WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Halmashauri ya Buchosa – Sengerema wametakiwa kuondoa tofauti zao na kivunja makundi haswa katika kipindi hichi wanapoelekea katika uchaguzi mkuu ili kukiwezesha chama hicho kupita kwa kishindo.
Hayo yamebainishwa na mgombea Ubunge Jimbo la Buchosa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eric Shigongo James alipokuwa akizungumza na Makatibu wa chama hicho na wagombea Udiwani CCM wa jimbo hilo kabla ya kuanza kampeni zake rasmi zinazotarajiwa kuzinduliwa Septemba 25, 2020 Mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Mjumbe wa kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Shigongo alisema kuwa katika kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni vyema wanachama na viongozi wa CCM kuvunja makundi yaliyokuwepo wakati wa kampenzi za kura za maoni na iwapo kuna ambao wametofautiana kwa namna yoyote, basi ni vyema wapatane na waungane katika kukiletea CCM ushindi katika uchaguzi ujao wa Rais, wabunge na madiwani.
“Ndugu zangu kama mimi na Dkt. Tizeba hatuna tofauti zetu, tulifungana kura za maoni lakini chama kikaniteua mimi kupeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi ngazi ya ubunge Buchosa, iweje kwenu ninyi madiwani mtengeneze makundi?
“Nawaombeni muondoe tofauti zenu kwani uchaguzi ndani ya chma chetu ulikwisha hivyo tuunganishe nguvu zetu katika kukipigania chama ili kiweze kuibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, 2020,” alisema Shigongo.
“Ninachowaomba ninyi madiwani, Makatibu wa Chama sasa tumemaliza kura za maoni zinaweza kuwa zilitugawanya gawanya hebu tuyasahau sasa CCM ni kimoja, nawaombeni muoneshe umoja, nguvu ili tuweze kumtafutia Mhe. Rais wetu mpendwa kura za kishindo katika jimbo letu, kwani mkifanya hivyo itatuletea heshima kubwa ndani ya CCM,” aliongeza Shigongo.
Kwa upande wake anayegombea udiwani kata ya Kasisa, Jasho Kabika ameomba kama kuna aliokwazana nao wamsamehe kwani kura za maoni ndani ya chama zilikwisha na anayemtambua kupeperusha bendera upande wa Ubunge ni Shigongo na si mwingine.
“Mbunge ni Shigongo, na wananchi wa Buchosa wote wanayemtambua kugombea ubunge Buchosa ndani ya Chama Chetu ni Shigongo, ushindi utakuwa asilimia 100 ndani ya chama chetu kwa upande wa udiwani, ubunge na hata urais,” alisema, Jasho Kabika, mgombea udiwani wa Kata ya Kasisa.
No comments:
Post a Comment