DK. SHEIN AIPONGEZA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 13 August 2020

DK. SHEIN AIPONGEZA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI

Dk. Ali Mohamed Shein.

Na Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameupongeza Uongozi na watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kazi nzuri  waliyofanya katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake.


Dk. Shein ametowa pongezi hizo Ikulu Jijini Zanzibar, alipokutana na Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali wakati ilipowasilisha taarifa ya Utekelezaji ya Mpango kazi kwa mwaka 2019/2020 na Mpango kazi wa mwaka 2020/2021, ambapo pia Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd alishiriki.


Amesema Wizara hiyo yenye Idara na taasisi kadhaa zinazotegemeana imepata mafanikio makubwa katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.


Katika nasaha zake, Dk. Shein aliwataka viongozi na watendaji wa Wizara hiyo kuendeleza juhudi  zilizofanikisha mafanikio hayo, na kubainisha kuwa zimeleta sifa na manufaa makubwa kwa Taifa na wananchi wake.


Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana, kuwa wamoja na  kupendana, ili ujio wa uongozi mpya uweze kuchochea kasi ya maendeleo. 


Dk. Shein aliutaka Uongozi wa Wizara hiyo kukaa na kufikiria njia ya kupata fedha kupitia mashirika mbali mbali ya Kimataifa kama vile Benki ya Dunia na ADB ili kuweza kuanzisha jengo  jipya na la kisasa kwa ajili ya Huduma za Maktaba litakaloweza kukidhi mahitaji ya wakati.


Aidha, aliiunga mkono azma ya Idara ya Huduma za Maktaba ya kuwa na maktaba katika kila Wilaya za Unguja na Pemba, kazi iliyoanza  utekelezaji wake katika Wilaya ya Kati Unguja. 


Aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kuwatumia wana taaluma Wazalendo waliobobea katika masuala mbali mbali ya kielimu yanayohitaji ushauri, badala ya kazi za namna hiyo kuzitangaza kwa wataalamu kutoka nje ya nchi.


Dk. Shein alitaka kufanyika juhudi za kuifanyia matengenezo Skuli ya Mkunazini kwa kufuata miongozo ya Mamlaka ya Mji Mkongwe, ili kuepuka athari zitakazojitokeza za kuanguka kwa jengo hilo  na kuleta maafa.


Aliukumbusha uongozi wa Wizara hiyo umuhimu wa kuufufua Uwanja wa michezo  uliopo Skuli ya Sekondari Lumumba kwa kupanda majani ili uweze kutumika katika mashindano mbali mbali ya skuli za Sekondari, jambo ambalo zamani lilikuwa likifanyika. 


Nae, Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali idd, alisema kumekuwepo maktaba za aina mbali mbali, hivyo akautaka uongozi wa Idara ya Huduma za Maktaba kufanya juhudi za kuwahamasisha wananchi na wanafunzi kutumia maktaba ziliopo ili kupanua wigo wa uwelewa.


Aidha, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza Wizara hiyo kwa hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa, na kuutaka uongozi wa Wizara hiyo kuyalinda na kuyaendeleza mafanikio hayo.


Vile vile aliutaka Uongozi wa Wizara hiyo kusimamia utendaji bora wa kazi kwa watumishi katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi mkuu, sambamba na kuondokana na matumizi mabaya ya mali na rasilimali za serikali , ikiwemo uuzaji wa mali zake, hususan magari.

 

Mapema, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma,  alisema katika kipindi hicho Wizara hiyo imepata mafanikio makubwa ya kuimarisha  sekta ya Elimu, hatua  iliyotokana na juhudi kubwa za Serikali ya Awamu ya saba, chini ya Uongozi wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein.


Aliyataja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na  ongezeko la Ufaulu wa watahiniwa  katika mitihani ya Taifa ya Kidato cha nne (F.IV) mwaka 2019 kwa daraja la kwanza, la pili na daraja la tatu.


Alisema ufaulu kwa watahiniwa wa daraja la kwanza uliongezeka kutoka watahiniwa 185 mwaka 2018 hadi watahiniwa 299 mwaka 2019, huku ufaulu wa watahiniwa wa daraja la pili ukiongeka kutoka 903 (2018) hadi watahiniwa 1,509 (2019).


“Watahiniwa  2,205 walifaulu  katika daraja la tatu kwa mwaka 2018 na kuongezeka hadi watahiniwa 2,915 mwaka 2019”, alisema.


Alisema Wizara hiyo ilifanikiwa kuajiri walimu 665, wakiwemo walimu 216 wa Sayansi, mwalimu mmoja wa masomo ya Ufundi pamoja na walimu 448 wa masomo ya Sanaa na Mkutubi. 


Aidha, alisema pamoja na mafanikio yaliopatikana, Wizara hiyo ilikabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo ongezeko kubwa la wanafunzi wanaoandikishwa kuanza madarasa ya maandalizi na msingi, ikiwa hali tofauti na uwezo wa miundombinu ya skuli ziliopo.


Vile vile alisema Wizara inakabiliwa na deni la shilingi Bilioni 1.65 linalotokana na ada na posho la wanafunzi wanaosoma elimu ya juu kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu, ambalo linapswa kulipwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2020/2021.


Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alikutana na Uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji ameipongeza Wizara hiyo kwa juhudi kubw aza kuleta maendeleo.


Nae, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Sira Ubwa Mamboya alisema katika kipindi hicho Wizara hiyo kupitia Programu ya Miundombinu na Huduma za Usafirishaji imepata mafanikio makubwa ikiwemo kukamilisha ujenzi w abarabara mbali mbali Unguja na Pemba kwa kiwango cha Lami kwa urefu w akilomita 63.6.


Alizitaja barabara hizo kuwa ni pamoja na Bububu-Mahonda – Mkokotoni kilomita 31, Pale – Kiongele km (4.6), Matemwe – Muyuni (km 7.6), Koani – Jumbi (km 3.2), Ole – Kengeja (km 13) pamoja na barabara ya Donge – Muwanda kilomita 4.2.

Aidha, alisema kupitia Programu ya TEHAMA Wizara imefanikiwa kuimarisha miundombinu katika sekta ya Afya kwa kuzinganisha na Mkonga wa Mawasiliano na masine za X-Ray ziliopo Kivunge na Makunduchi.


No comments:

Post a Comment