Mwenyekiti wa Bodi ya Mkonge Bi Mariamu Mkumbi wakati akihutubia wadau wa Tasnia ya mkonge katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Royal Village Jijini Dodoma. |
Wakuu wa Mikoa mbalimbali wakisikiliza mawasilisho mbalimbali katika mkutano wa wadau wa tasnia ya mkonge uliofanyika leo Jijini Dodoma. |
SERIKALI imesema kuwa uzalishaji wa zao la mkonge umeongezeka kutokana na jitihada za serikali na wadau mbalimbali na uwepo wa sera wezeshi katika kipindi cha serikali ya Awamu ya tano.
Kauli hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba aliyemwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye ufunguzi wa mkutano wa wadau wa zao la mkonge
Mgumba amesema uzalishaji wa zao la mkonge umeongezeka toka tani 19,700 mwaka 1970 hadi tani 36,000 ilipofika mwezi Desemba 2019 na kufanya Tanzania kuwa mzalishaji Mkubwa wa pili duniani baada ya Brazil.
"Takwimu hizi zinajumuisha mkonge unaozalishwa na wakulima wakubwa (Estates) ambao huzalisha takriban Tani 28,000 na wakulima wadogo ambao huzalisha takriban Tani 8,600 " alisema Naibu Waziri Mgumba.
Hata hivyo, alisema uzalishaji huu hauridhishi ikilinganishwa na fursa zilizopo kwenye Tasnia ya Mkonge kutaka wadau wajikite kuweka mikakati mizuri ili wakulima wengi zaidi wahamasishwe kulima mkonge.
Mgumba alisema pamoja na changamoto zilizopo serikali imejipanga kushughulikia mambo yafuatayo ili zao hili uzalishaji wake iongezeke.
Kwanza kuongeza tija na uzalishaji kwa kuanzisha vitalu vya mbegu ya mkonge katika Halmashauri zote amabako zao la mkonge linastawi.
Aidha, kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI Mlingano uzalishaji wa mbegu bora umeanza ili ziweze kuzalishwa kwa wingi.
Pili kufanya uhakiki wa mashamba ya Mkonge yaliyobinafsishwa ili yaweze kuzalisha mkonge kama ilivyokubaliwa kwenye mikataba;na tatu kutoa elimu kwa maafisa ugani katika vijiji na kata kwenye maeeo yanayolima mkonge.
Naibu Waziri Mgumba aliongeza kusema serikali itaongeza bajeti ya Kituo cha Utafiti TARI Mlingano ili kiweze kuzalisha mbegu bora za Mkonge na kuzisambaza kwa wakulima nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Mkonge Tanzania Mariam Nkumbi alisema Bodi umelenga kuongeza uzalishaji wa mkonge kufikia tani 120,000 ifikiapo mwaka 2025 kwa kufanya uhamasishaji katika wilaya 41 ndani ya mikoa 16 nchini.
" Tumelenga kuzalisha tani 60,257 ifikiapo mwaka 2025 ambapo kunahitajika wakulima wadogo 60,000 tu kutoka wilaya 41 zilizopo kwenye mikoa 16 endapo kila mkulima atalima ekari 2.5 za mkonge" alisema Mwenyekiti huyo wa Bodi ya mkonge
Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa mikoa 16 inayolima mkonge nchini Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa Tanzania Bara Mhandisi Evarist Ndikilo alisema wapo tayari kutoa uzoefu wao wa kusimamia Kilimo ili wakulima wengi wadogo wahamasike kuanzisha mashamba ya mkonge.
" Maelekezo ya serikali kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ni kuwa zao hili la mkonge lilimwe na wakulima wadogo wengi zaidi hivyo tupo tayari kutekeleza agizo hilo " alisisitiza Ndikilo.
Aliongeza kusema wakuu wa Mikoa wanaiomba Wizara ya Kilimo kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Wakuu wa mikoa wakati wa kikao cha wataalam wa mkonge hivi karibuni.
Naye Naibu Waziri Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashata Nditiye aliwahakikishia wadau wa mkonge kuwa serikali itahakikisha mazao yote yanayotokana na mkonge yanasafirishwa salama yakiwa ardhini,majini na angani kwa kuweka mazingira na miundombinu bora.
Lengo la Mkutano huu ni kujadili na kuzipatia majawabu changamoto zinazoikabili Tasnia ya Mkonge nchini ili kuongeza tija katika uzalishaji, ajira na kukuza sekta ya viwanda, pato la mkulima.
Mkutano huo wa wadau umeshirikisha Wakuu wa Mikoa 16,Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi ,wakulima,Wazalishaji bidhaa za Mkonge,taasisi za fedha na Wizara za kisekta chini ya uratibu wa Wizara ya Kilimo.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi Saad Kambona amewahakikishia wadau kuwa maelekezo ya serikali ya Awamu ya Tano kufufua zao la mkonge yanatekelezwa kwa vitendo ili kufika tani 120,000 ifikiapo mwaka 2025.
No comments:
Post a Comment