SERIKALI imetoa agizo kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) katika mikoa yote kusimamia Wakandarasi waliopo katika miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa kwa kuzingatia ubora katika matabaka yote ya ujenzi ikiwemo ujenzi wa makalvati yenye uimara ili kulinda barabara zetu ziweze kuishi miaka mingi zaidi.
Aidha, imesisitiza kuwa inataka kuona fedha zinazotumika katika miradi hiyo ikiendana na ubora ili kuipunguzia gharama kubwa za matengenezo ya barabara hasa vipindi hivi vya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hapa nchini.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Tabora ya kukagua athari kubwa zilizotokana na mvua kubwa kunyesha katika miundombinu ya barabara iliyokamilika na ile inayoendelea kutekelezwa ambapo ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa barabara ya Usesula - Komanga yenye urefu wa kilometa 117 inayojengwa kwa kiwango cha lami.
"Nimefurahishwa na mradi huu kwani mwaka jana nilipita hapa kwenye barabara za mchepuo lakini leo nimepita kwenye lami imara", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo ukikamilika mapema utaufungua mkoa wa Tabora na Katavi kwa kiwango cha lami na hivyo kufanya Sera ya Awamu ya Tano ya kuunganisha mkoa kwa mkoa inaendelea kutimia.
Naibu Waziri Kwandikwa, amesema kuwa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo unaojengwa na mkandarasi Jiangxi Geo - Engineering umefikia asilimia 39.7 huku kilometa 43.2 tayari zimeshawekwa lami.
Naibu Waziri huyo amesema kuwa wao kama Wizara wako tayari kutoa ushirikiano kwa mkandarasi na TANROADS ili mradi huu ukamilike kwa wakati.
Amesisitiza kuwa mbali na kazi nzuri zinazofanywa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa ajili ya usimamizi wa miradi mikubwa Serikali inaendeelea kutoa fedha kwa ajili ya kufungua mikoa yote ya nyanda za magharibi kwa mtandao wa lami.
"TANROADS msimamie Mkandarasi huyu tunataka kazi ziende kwa kasi lakini zishikamane na ubora zaidi", amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Awali akitoa taarifa ya mradi kwa Naibu Waziri huyo Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Tabora Eng. Raphael Mlimaji, amemuhakikishia Naibu Waziri huyo kumsimamia mkandarasi kwa karibu na kuhakikisha hakuna dosari zozote zitakazoweza kujitokeza siku za usoni.
Ameongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo unatumia aina ya lami (superpaved) ambayo ni imara sana na yenye kumudu vipindi vya baridi na joto.
No comments:
Post a Comment