WAZIRI KAIRUKI AHAMASISHA KILIMO CHA PAMOJA SAME - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 9 July 2020

WAZIRI KAIRUKI AHAMASISHA KILIMO CHA PAMOJA SAME

Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekzaji Angela Kairuki akizungumza na Mkuu wa wilaya ya Same Rosemery Senyamule alipowasili ofisini hapo wakati akiwa katika ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya uwekezaji katika wilaya hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Same Rosemery Senyamule akimueleza jambo Waziri Kairuki alipofika katika ofisi ya mkuu wa wilaya ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika wilaya ya Same kutemebelea maeneo ya uwekezaji.

Na Dixon Busagaga, Same

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Angela Kairuki, ameutaka uongozi  wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, kuhamasisha wananchi kulima kilimo cha pamoja, hususani yale mazao yenye uhitaji mkubwa katika viwanda, ili kuwezesha kilimo chenye tija na upatikanaji wa masoko ya uhakika.

Kairuki ametoa Rai hiyo jana, wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani humo, ambapo alisema kilimo cha pamoja kina manufaa makubwa kwa wakulima kwa kuwa wawekezaji wataweza kukununua mazao mengi kwa pamoja, na hivyo kuinua uchumi.

Kairuki alisema, yapo mazao yenye uhitaji mkubwa katika viwanda mbalimbali nchini, akitolea mfano wa  zao la Mtama, ambapo alisema kampuni ya Kilimanjaro Biochem (KBL) iliyopo wilayani Mwanga, ina mahitaji ya zaidi ya Tani 6,000 hivyo ni dhahiri, kuwa soko la uhakika litapatikana, endapo wakulima watalima kilimo cha pamoja na kuzalisha zao hilo kwa wingi.

"Wilaya ya Same ina fursa nyingi za Kilimo, kutokana na ardhi yake kuweza kustawisha mazao ya aina nyingi tofauti na maeneo mengine, kwani yapo maeneo ya umwagiliaji ambapo wanaweza kulima kilimo cha umwagiliaji na maeneo mengine makubwa ya kilimo kingine, hivyo hamasisheni kilimo cha pamoja chenye tija," alisema Kairuki.

Mbali na hilo,  Kairuki  alitaka pia Wilaya hiyo,  kujenga makumbusho ya Madini, ambayo watalii pamoja na wananchi watatembelea na kujionea madini mbalimbali ambayo yanapatikana wilayani humo.

"Fursa ya madini ni kubwa katika Wilaya hii, sasa wekeni mkazo kwenye utafiti ikiwezekana iwe kijiji kwa kijiji na kuwepo na maduka ya kuuzia vifaa vya uchimbaji ikiwemo baruti"

Aidha katika kupanua wigo wa uwekezaji, Katika wilaya hiyo,Kairuki alisema ipo haja ya kuangaliwa uwezekano wa kuanzishwa kwa machinjio ya kisasa, katika Wilaya hiyo,akieleza kuwa ipo mifugo mingi na endapo itaanzishwa machinjio, itakuwa fursa nzuri ya uwekezaji katika Halmashauri hiyo.

"Suala la kuanzisha machinjio, liende sambamba na upatikanaji wa mbegu bora za mifugo, pamoja na kutoa elimu kwa wafugaji juu ya umuhimu wa machinjio ili kuwawezesha kuitumia na kuleta tija kwa Wilaya"alisema Kairuki.

Katika hatua nyingine,Kairuki aliutaka pia uongizi wa Wilaya hiyo, kushughulikia migogoro ya Ardhi hususani ile inayohusu wananchi na wawekezaji kwa haraka, ili kuweza kutoa muafaka na kuwezesha uwekezaji kuendelea kwa tija.

"Mwekezaji anapofika mahali akakutana na migogoro, inamchelewesha kuanza kazi zake, lakini pia inakwamisha kasi ya uwekezaji, hivyo hakikisheni mnashughulikia migogoro kwa haraka iwezekanavyo, ili kupanua wigo wa uwekezaji"

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule,alisema wakulima kulima zao moja katika eneo moja, itawarahisishia wanunuzi kupata mazao wanayohitaji kwa wingi, na hivyo kuwa na masoko ya uhakika.

"Wakulima wanapolima mmojamoja  au mazao ya aina tofauti katika eneo moja,hayana tija kwao wenyewe na pia kwa serikali, pindi inapotarajia kuuza zao moja kwa Wingi kwa wakati mmoja, lakini inapotokea tukasema kata fulani ni ya zao fulani, wanaweza kukusanya mazao yakauzwa kwa pamoja na kuleta Tija," alisema Senyamule.

No comments:

Post a Comment