MAWAZIRI WA SADC SEKTA YA KAZI NA AJIRA KUKUTANA JIJINI DAR ES SALAAM - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 1 March 2020

MAWAZIRI WA SADC SEKTA YA KAZI NA AJIRA KUKUTANA JIJINI DAR ES SALAAM

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Mawaziri wa SADC sekta ya Kazi na Ajira utakaofanyika tarehe 2 – 6 Machi, 2020 Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi Bw. Robert Masingiri (kulia) ni Mratibu wa Kamati ya Habari – Maelezo Bw. Jonas Kamaleki.

Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi Bw. Robert Masingiri akitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa Habari kuhusu Programu ya Mafunzo kwa Vitendo Mahala pa Kazi (Internship) kwa vijana wakati wa mkutano wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama na Waandishi wa Habari.

Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia taarifa ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akiwapa taarifa ya Mkutano wa Mawaziri wa SADC sekta ya Kazi na Ajira katika Ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni Jijini Dar es Salaam.


Na: Mwandishi Wetu

MKUTANO
wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) sekta ya Kazi na Ajira unatarajiwa kufanyika hapa nchini kuanzia tarehe 2 hadi 6 Machi, 2020 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) uliopo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari alieleza kuwa Mkutano huo utafunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Kauli mbiu ya Mkutano huo ikiwa ni “Kukuza Soko la Ajira na Mahusiano Mema Sehemu za Kazi kwa Maendeleo Endelevu”.

Waziri Mhagama amesema kuwa katika Mkutano huo ambao kwa kiasi kikukubwa utawakutanisha Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Kazi na Ajira, Wataalam na Vyama vya Waajiri na Vyama vya Wafanyakazi kutoka Nchi Wanachama wa SADC na utakuwa na lengo la kujadili masuala mbalimbali ya sekta ya Kazi na Ajira katika Ukanda huo wa Afrika.

“Mkutano huu wa Mawaziri, Wataalamu na Wadau wa Utatu wa Sekta ya Kazi na Ajira utatoa fursa ya majadiliano ya pamoja  kwa nchi wanachama wa SADC kuangalia utekelezaji wa maazimio mbalimbali kuhusu masuala ya Kazi, Ajira, Vijana, Uhamaji wa Nguvukazi na Hifadhi ya Jamii”, Alisema Waziri Mhagama.

Alieleza kuwa katika Mkutano huo itazindua rasmi Programu ya Mafunzo ya Uzoefu kwa Wahitimu Mahala pa Kazi (Intership) kwa vijana inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Alieleza kuwa Programu hiyo ni Mahususi kwa vijana wa Kitanzania waliohitimu vyuo mbalimbali hapa nchini na inagharamiwa na Serikali kwa kushirikiana na Waajiri.

“Serikali iliamua kuanzisha Programu hii kwa lengo la kuwapatia fursa vijana ya kupata uzoefu, ujuzi, maadili ya kazi na namna bora ya kuhudumia wateja katika sehemu zao za kazi,” alieleza Mhagama

“Vijana 5,000 wameweza kunufaika na programu hiyo na kati yao vijana wapatao 1,000 waliomaliza muda wao wa mafunzo hayo wameweza kupata ajira katika maeneo mbalimbali,” alisema Mhagama   

Akitaja manufaa ya Programu hiyo ya Mafunzo kwa Vitendo Mahala pa Kazi kwa Vijana kuwa ni pamoja na Kuwawezesha vijana wanaoshiriki kuoanisha ujuzi waliopata kwenye taasisi za elimu na mafunzo pamoja na mahitaji halisi ya ujuzi kwa waajiri; Kuwezesha vijana kujifunza maadili, mtazamo chanya kuhusu kazi pamoja na tamaduni za kuishi mahali pa kazi na Kuwapatia uzoefu wa kazi unaohitajika na waajiri.

Aliongeza kuwa Programu hiyo imeongeza ushirikiano mzuri kati ya waajiri, Serikali na Vijana na imewapa hamasa waajiri kushiriki katika kuwajengea Ujuzi vijana, maadili na weledi unaohitajika katika soko la Ajira.

Aidha, Waziri Mhagama alitoa wito kwa Wananchi ikiwemo wamiliki na Wafanyakazi wa Mahoteli, Migahawa, Vyombo vya Usafiri na sehemu mbalimbali watakazotembelea wageni kuwakarimu na kutoa ushirikiano na ukaribisho unaostahili ili sifa ya nchi iendelee kuwa kielelezo kwa wageni.

No comments:

Post a Comment