubora wa elimu unasimamia vizuri.


Nae, Katibu Mkuu wa Wizara Elimu na Mafunzo ya Amali, Eng. Dkt. Idrissa Muslim Hijja alisema  hadi kufikia mwaka 2010 Zanzibar ilikuwa na jumla ya skuli 10 za Sekondari za Ghrofa, ikiwemo Lumumba, Haile Sellasie, Ben-bella, Hamamni, Forodhani,Tumekuja,Uweleni,Kiponda,Hurumzi na Mwanakwerekwe ‘C’.


Alisema katika kipindi cha miaka kumi ya Uongozi wa Awamu ya saba chini ya Dk. Ali Mohamed Shein, jumla ya skuli 26 za Sekondari za ghrofa zimejengwa nchini kote. Alieleza kuwa ufunguzi wa skuli hiyo sambamba na Skuli ya Sekondari Wingwi kisiwani Pemba, zinakamilisha jumla ya skuli 26 za Sekondari za ghorofa zilizojengwa katika Awamu ya saba.


Alisema Skuli hiyo iliyojengwa kupitia mradi wa Zanzibar Improving Students Prospects (ZISP) umegharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia  mkopo wa Benki ya Dunia kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 2.6 hadi kukamilika kwake.


Alisema lengo la mradi huo ni kuimarisha ubora wa elimu katika masomo ya Sayansi na Hesabati ngazi ya Sekondari na kuwapatia mafunzo ya somo la kiingereza walimu wote wanaosemesha somo la Sayansi.


Aidha, alisema Kampuni ya Ujenzi ya CRJE kutoka nchini China ndio iliojengwa skuli hiyo,chini ya usimamizi wa kampuni ya ‘Digital Space Consultancy’.


Katika hafla hiyo viongozi mbali mbali wa kitaifa walihudhuria , akiwemo Mgombea wa kiti cha Urais wa Zanzibar kupitia CCM Dkt. Hussein Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Abdalla  Sadalla,Mawaziri pamoja na wanafunzi. 



No comments:

Post a Comment