Dk. Ali Mohamed Shein. |
Na Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Makamo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amesema uamuzi wa CCM kumteua Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi kuwa mgombea wa kiti cha Urais kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao, umezingatia uwezo mkubwa na uaminifu alionao mgombea huyo.
Dk. Shein amesema hayo leo katika viwanja vya Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui katika hafla ya mapokezi ya Mgombea wa Chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu ujao Dk. Ali Hussein Mwinyi, baada ya kukamilika kwa mchakato wa kumpata mgombea kupitia vikao mbali mbali. Alisema Dk. Mwinyi ni mzaliwa wa Zanzibar na mwanachama kindakindaki, akiwa kiongozi muaminifu alielitumikia taifa kwa juhudi kubwa na mwenye kutoa maamuzi kwa hekima busara.
Alisema mwanachama huyo ni mtaratibu na ana mahusiano mema na watu, akibainisha chama hicho kutokuwa na mashaka yoyote na uwezo na uadilifu wake. Alisema kutokana mwenendo bora wa kiongozi huyo, CCM ina hakika kuwa atayalinda, kudumisha na kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa CCM iko tayari kuingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu, akibainisha kuwa na matarajio makubwa ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo.
“Serikali iko makini kwa uchaguzi, fedha kwa ajili ya uchaguzi huo zipo”, alisema.
Naye, mgombea wa kiti cha Urais kupitia chama hicho, Dk. Hussein Ali Mwinyi alisema azma ya kugombea wadhifa huo ni kuwatumikia Wazanzibar pamoja na Watanzania wote kwa uwezo wake wote, akibainisha dhamira ya kuwaletea maendeleo na ustawi katika maisha yao.
Alisema miongoni mwa vipaumbele vyake ni pamoja na kuendeleza amani iliopo ili Zanzibar iweze kupiga hatua zaidi za maendeleo, huku akiahidi kazi hiyo kufanyika kwa ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama.
Alisema analenga kuimarisha umoja na mshikamano wa Kitaifa miongoni mwa Wazanzibari wote ili kuondokana na hatari ya kuibuka kwa ubaguzi wa kimajimbo. Alieleza kuwa ataendeleza kasi ya maendeleo iliyoanzishwa na mtangulizi wake na kukamilisha miradi yote ya maendeleo kwa maslahi ya Wazanzibari.
Katika utekelezaji wa majukumu yake, Dk. Mwinyi alisema hatakuwa na muhali, huruma wala na atasimamia vita dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma, uzembe pamoja na watendaji wote wasiowajibika ipasavyo.
Aliwataka viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa kujiweka tayari kwa kazi ili kuweza kukipatia ushindi chama hicho, kupitia kampeni zitakazoendeshwa kisayansi ili hatimae kushika Dola.
Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi aliahidi kutetea maslahi ya Zanzibar kupitia Jumuiya zote za Kikanda na zile za kimataifa. Mapema, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Juma Abdalla Sadalla alisema hatua ya kwanza ya uteuzi wa mgombea wa chama hicho imekamilika, kupitia vikao halali vilivyoendeshwa kwa uwazi na bila makundi.
Alimsifia mgombea huyo kuwa ni mwanachama mchapakazi, mweledi, mwenye uelewa wa mambo na uwezo mkubwa katika kutoa maamuzi kwa hekima na busara. Mapema kiongozi huyo alipata mapokezi makubw akutoka kw awnanachi na wanachama wa CCM, waliojikusanya kutoka uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume hadi Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui, akiwemo msanii maarufu wa kizazi kipya kutoka Tanznaia Bara Ali Kiba.
No comments:
Post a Comment