SERIKALI za Uganda
na Rwanda, Jumapili zilikubaliana kubadilishana wafungwa, katika juhudi za
kupunguza uhasama baina yao, baada ya kushutumiana kwa mda mrefu na kufanyiana
ujasusi unaotajwa na wachambuzi kama wenye lengo la kutatiza amani ya kila
upande.
Rais wa Rwanda Paul Kagame, na
mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni ambao walikuwa marafiki wakubwa sana kabla
ya kutofautiana, walifikia makubaliano hayo katika kikao cha mjini Luanda,
Angola.
Viongozi hao hao walisaini mkataba
wa ushirikiano katika kurejesha hali ya utulivu baina yao, mwezi Agosti mwaka
uliopita, lakini utekelezaji wake umekosa kasi ilivyiotarajiwa.
Japo hakuna taarifa zaidi zimetolewa
kuhusu makubaliano ya jumapili, inafahamika kwamba viongozi hao wawili
walikubaliana kubadilishana wafungwa katika kikao kitakachofanyika Februari 21,
kwenye mpaka uliofungwa kati ya Rwanda na Uganda, mjini Katuna .
Kikao cha Angola kilisimamiwa na
rais Joao Lourenco, na kuhudhuriwa na rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo
Felix Tshisekedi.
Katika taarifa ya kurasa mbili yenye
vipengele 8 iliyotolewa na ikulu ya rais wa Angola, viongozi hao waliahidi kushirikiana
katika kuimarisha amani, utulivu, ujirani mwema na kuaminiana.
“Pande zote mbili zinatakiwa
kujizuia na vitendo vinavyoweza kuleta hali ya kutoaminiana au uhasama,
kuhusiana na madai ya kufadhili makundi yenye lengo la kutatiza serikali zake,”
kinasema kipengele cha pili, aya ya saba ya taarifa hiyo fupi.
Wiki iliyopita, rais wa Rwanda Paul
Kagame alisema kwamba hatashurutishwa kufungua mpaka kati ya Rwanda na Uganda
hadi serikali ya rais Yoweri Museveni itakapotimiza matakwa ya serikali ya Rwanda
ambayo ni pamoja na kuachilia huru raia wake wote wanaozuiliwa katika magereza
ya Uganda.
Rwanda ilifunga mpaka wake mwezi
Februari mwaka uliopita na kupiga marufuku biashara kati yake na Uganda.
Hakuna taarifa iliyotolewa iwapo
Rwanda ipo tayari kufungua mpaka wa Katuna ili kuruhusu raia wake kuingia
Uganda, au Kuruhsu bidhaa za Uganda kuingia Rwanda.
Rwanda inaishutumu Uganda kwa
kufadhili makundi ya waasi yenye lengo la kupindua serikali ya rais Paul
Kagame.
-Imetayarishwa na Kennes Bwire, Washington
DC.
-VOA
No comments:
Post a Comment