BENARD MEMBE: FAHAMU SABABU ZA VIGOGO WA CCM KUHOJIWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 6 February 2020

BENARD MEMBE: FAHAMU SABABU ZA VIGOGO WA CCM KUHOJIWA

Membe adai kuitwa katika kamati ya maadili ni jambo la muhimu kwake


CHAMA tawala nchini Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM) hii leo kimeanza kuwahoji makada wake watatu waandamizi akiwemo waziri wa zamani wa Mambo ya Nje Bernard Membe.

Makada wengine wawili ni makatibu wakuu wa zamani wa chama hicho Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba.

Mwezi Disemba, Halmashauri kuu ya CCM (NEC) iliagiza makada hao watatu kuhojiwa, hatua hiyo ilitimu baada ya 'vuta n'kuvute' ya muda ndani ya chama hicho.

Makada wote hao, "wanakabiliwa na tuhuma za maadili kwa mujibu wa Katiba ya Chama na Kanuni ya Maadili na Uongozi."

"Kukidhalilisha chama mbele ya Umma"

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole Disemba 13 2019, hata hivyo haikueleza bayana ni makosa gani ya kimaadili ambayo wanatuhumiwa nayo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, makada wengine watatu, Januari Makamba, Nape Nnauye na William Ngeleja walisamehewa baada ya kumuomba radhi mwenyekiti wa CCM, Rais John Pombe Magufuli.

Wanachama hao waliomba radhi kwake (Magufuli) baada ya "kukiri mbele yake kufanya makosa ya kimaadili yaliyokidhalilisha chama na viongozi wake mbele ya umma," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Wanachama hao watatu wa CCM pamoja na watatu ambao wanahojiwa hii leo wote sauti zao, wakiwa wakifanya nawasiliano kwa njia ya simu zilivujishwa kwenye mitandao nchini Tanzania wakizungumzia masuala mbalimbali kukihusu chama na mwenyekiti wake.

Sehemu ya mazungumzo yaliyovuja ya Mzee Yusuf Makamba na Kinana ni pamoja na kuandaa taarifa ya malalamiko dhidi ya 'mawanaharakati' Cyprian Musiba ambaye wanamtuhumu kwa 'kuwadhalilisha' bila kuchukuliwa hatua yoyote na kuhoji analindwa na nani.

•    Je, viongozi wastaafu wa CCM wanaweza 'kumzuia' Rais Magufuli 2020?

Kwa upande wa Membe, licha ya kusikika kwe nye mazungumzo hayo yalivuja, amekuwa pia akituhumiwa na baadhi ya wanchama wa chama hicho kuwa najipanga 'kumhujumu' Magufuli katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Kinana (kushoto) alikuwa Katibu Mkuu wa CCM wakati Magufuli akiingia madarakani

Membe anahusishwa na mipango ya kutaka kugombea tiketi ya urais kupitia CCM mwaka huu, hatua ambayo baadhi wanaitafsiri kama usaliti.

Japo katiba ya CCM inaruhusu hilo, imekuwa ni ada ya chama kumuachia rais aliye madarakani kupita bila kupingwa kwa awamu ya pili ya urais.

Watahojiwa kwa namna gani?


Wanachama hao waandamizi wanahojiwa Dodoma na kamati ya usalama na maadili ambayo ipo chini ya uenyekiti wa mwanasiasa mkongwe Philip Mangula, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara.

Membe alikuwa wa kwanza kufika kwa mahojiano hayo Alhamisi asubuhi, na kwa mujibu wa Mangula baada yake atafuata Kinana kisha Makamba.

Kila mmoja anatarajiwa kuhojiwa kwa siku moja.

"Tumepanga kuwahoji kwa siku moja kila mmoja, lakini utaratibu unaweza kubadilika kulingana na maelezo atakayotoa mhusika. Kama tutaona siku moja haitoshi, atarejea tena siku inayofuatia," Mangula amenukuliwa akisema na gazeti la Uhuru.

Kwa mujibu wa Mangula baada ya kuhitimisha kazi yao, vikao ya chama vitapitia maelezo ya watuhumiwa hao na kutoa maamuzi.

Baada ya mahojiano ya saa tano Membe amewaambia waandishi wa habari kuwa alikuwa na mkutano mzuri.

"Nimepata nafasi nzuri ya kufafanua mambo kadhaa ambayo chama changu ilitaka kuyajua...Safari hii ya kuja Dodoma imekuwa na manufaa makubwa sana, sana kwangu, kwa chama na kwa taifa letu...mengine yatakuwa yanapatikana kidogo kidogo nikishiba," amesema Membe.

Watapewa adhabu gani?


Swali moja ambalo wengi wanajiuliza toka mwezi Disemba ni adhabu gani wanayoweza kupatiwa makada hao waandamizi endapo watakutwa na hatia.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la 2017 zimebainisha adhabu tatu kwa wanachama wanaofika mbele ya kamati hiyo.

"Katika kanuni hizo kifungu cha 5(2) kinasema; wanachama wanaovunja maadili ya chama kama yalivyoainishwa katika katiba ya CCM na kanuni za CCM wanachukuliwa hatua za kuwarekebisha na kama itashindikana kuwarekebisha ni kuwaondoa katika chama au katika uongozi," linaripoti gazeti hilo.

-BBC

No comments:

Post a Comment