WANARUKWA WALILIA KUGAWANYWA KWA HALMASHAURI YA WILAYA YA SUMBAWANGA KUSOGEZA HUDUMA KWA JAMII - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 14 February 2020

WANARUKWA WALILIA KUGAWANYWA KWA HALMASHAURI YA WILAYA YA SUMBAWANGA KUSOGEZA HUDUMA KWA JAMII

 
Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo


MWENYEKITI wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) wa Rukwa ambaye ni Mkuu wa mkoa huo Mh. Joachim Wangabo ameridhia kupeleka kwenye ngazi husika mchakato wa kuanzishwa kwa Halmashauri mpya itakayotokana na kuigawa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga yenye Tarafa 4, Kata 27, vijiji 114, vitongoji 494 na kilomita za mraba 8,871 baada ya wajumbe 23 wa kamati hiyo kukubaliana na hoja iliyowasilishwa kutokana na kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) ya Sumbawanga.

Mh. Wangabo alisema kuwa kamati imeafikiana kutokana na halmashauri hiyo inayopendekezwa kukidhi vigezo vyote vilivyowekwa na Wizara ya Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa na kuahidi kuwa ofisi yake kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa ushauri huo unatekelezwa na kuongeza kuwa sambamba na kuigawa halmashauri kuna jambo pia la kuigawa jimbo la uchaguzi la Kwela kutokana na jiografia ya jimbo hilo.

“Jimbo hili la Kwela ambalo ni sawasawa na hii halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ina kata 27, kule bonde la Ziwa Rukwa kuna kata 13 kwahiyo iko haja, kwasababu tatizo la kijiografia ni kwamba hii safu ya milima ya inaleta ugumu au changamoto ya usafiri na namna ya kuwafikia wale waliopo bonde la Ziwa Rukwa na lenyewe limetawanyika ni kubwa na pana lakini ukija ukanda wa juu na wenyewe ni mkubwa umetapakaa kwahiyo haya ya kijiografia ni vizuri kuyakaa haya maeneo yakawa ni tofauti ili tuweze kuleta unafuu mkubwa wa maendeleo kwa wananchi wetu,” Alisisitiza.

Aidha, Aliwapongeza wajumbe wote wa kamati hiyo kwa kukubaliana kwa kauli moja bila ya mvutano wa aina yoyote na kuwashukuru viongozi hao kwa kuwa waelewa juu ya kuungana pamoja katika kuhakikisha wanafikisha maendeleo kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa na kuongeza kuwa kitendo hicho kitaacha alama ya uongozi wao kwa wananchi wa Mkoa huo.

Mh. Wangabo ameyasema hayo wakati akifunga kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) chenye wajumbe 23 wakiwemo wakuu wa wilaya, wabunge wa mkoa, wenyeviti wa halmashauri, wakurugenzi wa halmashauri pamoja na Mwenyekiti na katibu ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa.

 Awali wakati akichangia katika hoja hiyo Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule alisema kuwa Kikao cha kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilipendekeza endapo jambo hilo la kuigawa halmashauri itashindikana basi ni vyema baadhi ya kata zilizopo halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga zikakabidhiwa kwa manispaa ya Sumbawanga ili kupunguza ufuatiliaji wa huduma za kiutawala katika makao makuu ya sasa ya halmahsuri hiyo ya Wilaya.

“Mheshimiwa Mkuu wa mkoa kutoka makao makuu ya halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga katika mji mdogo wa Laela hadi kufika kata ya Kifinga ni mwendo wa kilomita Zaidi ya 200 na hivyo kusababisha wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kushindwa kufika kwa urahisi katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kwaajili ya mahitaji ya kiofisi na hivyo kwenye kikao yalipokewa mapendekezo kwamba kata nne ambazo zipo mbali na makao makuu ya halmashauri basi zihamishiwe manispaa ya Sumbawanga,” Alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kwela Mh. Ignus Malocha alisema kuwa suala la kufuatilia kuanzishwa kwa halmashauri mpya pamoja na jimbo jipya walianza tangu mwaka 2014 lakini baada ya Tume ya Uchagu kutoa majibu, yalionekana maeneo mengine yamekubaliwa kugawanywa lakini jimbo hilo la Kwela halikuonekana kufanyiwa kazi.

Katika upande Mwengine wajumbe wa kikao hicho wamekubaliana kuanzisha mchakato wa kuanzishwa kwa huduma ya reli kutoka katika mji wa Tunduma, Mkoani Songwe hadi katika bandari ya Kasanga katika Wilaya ya Kalambo, Mkoani Rukwa ambapo reli hiyo itaunganishwa kutoka katika reli ya TAZARA inayohudumia kutoka Tanzania kwenda Zambia.

No comments:

Post a Comment