RC NCHIMBI ATUMIA QURAN NA BIBLIA KUWAFUNDA WALIMU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 10 February 2020

RC NCHIMBI ATUMIA QURAN NA BIBLIA KUWAFUNDA WALIMU

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt Rehema Nchimbi (aliyeshika kisemeo) akiongoza mkutano wa wadau wa elimu wa mkoa huo, kulia kwake ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida  Dkt. Angelina Lutambi, anayefuata ni Afisa Elimu Mkoa wa Singida Mwalimu Nelasi Aron Mulungu.

Wanafunzi ambao ni wasichana rika  ndani shule za msingi katika kijiji cha Nkwae katika Wilaya ya Singida DC  wakisubiri kupokea fedha   jumla ya shilingi kwa ajili ya mahitaji ya kishule ili kuepuka  vishawishi vinavyowafanya  washindwe kufanya vizuri kwenye  masomo yao kushoto ni Julius Nusu Kaimu Mratibu wa   Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF Wilaya ya Singida akitoa maelekezo kwa wazee na wanafunzi.




Na John Mapepele


“MSHIKE sana huyo elimu msimwache aende zake pia mtafute hadi Uchina”  ni maneno aliyoyasema leo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi katika kikao kazi cha wadau wote  wa elimu kwenye Mkoa wa Singida kutafakari ufaulu wa wanafunzi kwenye Shule za Msingi na Sekondari  ambapo amesema  mkakati wa mwaka 2020  ni kwamba Mkoa wa wake lazima uwe miongoni  mwa kumi bora.


Kwa mujibu wa Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Mwalimu Nelasi Mulungu  kwa matokeo ya mitihani ya mwaka 2019 Mkoa ulishika nafasi ya  22 kitaifa  kwa Shule za Msingi na  nafasi ya 21 kwa Kidato cha Nne na nafasi ya 2 kwa mitihani ya Kidato cha Sita.


Kikao kazi hicho kilikuwa na kauli mbiu “Timiza Wajibu Ongeza ufaulu”  ni cha aina yake kilicho washirikisha  wadau wote wa elimu ambapo Mkuu wa Mkoa  alisema  kuwa  kama Singida unaweza kushika nafasi ya pili  kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita 2019 pia unaweza kushishika nafasi ya kwanza  katika mitihani yote kinachotakiwa ni kutafakari  na kuweka mkakati wa pamoja kwa wadau wote.


Dkt. Nchimbi ambaye pia kwa taaluma ni mwalimu aliyeanzia shule za msingi hadi  vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi alitumia muda mwingi kutoa maneno  kutoka  katika vitabu vitakatifu vya mungu vya Quran na  biblia akisisitiza kuwa   vitabu hivyo vyote  vimesisitiza  kuitafuta kwa bidii elimu  ambapo alisema wadau wa elimu wanapaswa  kutafakari  kwa kina  ni kwa nini elimu imeendelea kushuka katika mkoa huo wakati wao wana wajibu na kwamba kutowafaulisha watoto  ni dhambi kubwa.




“Nasema kwa dhati ya  moyo wangu  uchina  katika dunia hii ni Singida watu wanatakiwa kutoka mataifa yote kuja kutafuta elimu hapa kwetu na watu wa kuifanya  iwe Uchina ni nyie”alisisitiza Dkt Nchimbi 


Katika kikao hicho Dkt nchimbi alikataa utaratibu wa kawaida wa  kikao wa kuanza kusoma taarifa  za maendeleo ya elimu  na badala yake akaelekeza  kuanza  na ajenda ya kila mshiriki kueleza  nini kifanyike ili kuboresha ufaulu wa wananfunzi.



Alisema  kutokana na kile alichokiita  dhambi ya baadhi ya walimu kutotekeleza wajibu wa kutoa elimu  kwa kijituma  Mungu amekuwa  akiwaadhibu na kujikuta wanapata matatizo makubwa ya kiuchumi na kijamii.


“Mungu anatoa adhabu hapa hapa duniani   baadhi ya walimu wanaacha kuwafundisha watoto kwa bidii unakuta waingia mikopo kwa wakopeshaji haramu  ambao wana wakopesha milioni tatu wanalipa milioni ishirini na ATM kadi zao zinachukuliwa na hao matapeli” aliongeza Dkt. Nchimbi.


Hatimaye Mkuu wa Mkoa akapiga marufuku tatu ili kunusuru  kushuka kwa ufaulu katika mkoa wake.


Alipiga marufuku kwa wakopeshaji haramu kuendelea kuwakopesha  walimu ambapo aliwaelekeza wakuu wote wa wilaya kwenye Mkoa wa Singida kuanzisha operesheni maalum ya kuwasaka wakopeshaji haramu na kuwachukulia hatua kali za kisheria.


Aidha alipiga marufuku kwa kwa wenye mabanda ya kuonyeshea video kuwaingiza wanafunzi  na kutaka Kamati za Ulinzi na Usalama za kila wilaya kuwakamata  wenye  vibanda ambapo alisema  hakuna yeyote anayevunja sheria atakayepona  na kwamba wazazi  wanafunzi wanaoshinda kwenye mabanda hayo watafuatiliwa kikamilifu ili pia sheria ichukue mkondo wake  kwa kuwa nao ni wadau wakuu katika kuhakikisha kuwa watoto wao wanahudhuria masomo kikamilifu..


Marufuku ya mwisho ilikuwa katika suala la wanafunzi kucheza michezo ya kamali katika  nyumba za starehe  ambapo alisema  nyumba  ziutakazobainika zikiwaingiza wanafunzi zitachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufungiwa biashara hizo.



Awali kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Singida Mwalimu, Nelasi Mulungu  kipaumbele cha Mkoa ni kuongeza ufaulu katika mitihani yote, kuboresha miundombinu, kupambana na utoro, kuongeza samani na kuboresha ufundishaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kwa Mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya mwaka 1995 kila shule ya msingi ni lazima iwe na darasa la awali.  

 Hivyo Mkoa una jumla ya madarasa ya awali 536 kwa upande wa shule za Serikali na shule 30 za awali zisizo za Serikali.



Amesema, Mkoa wa Singida una shule za msingi 569 kati ya hizo shule 536 ni za Serikali na shule 33 ni za Watu binafsi, Taasisi na Mashirika ya Dini.  Kwa shule za msingi hali halisi ya mahitaji ya Walimu Kimkoa ni 9,885 ikilinganishwa na waliopo 5,292 sawa na asilimia 53.5. Upungufu wa Walimu wa shule za msingi ni 4,593.


Kwenye matokeo ya kuhitimu elimu ya msingi ufaulu umekuwa ukiongezeka sambamba na idadi ya wanafunzi kwa kila Halmashauri hivyo kwa mwaka 2017 wanafunzi waliofaulu ni 17,863, mwaka 2018 ni 20,617 na mwaka 2019 ni 22,484.


Katibu Tawala Mkoa wa Singida  Dkt. Angelina Lutambi alisema  katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Joseph Magufuli imetoa zaidi ya bilioni 50 katika eneo  la elimu  pekee na kwamba  fedha hizo ni nje ya mishahara ya walimu.


Alisema  walimu na wadau wote wa elimu wanapaswa  kushirikiana  ili kuinua kiwango cha ufaulu kwa kuwa Serikali tayari imeshatekeleza wajibu wake wa kuwawezesha kwa kiasi kikubwa.


Alipongeza jitihada za Mhe. Rais  Magufuli za kuwezesha  kwenye sekta mbalimbali ambapo alisema  uwezeshaji umekuwa wa kiwango cha juu kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni watumishi wa Serikali kuunga mkono juhudi hizi kwa vitendo.


Alisema kauli mbiu ya mwaka huu ya “Timiza Wajibu Ongeza ufaulu” ndiyo mwongozo na dira  katika Sekta ya Elimu kwenye Mkoa wa Singida hivyo bila kutimiza wajibu wa kila mdau nhakutakuwa na ufaulu wowote  na kuwataka walimu kusimamia viapo vyao.

No comments:

Post a Comment