KIWANDA CHA KUCHENJUA, KUTAKASA MADINI CHAANZA KAZI, DODOMA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 8 June 2020

KIWANDA CHA KUCHENJUA, KUTAKASA MADINI CHAANZA KAZI, DODOMA

 Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Eyes of Africa Ltd (EOA) Ferenc Molnar akionesha moja ya mtambo mkubwa na wakisasa wa kutakasa madini wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) walipotembelea kiwanda hicho jijini hapa mwishoni mwa wiki.

 Mtendaji Mwendeshaji wa kiwanda hicho, Prince Mugisha akionesha moja ya jarida (Catalogue) ya huduma zinazotolewa na EOA.

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Eyes of Africa Ltd (EOA), Ferenc Molnar akisisitiza jambo kwa wanahabari. Kulia kwake ni baadhi ya mitambo ya kusafisha dhahabu.

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Eyes of Africa Ltd (EOA), Ferenc Molnar akiwa na watendaji wengine ndani ya kiwanda hicho.

 Ferenc Molnar akionesha jinsi moja ya teknolojia ya mtambo huo wa wa kisasa ulivyoweka jina (Lebel) ya moja ya taasisi kwenye dhahabu.

 Madumu ya kuhifadhia madawa yakiwa kwenye chumba maalumu kiwandani hapo.

Mtendaji Mwendeshaji wa Kiwanda cha EOA,  Prince Mugisha akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari.

Taswira ya kiwanda hicho.


Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Dodoma


HATIMAYE Kiwanda cha kwanza kikubwa chenye uwezo wa kutakasa dhahabu na madini mengine kwa ubora wa mahitaji ya soko la kimataifa sasa kimeanza rasmi uzalishaji nchini.

Kiwanda hicho kinachojulikana kama Eyes of Africa Ltd ( EOA) kimeanza uzalishaji wake kwa uwezo wa kutakasa dhahabu na madini mengine kwa kati ya kilo 30 hadi 50 kwa siku, huku shabaha iliyopo ni kufikia kilo 1000 ifikapo 2021.

Waziri wa Madini Doto Biteko, mnamo Agosti 20 mwaka jana wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho alisisitiza mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wake kitatoa fursa kwa Wafanyabiashara nchini kusafisha dhahabu zao, lakini kitawezesha Taifa kuwa na akiba ya madini yenye ubora wa viwango vya kimataifa kufikia asilimia 99.99 kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) 

Aidha, Januari mwaka jana, Rais John Magufuli aliagiza BoT kuwa na akiba ya dhahabu na kuhimiza haja ya Serikali kudhibiti usafirishaji wa madini kutoka hapa nchini. Ambapo Tanzania ni nchi ya 4 kwa kuzalisha dhahabu ikitanguliwa na Afrika Kusini, Ghana na Mali.

Biteko alisema mara baada ya kukamilika kwa kiwanda hicho BoT itaanza kununua dhahabu iliyotakaswa ambayo itawekwa kwenye akiba ya Taifa ya dhahabu na hatimaye kusaidia taifa kuanza kuuza dhahabu yenye ubora kiushindani kwenye soko la kimataifa.

"Hatua ya Serikali kutoa leseni ya kuanzisha viwanda vya namna hii ni takwa la kisheria kutokana na mabadiliko ya hivi karibuni ya sheria ya madini." alisema Biteko.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya kiwanda hicho, kilichopo pembezoni mwa Kiwanja cha Ndege jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa EOA, Ferenc Molnar alisema kwa sasa ujenzi umekamilika kwa asilimia 100, mitambo yote imekwishafungwa na uzalishaji umeanza.

Molnar alisema kupitia kiwanda hicho Taifa linakwenda kuongeza thamani ya dhahabu na madini yake mengine kutoka kati ya asilimia 70 na 90 iliyopo kwa sasa na kufikia kiwango cha asilimia 99.99 kinacho kubalika kwenye soko la kimataifa.

Mkurugenzi huyo mkuu mbali ya kuwakaribisha wafanyabiashara wote na taasisi nyingine zilizo kwenye mnyororo wa uzalishaji wa madini, aliweka bayana kwamba kwa sasa wapo mbioni kusaini mkataba wa utendaji wa pamoja na Shirikisho la Wachimbaji Wadogo  wa Madini (FEMATA).

" Tutaingia mkataba na FEMATA kwa sababu fedha inayotokana na mauzo ya dhahabu yao huwa moja kwa moja inarudi nchini na kunufaisha Taifa kwa ujumla...lakini wachimbaji wakubwa wanapochimba dhahabu huisafirisha nje ya nchi na huishia huko huko labda sana watalipa mrahaba pekee." alisema Molnar.

Alisema sababu nyingine ya kufanya kazi na wachimbaji wadogo ni kuwawezesha kuanza kukopesheka kwenye taasisi za fedha na zaidi kuimiliki na hatimaye kupata thamani halisi kupitia mauzo ya dhahabu iliyotakaswa.

Molnar alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi wazalishaji wakubwa wa dhahabu ambapo uzalishaji wake kwa sasa unafikia kati ya tani 4.5 hadi 5 kwa mwezi, na uzalishajj wake kwa mwaka kufikia tani 60.

" Tunapozalisha dhahabu ambayo imetakaswa tutakuwa na soko la uhakika na itakubalika kwenye vyombo vyote vya fedha...na Taifa litapata mapato stahiki. Uwepo wa kiwanda hiki utampunguzia mzalishaji gharama kubwa ya kusafiri nje ya nchi ili kupata huduma kama hii." alisema  Molnar na kuongeza;

"FEMATA na wazalishaji wengine wa madini kupitia kiwanda hiki sasa wataweza kwenda benki na kuhifadhi dhahabu, kukopesheka  na hatimaye kuruhusu iuzwe pale tu bei ya soko la dunia  itakapokuwa nzuri." 

Kwa upande wake Mtendaji Mwendeshaji wa Kiwanda cha EOA, Prince Mugisha alisema lengo la Tanzania kwa sasa ni kuhakikisha tunapata thamani halisi kulingana na madini yaliyopo, wachimbaji wengi kwa sasa hujikuta wakiuza dhahabu peke yake wakati inapochimbwa inakuwa na madini mengine ambatani, ikiwemo Fedha, Platnum, Brass na mengineyo.

"Kwa mujibu wa sheria ya madini nchini rasilimali hiyo haipaswi kuuzwa ikiwa  katika hali ghafi. Hivyo kiwanda hiki kitakuwa na uwezo wa kubaini madini mengine yaliyopo ndani ya dhahabu, kuyatayarisha kwa maana ya kuyatakasa na kuyapeleka sokoni katika hali ya ubora na viwango vya soko kimataifa." alisema Mugisha.

No comments:

Post a Comment