Na Ramadhani Kisimba, WFM-Dodoma
SERIKALI ya Tanzania itanufaika na msaada wa dola za Marekani milioni
600 zitakazotolewa na Taasisi ya Global Fund mwezi Januari mwakani kwa ajili ya
kusaidia kukabiliana na maradhi ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria katika kipindi cha miaka mitatu.
Ahadi hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Mkuu wa Mfuko huo Barani Afrika
Bw. Linden Morrison, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na
Mipango Jijini Dodoma.
Amesema kuwa fedha hizo sawa na takriban shilingi za Tanzania trilioni
1.4 zitatumika kuimarisha afya kwa kupambana na magonjwa ya Ukimwi, Kikufua
Kikuu na Malaria ambapo vifaa tiba na vitendanishi mbalimbali vitanunuliwa
kupitia msaada huo katika kipindi cha miaka mitatu (2021-2023).
Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka 15 ambacho taasisi yake imekuwa
na uhusiano mzuri na Tanzania, Mfuko wake tayari umetoa msaada wa dola za
Marekani bilioni 2 kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya hususan katika mapambano
dhidi ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameishukuru Taasisi hiyo
ya Kimataifa ya Global Fund kwa mchango mkubwa iliyoipatia Tanzania katika
mapambano dhidi ya magonjwa hayo hasa malaria, ugonjwa unaoongoza kusababisha
vifo vya watanzania wengi.
Dkt. Mpango aliahidi kwamba fedha hizo zitatumika kikamilifu na kama
ilivyokusudiwa ili zilete matokeo chanya kwa kuwafikia walengwa nchini kote.
‘‘Nimefurahi kwa sababu nina
matumaini kuwa tumepata nguvu ya kupambana na magonjwa haya makubwa, ili
Watanzania wawe na afya njema na waweze kujenga uchumi wa nchi yao’’ Alisema
Mhe. Mpango.
Aidha Dkt. Mpango alisema katika kikao hicho wamejadili namna ya
kuboresha zaidi ushirikiano uliopo kati ya pande hizo mbili ikiwemo kuangalia
namna ya kutoa msamaha wa kodi kwenye vifaa yakiwemo magari ya kubebea wagonjwa
na dawa zinazoingizwa nchini na Taasisi hiyo kwa ajili ya mradi huo.
“Aidha, Ili kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na Taasisi ya Global
Fund, nchi itahakikisha inakuwa na ushiriki mpana katika Bodi ya Wakurugenzi ya
Mfuko huo ili sauti ya nchi iweze kusikika zaidi” aliongeza Dkt. Mpango
Kuhusu ubadhirifu wa zaidi ya dola za Marekani 400,000 zinazodaiwa
kufujwa na baadhi ya Watendaji wa Serikali wanaotekeleza mradi huo hapa nchini,
Dkt. Mpango ameuahidi Mfuko huo kwamba Serikali itachunguza na kuwachukulia
hatua kali watu wote waliohusika na vitendo hivyo.
No comments:
Post a Comment