PAUL MAKONDA APIGWA MARUFUKU KUINGIA MAREKANI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 31 January 2020

PAUL MAKONDA APIGWA MARUFUKU KUINGIA MAREKANI


 
Marekani inamshutumu Makonda kwa kushiriki katika ukandamizaji wa haki za binaadamu Tanzania.

MKUU wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, apigwa marufuku kuingia Marekani.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani leo Ijumaa, Januari 31 2020 marufuku hiyo pia inamhusisha mke wa Makonda Bi Mary Felix Massenge.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makonda anashutumiwa kwa kushiriki katika ukandamizaji wa haki za binaadamu.

Ukandamizaji wa haki ambao Makonda anashutumiwa kuutenda ni pamoja na kunyima watu haki ya kuishi, haki ya uhuru wa kujiamulia mambo na usalama wa watu.

"Wizara ina taarifa za uhakika kuwa Makonda amehusika katika uvunjifu huo wa haki kupitia nafasi yake kama mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam. Katika nafasi yake hiyo, pia amelaumiwa kwa kukandamiza upinzani wa kisiasa, kukandamiza haki ya kujieleza, na kushambulia makundi yasiyo na sauti," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Michael Pompeo ametumia mtandao wake wa Twitter kutangaza marufuku hiyo.



"Leo tumetangaza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Christian Makonda kuwa hataruhusiwa kuingia Marekani kwa kushiriki kwake katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu. Tuna wasiwasi mkubwa juu ya kuporomoka kwa heshima ya haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania," ameeleza Pompeo katika ujumbe wake huo.

Taarifa hiyo ya serikali ya Marekani pia imeikosoa Tanzania juu ya hali ya haki za binaadamu,
" (Hali hiyo) inajumuisha matendo ya viongozi yanayokandamiza uhuru wa kujieleza, uhuru wa jumuiya, uhuru wa kukusanyika kwa amani, kukandamiza makundi yasiyo na sauti na upinzani wa kisiasa na kutishia maisha.

"Hatua hizi dhidi ya Paul Christian Makonda zinatilia mkazo hofu yetu ya kuvunjwa kwa haki za binadamu Tanzania pamoja na kuunga mkono kwetu uwajibikaji kwa wale wote wanaohusika katika ukandamizaji huo. Tunaitaka serikali ya Tanzania kuheshimu haki za binadamu na za msingi kama uhuru wa kujieleza, jumuiya na mikusanyiko ya amani," imeeleza taarifa hiyo.

-BBC

No comments:

Post a Comment