![]() |
Waziri wa Mambo ya Ndani George Simbachawene |
WATU 20 wamekufa Jumamosi Februari
1, 2020 kutokana vurugu za waumini kukanyangana katika harakati za kujaribu
kufikia mafuta ya upako kwenye kongamano la mahubiri ya Mchungaji Boniface
Mwamposa mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Ndani George
Simbachawene amesema kiongozi huyo wa kidini anatakiwa kuwajibika kwani
hakuchukuwa tahadhari wakati wa kuwakusanya waumini katika ibada hiyo na hivyo
serikali lazima ichukue hatua zinazostahiki.
“Kwa sababu inasikitisha kuna idadi
kubwa ya watu umewakusanya mahala, mwenye jukumu la kuhakikisha usalama wao ni
wewe uliyewakusanya hapo, pamoja na jukumu la serikali kuhakikisha watu wako
salama. Kwa idadi kubwa ya watu kama hiyo unapotoa maelezo au maneno ambayo
yanaweza kusababisha mhemko na watu wakaweza kukimbizana na kufikia hatua ya
kuumia basi una wajibu wa kuwajibishwa katika kosa hilo.
“Kwa hiyo nitoe rai kwa viongozi wa
madhehebu na shughuli za kidini na mikusanyiko mbalimbali kujua kwamba wanao
wajibu wa kuhakikisha usalama wa watu hao. Mchungaji au mtume Boniface Mwamposa
baada ya tukio hili alitaka kukimbia. Lakini hivi ninavyo zungumza yuko katika
mikono ya Jeshi la polisi. Na tunafikiria kumtoa Dar es Salaam kumrudisha Moshi
ili aende akawajibike kwa kosa au madhara haya ya maafa ambayo kwa kweli kwa
uwazi yeye na wenzake wamesababisha,” ameeleza waziri.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi
Warioba alithibitisha taarifa hizo za awali juu ya waumini 20 kufa.
“Taarifa za awali tulizonazo ni kuwa ni waumini 20 wamepoteza maisha lakini tunaendelea kufuatilia maeneo mengine ya zahanati, vituo vya afya na hospitali kama kuna watu walipelekwa huko,” amesema Kippi.
Vyanzo vya habari vinaeleza kuwa
waumini hao walikumbwa na maafa hayo wakati wakikanyagana kwa ajili ya
kugombania kukanyaga mafuta yaliyomwagwa na mhubiri huyo yakidaiwa kuwa na
upako.
Inaelezwa kuwa watu zaidi ya 40
walikanyagana katika harakati za kugombania mafuta ya upako na kukimbizwa
hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.
Idadi ya waliokufa huenda ikaongezeka kwa kuwa hakuna taarifa ya ujumla ya majeruhi waliopelekwa katika vituo vya afya vya jirani pamoja na Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
-VOA
No comments:
Post a Comment