TMA YATABIRI MVUA ZA MASIKA ZINAZOTARAJIA KUANZA MWEZI MACHI HADI MEI, 2020 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 13 February 2020

TMA YATABIRI MVUA ZA MASIKA ZINAZOTARAJIA KUANZA MWEZI MACHI HADI MEI, 2020

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk. Agnes Kijazi akitoa utabiri wa mvua za masika kwa kipindi cha Machi hadi Mei, 2020 leo jijini Dar es Salaam kwa wanahaabari (hawaapo pichani). 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk. Agnes Kijazi (kushoto) akitoa utabiri wa mvua za masika kwa kipindi cha Machi hadi Mei, 2020 leo jijini Dar es Salaam kwa wanahaabari (hawaapo pichani). Kulia ni Kaimu Meneja wa Huduma za Utabiri TMA, Wilberforce Kikwasi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk. Agnes Kijazi (kulia) akifafanua jambo kwa wanahabari (hawapo pichani) alipokuwa akitoa utabiri wa mvua za masika kwa kipindi cha Machi hadi Mei, 2020 leo jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Mtaalam wa Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Bi. Rose Senyagwa pamoja na Mkurugenzi Huduma za Utabiri TMA, Dk. Hamza Kabelwa.

Mtaalam wa Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Bi. Rose Senyagwa (kushoto) akieleza jambo kwa wanahabari (hawapo pichani) kwenye utabiri wa Mvua za Masika zinzotrajia kuanza Mwezi Machi hadi Mei, 2020 leo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk. Agnes Kijazi (wa pili kulia) akifafanua jambo katika mkutano huo. Kutoka kushoto ni Mtaalam wa Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Bi. Rose Senyagwa, Mkurugenzi Huduma za Utabiri TMA, Dk. Hamza Kabelwa pamoja na Kaimu Meneja wa Huduma za Utabiri TMA, Wilberforce Kikwasi (Wa kwanza kulia).


MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) leo imetangaza utabiri wa Mvua za Masika zinzotrajia kuanza Mwezi Machi hadi Mei, 2020 huku ikizitaka Mamlaka za Miji na sekta anuai husika kujipanga ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa tarajiwa kipindi chote.

Akizungumza na wanahabari leo alipokuwa akitoa utabiri huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk. Agnes Kijazi amesema mvua za masika kwa kipindi cha Machi hadi Mei, 2020 zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba, maeneo mengi ya mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro. Alisema hali kama hiyo pia inaatarajiwa maeneo ya mashariki mwa mkoa wa Geita pamoja na mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara.

Dk. Kijazi amesema kwa maeneo ya mkoa wa Kagera, magharibi mwa mkoa wa Geita, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Pwani na Kisiwa cha Mafia pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.

Aidha ameongeza kuwa mvua za nje ya msimu zinazoendelea kunyesha katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, hususan yaliyopo katika pwani ya kaskazini zinatarajiwa kuendelea na kuungana na msimu wa mvua wa Masika 2020.

Aidha, maeneo ya magharibi mwa Ziwa Viktoria na maeneo mengine ya pwani ya kaskazini Mikoa ya Dar es salaam, Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro alibaaainisha yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.

"...Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya mashariki mwa mkoa wa Geita, mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara. Aidha, mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kagera, magharibi mwa mkoa wa Geita na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma Wilaya za Kakonko na Kibondo. Mvua hizi zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili ya mwezi Machi, 2020 na kuisha kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Mei, 2020," alisema Dk. Kijazi.

Hata hivyo kwa maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, kwa Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro aliongeza kuwa mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi; ambazo pia zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi, 2020 na kuisha kati ya wiki ya pili na tatu ya mwezi Mei, 2020.
 Akitoa tahadhari kwa sekta za Kilimo, Usalama wa Chakula, Samaki na Mifugo alisema mvua za wastani hadi juu ya wastani zinaweza kufaa kwa uzalishaji wa mazao ikiwa ni pamoja na yale yanayoweza kustawi kwenye unyevunyevu wa udongo uliopitiliza kama vile mpunga.

Pamoja na hayo TMA imezitaka sekta hizo kujipanga kwani wadudu waharibibu na magonjwa vinaweza kujitokeza kutokana na hali ya umajimaji na maji yaliyotuama hivyo kuangalia namna ya kukaabiliana na hali hiyo ikijitokeza.

Hata hivyo, magonjwa ya mifugo kama vile homa ya bonde la ufa, ugonjwa na kwato na midomo yanaweza kujitokeza, hivyo wakulima wanashauriwa kuchukua hatua stahiki za kudhibiti mmomonyoko wa udongo na kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.

"...Sekta ya uvuvi inaweza pia kuathirika kutokana na uwezekano wa ongezeko kubwa la maji katika mabwawa ya kufugia samaki, hivyo wafugaji wa samaki wanashauriwa kuimarisha miundombinu ya mabwawa yao.  Aidha, katika maeneo ambayo mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa, wakulima wanashauriwa kupanda mazao yanayokomaa mapema na yasiyohitaji maji mengi katika ukuaji wake. Jamii inashauriwa kuhifadhi malisho na kuvuna maji ya mvua kwa matumizi ya baadaye.
 
TMA imezishauri Mamlaka za Miji kuchukua tahadhari kwani miundombinu na huduma za maji safi na maji taka zinaweza kuathirika, hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

"...Mamlaka za Miji pamoja na wananchi wanashauriwa kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa miundombinu pamoja na njia za kupitisha maji zinakuwa wazi na safi ili kuepusha mafuriko na athari nyingine zinazoweza kutokea kutokana na maji kutuama. Kwa Sekta ya Afya mvua za wastani hadi juu ya wastani zinazotarajiwa, zinaweza kusababisha kutuama kwa maji na kuweka mazingira mazuri kwa mazalia ya mbu na hivyo kusababisha matukio ya kuongezeka kwa ugonjwa wa malaria.

Aidha, kwa maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, kuna uwezekano wa jamii kutumia maji ambayo sio salama na hivyo kupelekea kuwepo kwa magonjwa ya milipuko mfano ugonjwa wa kuhara na homa ya matumbo. Hivyo, jamii na mamlaka husika wanashauriwa kuchukua hatua stahiki ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

TMA pia katika utabiri huo, imeeleza mvua kubwa inaweza kusababisha mafuriko na watu kupoteza maisha, kutokea uharibifu wa muindombinu na mali nyingine, hivyo kuzishauri mamlaka za maafa na wadau kwa ujumla kuchukua hatua stahiki za kujiandaa na kukabiliana kikamilifu na athari zinazoweza kujitokeza.

No comments:

Post a Comment