MKUU wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi 638,979 wa vijiji vyote 339, Mitaa 167, Kata 96, Tarafa 16, Halmashauri 4 na Wilaya 3 Mkoani Rukwa walioandikishwa kwaajili ya kupiga kura, kujitokeza katika kupiga kura katika uchaguzi mkuu utaofanyika siku ya Jumatano ya tarehe 28 mwezi Oktoba mwaka huu ili kuwachagua Madiwani, Wabunge Pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, Mh. Wangabo ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha wakulima kuwa katika kipindi hiki cha Kampeni wasisahau kuandaa mashamba yao kwaajili ya msimu wa kilimo wa mwaka 2020/2021 na kusisitiza kuwa wananchi wasiegemee sana siasa wakasahau Maisha ya kawaida ambayo ni kilimo kwa wananchi wengi wa mkoa wa Rukwa.
“Wakati huo huo vyote lazima viende Pamoja na maandalizi ya kilimo, si mvua karibu zinanyesha, ni lazima watu wakaandae mashamba yao, tusiegemee sana siasa tukasahau pia kuna Maisha ya kawaida kwetu sisi ni kilimo, kwahiyo ni lazima tuandae mashamba mapema, uchaguzi unapopita mvua zikinyesha tunakwenda kupanda, mvua za kwanza ni za kupandia, kwahiyo vyote tuvibebe, tumeelewana,” Alisistiza.
Mh. Wangabo ameyasema hayo leo tarehe 22.9.2020. alipotembelea miradi ya Lipa kulingana na Matokeo (EP4R) na Miradi ya Afya na Usafi wa Mazingira (SWASH) inayotekeleza ujenzi wa madarasa na vyoo vya wananfunzi kwa shule za msingi na Sekondari Wilayani Kalambo ambapo wilaya hiyo imepokea jumla ya Shilingi 529,679,504 kwa mwaka huu wa fedha ili kutekeleza miradi hiyo.
Awali wakati akisoma taarifa ya miradi hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo Eric Kayombo alisema kuwa Shilingi 353,900,000 ilipokelewa katika shule saba za msingi kwaajili ya ujenzi wa madarasa na vyoo na Shilingi 175,776,504 ilipokelewa katika shule nyingine 7 za msingi kwaajili ya ujenzi wa vyoo.
“Mheshimiwa Mkuu wa mkoa utekelezaji wa miradi hii umeanza mwaka huu wa fedha 2020/2021 badala yam waka 2019/2020 hii ni kutokana na halmashauri kupokea fedha za miradi mwishoni mwa mwaka wa fedha 2019/2020 na kufanya kuvuka mwaka na kuanza kutekeleza mwaka huu wa fedha, Miradi ya EP4R ipo katika hatua za msingi na miradi ya afya na usafi wa mazingira ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji,” Alisema.
Mh. Wangabo ametoa miezi miwili kwa halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kuhakikisha wanamaliza miradi hiyo kwa shule za msingi na sekondari ili kuimarisha miundombinu ya shule hizo ambazo iradi hiyo inatekelezwa ikiwemo shule ya sekondari ya Wasichana Matai ambayo inatarajiwa kuanza kupokea wananfunzi kuanzia mwaka 2021.
No comments:
Post a Comment