DK. MWAKYEMBE, MAKONDA WAANGUKA VIBAYA KURA ZA MAONI...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 21 July 2020

DK. MWAKYEMBE, MAKONDA WAANGUKA VIBAYA KURA ZA MAONI...!

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe (wa nne kulia) akifuatilia kwa makini zoezi la kuhakiki kura za maoni.

Dk. Tulia Ackson (aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge) akiwa amebeba mzigo wa kura zake za maoni. Dk. Tulia ameshinda kwa kishindo kwa idadi ya kura 843, huku akifuatiwa na Bw. Mahenge Mabula aliyepata kura 16 (mshindi wa pili) na mshindi wa tatu akiwa ni Charles Mwakipesile aliyepata kura 11.

Dk. Tulia Ackson akitafakari kwa furaha baada ya ushindi.

Bw. Ally Mlagila 'Kinanasi' aliyemshinda alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe.

Prof Joyce Ndalichako (kura 405) akipongezwa na mshindani wake (kulia) mara baada ya kuibuka mshindi kura za maoni Jimbo la Kasulu Mjini, mkoani Kigoma. Mshindani wake, Daniel Nsanzugwanko kaambulia kura 80.

*DK TULIA KIDEDEA MBEYA MJINI...!

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe ameshindwa kutetea kiti chake katika kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujikuta akishindwa vibaya na mshindani wake mkuu katika kura hizo, Ally Mlagila 'Kinanasi'.

Hadi mwandishi wa habari hizi akiondoka ukumbini ulipofanyika uchaguzi huo, Bw. Ally Mlagila 'Kinanasi' alikuwa ameshinda kwa kura 493, huku akifuatiwa na Bw. Hunter Mwakifuna akipata kura 288 na Dk. Mwakyembe akiambulia kura 252 na kushika nafasi ya tatu katika mchuano huo.

Kwa matokeo haya ya awali ya kura za maoni ndani ya CCM, Dk. Mwakyembe anakuwa ameshindwa kutetea nafasi yake ya kuwawakilisha wana-Kyela kupitia Chama Cha Mapinduzi.
Kigogo mwingine maarufu aliyeanguka ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Makonda aliyeachia nafasi ya ukuu wa mkoa na kwenda kujaribu kugombea ubunge Jimbo la Kigamboni.

Katika matokeo ya awali Bw. Makonda amejikuta akishindwa vikali na mpinzani wake, Bw. Faustine Ndugulile aliyejizolea kura 190 sawa na asilimia 45, huku Makonda akiambulia kura 122 sawa na asilimia 30. Wengine waliofuatia katika kinyang'anyiri hicho ni Bw. Abubakari Kachwamba aliyepata kura 39 sawa na asilimia 9.8 na Bw. Allan Sanga aliyeambulia kura 15, ikiwa ni asilimia    3.7. ya kura zote zilizopigwa yaani kura 398.

Kigogo mwingine aliyeangukia 'pua' ni David Kafulila aliyeachia ngazi serikalini ya Ukatibu Tawala Mkoa wa Songwe na kwenda kugombea Jimbo la Kigoma Kusini. Aliyeshinda katika kura za maoni ni Bi. Hasna Mwilima aliyejinyakulia kura 272, huku Kafulila akiambulia nafasi ya nne kwa kupata kura 64. Mshindi wa pili katika mchuano huo ni Bw. Nashoni aliyejipatia kura 141, huku mshindi wa tatu akiibuka Bw. Kizito kwa kura 117. Kwa matokeo hayo Kafulila ameshika nafasi ya nne na kuangushwa na wapiga kura.

Wengine ni Eng Sasilo kura 01, Bwire kura 02, Rugema kura 07, mzee Mtura kura 11, Hacharika kura 10 na Aminiel kura 29.

Jimbo la Mbeya Mjini, Dk. Tulia Ackson (aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge) ameongoza katika kura za maoni kwa tiketi ya CCM kwa kushinda kwa kishindo idadi ya kura 843, huku akifuatiwa na Bw. Mahenge Mabula aliyepata kura 16 (mshindi wa pili) na mshindi wa tatu akiwa ni Charles Mwakipesile aliyepata kura 11.

Mchuano mkali na wa kuvutia ni wa Jimbo la Buchosa ambapo watiania Dk. Charles Tizeba wamefungana na mwenzie Bw. Erick Shigongo ambapo wote wamepata kura 354.

Jimbo la Siha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Agrey Mwandry ameshindwa vibaya katika kura za maoni na Eng.Betson Maimu. Katika mchuano huo uliokuwa na wagombea watano, Maimu ameibuka mshindi wa kwanza kwa kura 231, akifuatiwa na Bw. Mwandry aliyepata kura 151.

Katika mchuano huo; wagombea wengine walikuwa ni Dk. Godwin Mollel alieambulia kura 58, Justine Kweka kura 85, Lameck Munuo kura 91. Katika Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nasari ameshindwa kulitetea Jimbo hilo aliloliongoza akiwa Chadema kabla ya kuhamia CCM. Matokeo ya kura za maoni ndani ya CCM katika jimbo hilo yanaonesha; Bw. John D ameshinda kwa kura 536, akifuatiwa na Bw. Dan Pallangyo aliyepata kura 63, Bw. Mbise kura 41 na Nasari kuambulia kura 23.

No comments:

Post a Comment