MBUNGE UMMY ALIVYOPAMBANA 'KUZIREJESHA' COASTAL UNION NA AFRICAN SPORTS - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 1 July 2020

MBUNGE UMMY ALIVYOPAMBANA 'KUZIREJESHA' COASTAL UNION NA AFRICAN SPORTS

 Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu  na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga (CCM) kushoto akipokea tuzo ya heshima kutoka kwenye Mwenyekiti wa Baraza la wazee la Klabu ya Coastal Union ikiwa ni kutambua mchango wake kuisaidia timu hiyo wakati ilipopanda daraja na kurudi Ligi kuu.


 Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu  na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga (CCM)kulia akigawa vifaa vya michezo kwa timu za soka mkoani Tanga zilizokuwa zikishirika Ligi ya Banda Cup msimu uliopita ambapo vifaa hivyo alivitoa yeye.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga katika akiwa na baadhi ya viongozi wa timu ya Coastal Union wakati akipokwenda kuwakabidhi kiwanja eneo la Maweni Jijini Tanga kushoto ni Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daudi Mayeji kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya City Plan Consultants (T) Limited Dkt Juma Mohamed.


 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Ummy Mwalimu katikati akiwa na viongozi wengine pamoja na timu ambazo alizikabidhi vifaa vya michezo jezi kwa ajili ya kushiriki Mashindano ya Banda Cup msimu uliopita.

NA MWANDISHI WETU, TANGA


UNAPOZUNGUMZIA mafanikio ya soka kwa Mkoa wa Tanga huwezi kuacha kulitaja jina la Ummy Mwalimu ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa huo (CCM) na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto ambaye amefanya kazi kubwa kurudisha heshima ya michezo.

Sie sote ni mashahidi kwamba bila juhudi kubwa ambazo alizifanya kwa kushirikiana na viongozi wengine wa mkoa huo mkoani Morogoro wakati timu ya Coastal Union ikitafuta tiketi ya kureja Ligi kuu ingekuwa ni ndoto wana Tanga kushuhudia michuano hiyo mikubwa hapa nchini ikichezwa mkoani hapa.

Bila kujali jambo lolote licha ya kuwa na shughuli za kitaifa alilazimika kuungana na wana michezo mkoani Tanga kupiga kambi mkoani Morogoro ili kuhakikisha anatimiza ndoto zake za kuhakikisha anaandika historia ya kuirudisha Ligi kuu timu hiyo Kongwe hapa nchini ambayo ilishuka daraja kabla ya kurejea tena.

Licha ya kuipandisha timu hiyo ikiwa mkoani Morogoro lakini alilazimika kuisindikisha hadi mkoani Tanga akiwa na msafara mkubwa wa magari huku akilakiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella eneo la Pongwe huku akiendelea kuisapoti timu hiyo katika Nyanja mbalimbali.

Hakuna asiyejua juhudi kubwa ambazo amezifanywa kuhakikisha anapambana kwa hali na mali ili timu hiyo inarudi Ligi kuu baada ya kushuka daraja mara kadhaa na kupoteza mwelekeo ambapo aliamua kulivalia njuga suala hilo na kusimama kidete na kufanikisha ndoto yake.

Katika makala hii leo Nataka japo nikueleza jambo utambua kwamba unapomzungumzia Mbunge Ummy Mwalimu amefanya nini kwenye kulipata mafanikio soka la Mkoa wa Tanga mpaka limefikia hapo lilipo lakini pia ameendelea kuwa bega kwa bega na timu kongwe za mkoa huo ambazo zilikuwa na historia ya soka.

Tukianzia kwa Klabu ya Coastal Union “Wagosi wa Kaya” ambao mwaka 1988 waliandika historia mkoani Tanga kwa kuchukua Ubingwa wa soka nchini ambao mpaka sasa imekuwa ni klabu ambayo ikiingia katika kumbukumbu za mabingwa wa nchi hii huwezi kuacha kuizungumzia.

Salimu Bawaziri ni Mjumbe wa Kamati ya Mipango na Fedha katika timu ya Coastal Union anaeleza kwamba mchango wa Mbunge Ummy ndani ya timu hiyo ni mkubwa na hauwezi kusaulika kwani amekuwa mstari wa mbele kuwasaidia tokea wakiwa Ligi daraja la kwanza mpaka akahakikisha timu inapanda daraja kwa kushirikiana na viongozi.

“Nakumbuka wakati tukiwa kule mkoani Morogoro tunapotafuta tiketi ya kupanda daraja mara kwa mara alikuwa anakuja kukutana na wachezaji na viongozi kwa kutoa motisha na hamasa kwa wachezaji kwa lengo la kuhakikisha tunapambana na kurejea Ligi kuu hivyo mchango wake ni mkubwa sana mpaka tulipo sasa na bado amekuwa akitusaidia”Anasema Bawaziri.

Anasema licha ya viongozi wengi kusaidia lakini Mbunge Ummy aliweza kuibeba timu hiyo tokea kipindi timu hiyo inashiriki Ligi daraja la kwanza hapa nchini na hakuweza kuiacha pekee bali alikuwa akifika kambini kwa kuzungumza na wachezaji kuwapa motisha jambo ambalo limechangia kwa asilimia kubwa kuweza kurudi ligi kuu.

“Kwa kweli msaada ambao ametusaidia ni mkubwa na hatuwezi kuusahau kufanya jitihada kubwa kwetu lakini pia kuweza kutusaidia kuweza kupata uwanja eneo la Maweni lenye ukubwa wa mita 7632 mkubwa ambao tutaanza kuufanyia kazi ambao huu utakuwa ni chachu kubwa kwa maendeleo ya timu yetu”Anasema

Hata hivyo anasema kuwa watahakikisha wanakuwa bega kwa bega naye kila wakati kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya timu hiyo na historia ambayo ameiweka itakayodumu kwa vizazi na vizazi kwani kila watakapotumia eneo hilo lazima watakumbuka jambo hili kubwa lilifanywa na mbunge Ummy.

Hata hivyo Mbunge Ummy anaeleza dhamira yake ya kusaka eneo hilo ambapo anasema kubwa zaidi ni kuisaidia timu hiyo katika mipango iliyokuwa nayo kuanza kwenda vema huku wakijipanga kwa hatua nyengine lakini kubwa kwa kuwa na eneo lake ambalo watalitumia katika matumizi mbalimbali ikiwemo uwanja wa kuchezea.

““Nataka niwaambie Coastal Union tutaendelea kuwa pamoja katika harakati zetu za kuwania Ubingwa wa Ligi kuu labda niwahaidi kuwatafutia wadau pia niwaambie bado tunaendelea kutafuta wadau na nihaidi hata ile block yenye square mita 9600 yenye thamani milioni 48 nitafue wadau ili waweze kupata eneo hilo”Anasema

Anasema atasaidia kutafuta wadau ili kupata eneo hilo ambalo litakuwa kwa ajili ya matumizi ya ujenzi wa Hosteli,Gym ya Mazoezi na Ukumbi wa sherehe wa Coastal Union kwa sababu watu wa Tanga wana fanya sherehe na kitchen party kila siku

“Labda ndugu zangu wapenzi wa soka na wana michezo wenzangu jambo hilo limewezekana kutokana na mshikamano uliopo baina ya viongozi na wanachama huku wakiwataka kuuendeleza ili kuweza kupata mafanikio makubwa siku zijazo kwenye michuano ya ligi kuu”

Mbunge Ummy hakuishia hapo lakini pia anasisitizia timu hiyo kufanya vizuri kwa timu hiyo ndio imekuwa sababu ya kuwavuta wadau ambao wameweza kuwasaidia katika masuala mbalimbali hivyo wachezaji na walimu wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanajipanga vema kwa ajili ya kufanya vizuri.

“Lakini pia eneo hilo la kiwanja ambacho tuliwakabidhiwa timu hiyo nitagharamia gharama za hati ya usajili mpaka kupata hati yenye jina la klabu ya Coastal Union na hivi karibuni nitakwenda kuwakabidhi rasmi kwa lengo la kuanza kuendelea na mipango yao “Anasema

Hata hivyo Mbunge huyo anatoa wito kwa wakazi wa Jiji la Tanga wanaotaka kuwekeza waende eneo la Pongwe ambalo lina viwanja 937 hivyo watumie nafasi hiyo kwa sababu timu ya Coastal Union wakiwa hapo itavutia lakini pia kuwepo kwa eneo kwa ajili ya zahanati kama walivyofanya kutoa kwa shule ya Msingi.

Hatua ya Mbunge Ummy kuikabidhi eneo timu hiyo kulipelekea Mwenyekiti wa Coastal Union Steven Mnguto kuishiwa na maneno ya kuzungumza huku akionyesha furaha yake isiyokuwa ya kifani kwake kwa kuisaidia timu hiyo lakini pia kuweza kurudisha heshima ya soka kwa mkoa huo.

“Mh Mbunge hapa nilipo nimeishiwa maneno ila nisema mama Ummy umetusaidia sana ulikuwa wapi siku zote kauli ya Mungu anasema nitakuwa muda na saa usizotarajia kila tunapofanyaa tukio kubwaa tunaona nyota inatuandama tulipata basi wakati tunapanda daraja kipindi kile safari hii tumepanda nyota nyengine imekuja kiwanja tuendelee kuomba na kushikamana”Anasema.

Hata hivyo naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Tanga (TRFA) Saidi Soud anasema wao kama wasimamizi wa soka la mkoa wa Tanga wamehemewa na furaha kwa jambo hilo ambalo ni la kihistoria kutokana namna Waziri huyo alivyowashika mkono.

“Labda nisema Waziri Ummy ni mama wa kweli nakumbuka wakati unasema utatushika mkono huko mbele tulikuwa tunasuasua lakini ujio wako umesaidia kuvunja hata makundi yaliyokuwa yakirudisha nyuma maendeleo “Anasema.

Akizungumza katika Halfa hiyo, Mkurugenzi wa Kampuni ya City Plan Consultants (T) Limited Dkt Juma Mohamed anaeleza namna Mbunge Ummy alivyofanikisha upatikanaji wa eneo hilo ambapo anaeleza kwamba walipata ombi kutoka kwake na kuona namna ya kupata eneo la Michezo kwa timu ya Coastal Union.

Anasema baade waliweza kulijadili na kuliwasilisha kwa wadau ambao ni wananchi wa eneo la hapa na kuweza kupatikana kwa eneo hilo ambapo pia unaweza kutoa viwanja cha mpira hamsini kwa mia moja lakini panazaidi ya eneo la pitch ya mpira.

“Tulikubaliana kuhifadhi viwanja 16 upande block za chini kwani kuna masuala wanaendelea na majadiliano vitalipiwa kwa ajili ya kuweka maeneo mbalimbali ya michezo nah ii itafungua ukurasa mpya wa soka kwa mkoa “Anasema Dkt Juma.

Licha ya hivyo Mbunge Ummy aliweza kufanya ziara ya mara kwa mara kutetembelea kambi ya timu ya Coastal Union iliyokuwepo eneo la Saruji Jijini Tanga wakati timu hiyo ikishiriki daraja la kwanza na nikiwa kwenye nafasi ya tatu kwenye kundi B.

Baada ya kutembelea kambi hiyo aliwasisitizia wachezaji kuongeza jitihada na kujituma ili kushinda mechi nne zilizobakia kwa lengo la kujihakikishia nafasi ya kucheza ligi kuu ya Tanzania bara msimu wa mwaka 2018/2019 jambo ambalo lilifanikiwa na kuiwezesha timu kurudi ligi za juu.

“Katika nukuu ya maneno yake wakati huo ndugu zangu “Coastal Union ikipanda daraja na kucheza Premier League sio tu itawezesha vijana kupata kipato bali pia itachochea uchumi na maendeleo ya Jiji la Tanga mwisho wa kunukuu“

Katika kuhamasisha huko Mbunge Ummy aliwakabidhi shilingi milioni 3 na nusu kwa ajili ya mishahara ya wachezaji ya mwezi Desemba na gharama za chakula huku akihaidi kutoa zawadi y ash.milioni 2 kwa kila mechi watakayoshinda kati ya mechi nne zilizobaki.

Baada ya hatua hiyo Kocha Mkuu wa timu ya Coastal Union Juma Mgunda amemuhakikishia Mbunge Ummy kuwa vijana wapo tayari kufanya vizuri kwenye Ligi na hivyo hatutakuangusha katika michezo yao hiyo iliyosalia katika michuano ya Ligi Daraja la kwanza jambo ambalo walilfanikisha kwa asilimia kubwa na kurejea ligi kuu.

Pia walimshukuru Mbunge Ummy kwa kujitoa kwake ili kuhakikisha timu hiyo inapanda daraja ambapo tukio hilo la makabidhiano limehudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Tanga (TRFA) Said Soud na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Coastal Union Salim Bawaziri

“Motisha kwa wachezaji wa timu ya Coastal Union" 

Mbunge Ummy kwa kuonyesha kujali na kuwathamini wana michezo mkoani Tanga alilazimika kuwalipa wachezaji wa timu ya Coastal Union na African Sports mishahara kwa kipindi Fulani huku akihamasisha uwanjani.

Hatua hiyo inatajwa kwamba imechangia uwepo wa timu hiyo kwenye Ligi madaraja tofauti huku zikiendelea kufanya vizuri kutokana na uwepo wake ambao umekuwa na mchango mkubwa kwenye soka.

Wakati mwengine wana Tanga ambao wanakuwa wakijitokeza kwenye viwanja vya Mkwakwani wametakuwa ni mashahidi tosha Mbunge Ummy amekuwa akihudhuria mechi za timu hiyo licha ya kuwa nje ya mkoa huo kwa wakati huo lakini hulazimika kufika hata kipindi cha pili uwanjani ikiwa ni kuwahamasisha wanamichezo.

Kutembelea kambi ya wachezaji.
Ummy ni miongoni mwa viongozi wachache ambao kila wakati timu ya Coastal Union inapojiandaa kwa ajili ya kucheza na timu kubwa nchini ikiwemo Simba, Yanga na hata nyengine amekuwa akitinga kambini kuzungumza na wachezaji ikiwezekana kula nao chakula cha mchana huku akiwahamasisha suala la ushindi ni lazima.

Hatua hiyo imetajwa kwamba imechangia kwa asilimia kubwa wachezaji wa timu hiyo kupata hari kubwa ya kuweza kufanya vizuri katika michuano ya Ligi Daraja la kwanza na hatimaye kurudi Ligi kuu na kudumu mpaka wakati huo.

Uhamasishaji.
Mbunge Ummy ambaye siku zote nimeshindwa nimfananishe na kiongozi gani hapa nchini amekuwa na desturi ya kila mechi zinapokuwa zikicheza timu kongwe za mkoa wa Tanga amekuwa akishirikiana na mashabiki na wapezi majukwaani kuhamaisha ushindi kwa staili ya kushangilia.

Staili hiyo ya ushangiliaji ilipelekea kuchangia kuwaibua mashabiki wengi wapya ndani ya timu hiyo ambao kila timu hiyo inapokuwa ikicheza mechi zake za nyumbani wanalazimika kufika uwanjani na kuujaza uwanja hali ambayo ilichangia kwa asilimia kubwa kwenye michezo ya nyumbani timu kufanya vizuri kutokana na hamasa.

Hata hivyo Mbunge Ummy hakuiacha nyuma Klabu ya African Sports ambao waliwahi kuwa mabingwa wa kombe la Muungano mwaka 1988 ambapo wakati huo taji hilo ndio lilikuwa kubwa zaidi nchini,michuano hiyo iliyoshirikisha timu za Bara na Visiwani na kumpata bingwa wa jumla wa nchi na pia wawakilishi wa michuano ya Afrika.

Bingwa wa Bara alikuwa anakwenda kucheza Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati pekee,lakini bingwa wa Muungano wakati huo alikuwa anacheza Klabu Bingwa Afrika na mshindi wa pili wa Ligi ya Muungano, alikuwa anacheza iliyokuwa michuano ya Kombe la Washindi Afrika, baadaye ikaongezeka na mshindi wa tatu akawa anacheza Kombe la CAF.

Pamoja na kushiriki michuano hiyo lakini miaka ya nyuma timu hiyo iliyumba na kushuka daraja kwa nyakati tofauti licha ya kurejea Ligi kuu lakini ilishindwa kuhimili mikimikii ya ligi hiyo na kujikuta wakishuka daraja wao na mahasimu wao Coastal Union na Mgambo Shooting kwa wakati mmoja.

Baada ya kushuka daraja wakajikuta wakishindwa kuhimili vishindo vya daraja la kwanza na kujikuta wakirudi kucheza Ligi daraja la pili walilopo mpaka wakati huu huku wakipambana kuhakikisha wanarejea walipotoka kwa kuweka mipango imara ambayo itawafikisha huko.

Kwa kuona hali ya timu hiyo Mbunge Ummy aliamua kujitosa na kuanza kuisaidia katika masuala mbalimbali ikiwemo vifaa vya vyenye thamani ya zaidi ya milioni 1.5 ikiwemo vyakula wakati wa kamb na motisha ikiwa ni mkakati kabambe wa kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri kwenye mashindano wanayoshiriki na hatimaye kucheza ligi daraja la kwanza msimu ujao.

Mbunge Ummy anasema vifaa hivyo vitakuwa ni chachu ya timu hiyo kuweza kufikia malengo yao huku akieleza dhamira yake kubwa ni kuhakikisha timu hiyo inarejea ligi daraja la kwanza na ile ya Coastal Union ihakikisha msimu ujao inarudi Ligi kuu.

“Niseme tu sisi tumejipanga kuhakikisha tunazirejesha timu hizi kwenye michuano ya Ligi kuu soka Tanzania bara tukianzia na timu ya Coastal Union lakini ndugu zangu African Sports mhakikishe mnarudi ligi daraja la kqwanza na baadae ligi kuu “Anasema

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Mwenyekiti wa Klabu ya African Sports, Awadhi Salehe Pamba anamshukuru Waziri Ummy kwa kuwasaidia msaada huo ambao utakuwa ni chachu kwao kuweza kufikia malengo yao kutokana na changamoto hiyo kwisha.

Alisema msaada uliotolewa na Mbunge Ummy utakuwa chachu kubwa kwao kuweza kufikia malengo yao waliojiwekea ya kuhakikisha wanarudi ligi kuu kwani ndio ndoto yao kubwa ambayo wamekuwa wakiiwaza kila wakati.

“Mbunge Ummy tukushukuru sana katika hili umetupa nguvu ya kuweza kupambana na tuna kuhaidia kuhakikisha tunairudisha timu Ligi daraja la kwanza na hatimaye ligi kuu.

No comments:

Post a Comment