Mawakala kutoka Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam wakiwa katika mafunzo ya jinsi wanavyoweza kuzuia utakatishaji fedha. |
BENKI ya NMB imetoa mafunzo maalum kwa mawakala wake kuhusiana na namna ya kuzuia utakatishaji fedha; na pia mbinu za kuzuia kufadhili shughuli za kigaidi.
Mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam na Arusha, ni utekelezaji wa maagizo ya Benki Kuu (BoT) kuhakikisha mawakala wa benki hawawi sehemu ya kutakatisha fedha zinazopatikana kwa njia zisizo halali.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, Meneja Mwandamizi wa NMB Kitengo cha Wakala - Bw. James Manyama alisema ili mawakala hao kutotumika vibaya hawana budi kuzingatia sheria na kanuni za fedha zinazosimamiwa na Benki Kuu ili kushirikiana na Serikali katika kukomesha vitendo hivyo.
Christine Mwidunda, akitoa mafunzo kwa Mawakala jijini Arusha. |
“Ni wajibu wetu kama Benki kuwaelimisha mawakala wetu kuwa makini wakati wote hasa kwa wateja ambao wameshajenga ukaribu na mazoea nao. Pia ni muhimu kuwa makini na wateja wanaoweka fedha nyingi na kisha wanazitoa ndani ya muda mfupi, na ukiangalia kiasi hicho cha fedha wanachoweka hakiendani na maisha yao. Inapotokea hali hiyo wanapaswa kutoa taarifa sehemu husika,” alisema James.
Christine Mwidunda, ambaye ni Meneja wa Mawakala NMB, alisema vyanzo vya fedha haramu ni kama vile ukwepaji wa kodi, biashara zilizopigwa marufuku zikizemo dawa za kulevya, usafirishaji wa silaha na binadamu, ugaidi na utekaji n.k.
Mawakala wakiwa na vyeti walivyopewa baada ya kuhitimisha mafunzo ya namna gani wanaweza kuzuia utakatishaji fedha. |
Mmoja wa Mawakala wa NMB-Monica Temu alisema mafunzo hayo yamewapa maarifa sahihi ya kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu huku wakiwa wanafahamu mipaka ya kazi na namna ya kutilia mashaka wateja wanaotumia mawakala kutakatisha fedha zao jambo ambalo pia lingeweza kuwaweka katika wakati mgumu na mamlaka za nchi.
Benki ya NMB Imepanga kutoa mafunzo haya kwa mawakala wake wote 7700 ambao wametapakaa nchi nzima ifikapo mwezi Oktoba, 2020.
No comments:
Post a Comment