MAJALIWA:TUTAHAKIKISHA CORONA HAISAMBAI ZAIDI NCHINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 23 March 2020

MAJALIWA:TUTAHAKIKISHA CORONA HAISAMBAI ZAIDI NCHINI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza katika kikao kazi cha  Mawaziri na Makatibu Wakuu  cha kujadili ugonjwa  wa Corona (COVID- 19) nchini kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Machi 23, 2020. Katikati ni Waziri wa Afya,  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto, Dkt. Zainab Chaula. (Picha na OIfisi ya Waziri Mkuu)


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kufanya tathmini ili kuhakikisha inazuia ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) isiweze kusambaa kwa kiasi kikubwa nchini.

Pia, Waziri Mkuu amevishukuru vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Serikali katika kuelimisha umma namna ya kujikinga na virusi vya corona.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Machi 23, 2020) wakati akizungumza na Mawaziri na Makati Wakuu katika Kikao Kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma.

Imeelezwa kuwa kinga dhidi ya virusi vya corona liwe ni jambo la kimkakati zaidi kuliko kusubiri kutibu, hivyo kwa sasa Serikali imeweka mkazo kwenye kuwahamasisha wananchi kujikinga na virusi hivyo.

“…Mawaziri hakikisheni katika kipindi hiki ziara za kwenda kukagua miradi zielekezwe kwa Wakurugenzi ikibidi kwa Makatibu Wakuu, Mawaziri mnatakiwa mjikite katika kukinga Taifa na corona.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeunda kamati tatu kwa ajili ya kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi ya corona (COVID-19). Kamati hizo ni ya Kitaifa ambayo itaongozwa na Waziri Mkuu na itahusisha baadhi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Kamati ya pili ni ya Makatibu Wakuu  kutoka sekta husika na itaongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi na kamati ya tatu ni ya Kikosi Kazi cha Taifa ambacho kitaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto huku wajumbe wake wakiwa ni wataalamu akiwemo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Awali,Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema katika kipindi cha saa 24 jumla ya watu 292,142 duniani walibainika kuwa na virusi vya corona kati yao watu 12,784 walifariki.

Pia, katika Bara la Afrika watu 736 walibainika kuwa na virusi vya corona na kati yake watu 20 walifariki katika kipindi cha saa 24.

Akizungumzia kwa upande wa Tanzania, Waziri Ummy alisema jumla ya watu 12 walibainika kuwa na virusi vya corona tangu mgonjwa wa kwanza alivyogundulika nchini na kwamba wagonjwa wote hali zao ni nzuri na mmoja amepimwa zaidi ya mara mbili na kubainika kuwa hana virusi.

No comments:

Post a Comment