WATAALAMU WA MAABARA WAIPONGEZA SERIKALI KWA KUBORESHA MAABARA NCHINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 3 December 2019

WATAALAMU WA MAABARA WAIPONGEZA SERIKALI KWA KUBORESHA MAABARA NCHINI

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maabara ya Vetenari Tanzania, Dkt. Furaha Mramba akifafanua umuhimu wa kuwa na maabara zenye uwezo wa uchunguzi na utambuzi wakati wa mkutano wa mwaka kwa wataalam wa maabara waliokutana kwa kutumia dhana ya Afya  moja  inayojumuisha  sekta za Afya ya Binadamu , Wanyamapori, Mifugo na mazingira, jijini Arusha.

Mratibu wa Mradi wa Kuwezesha Maabara nchini kutoka Finland, Dkt. Mika Aho , akifafanua umuhimu wa mradi huo katika kuimarisha maabara kwenye uchunguzi na utambuzi wakati wa mkutano wa mwaka kwa wataalam wa maabara waliokutana kwa kutumia dhana ya Afya  moja  inayojumuisha  sekta za Afya ya Binadamu , Wanyamapori, Mifugo na mazingira, jijini Arusha.

WATAALAMU wa maabara nchini kutoka sekta ya Afya ya binadamu, Afya ya wanyamapori, mifugo na mazingira wameipongeza serikali ya awam ya tano kwa jitihada zake za kuboresha maabara za sekta hizo kwa kuziwezesha kuwa na vitenganishi, vifaa vya kisasa, teknolojia  na kuwajengea ujuzi wataalam hao ili kuweza kufanya utambuzi na uchunguzi ndani ya maabara.

Akiongea wakati wa mkutano wa mwaka wa Mtandao wa wataalam wa maabara nchini (LABSNET), Jijini Arusha,  Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maabara ya Vetenari Tanzania, Dkt. Furaha Mramba amefafanua kuwa kutokana na jitihada za serikali katika kuimarisha kuboresha utendaji wa maabara nchini, tayari maabara za hapa nchini zinao uwezo wa kutambua magonjwa yote yanayowapata mifugo lakini pia na magonjwa yanayowapata binadamu.

“Zamani tulikuwa tunapeleka sampuli nje ya nchi hususani katika nchi ya Kenya na katika nchi ya Afrika kusini, lakini miaka ya hivi karibuni kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na serikali katika kuboresha utendaji wa maabara tulizonazo, tayari tunazo maabara za rufaa ambazo zinauwezo mkubwa wa kufanya utambuzi na uchunguzi wa magonjwa” Amesisitiza Dkt. Mramba.

Dkt. Mramba ameongeza kuwa lengo la kukutana kwa wataalam wa maabara nchini kutoka katika sekta zote za Afya ni kujadiliana na kuona mbinu bora za kufanya uchunguzi na kutambua kwa wepesi na kwa haraka magonjwa kabla hayajaleta madhara makubwa kwa mifugo na binadamu. Amefafanua kuwa katika mkutano huo wameshiriki wadau wa maendeleo katika sekta ya maabara kutoko Marekani na Finland.

“Tunapokutana na wadau hawa ambao hutufundisha teknolojia za kisasa za maabara na hutupatia vifaa vyenye uwezo mkubwa wa utambuzi wanaweza kujua ni teknnolojia gani tunaihitaji kwa sasa na maabara gani zinahitaji kujengewa uwezo katika uchunguzi na utambuzi. Wadau hawa kwa jinsi wanavyo unga juhudi za serikali ndio maana sekta ya maabara hapa nchini  imekuwa bora,” Amesema Dkt. Mramba.

Kwa upande wake Mratibu kutoka Finland wa Mradi unaotekelezwa hapa nchini wa Kuimarisha Afya na Usalama katika Maabara kwa kujenga uwezo wa Utambuzi, Dkt.Lina Voutilainen, amebainisha kuwa wamekuwa wakiunga  mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuboresha utendaji wa maabara nchini kupitia Wakala wa Maabara ya Vetenari Tanzania kwa kuwajengea uwezo wataalam wa maabara na kuwapatia vifaa vyenye uwezo mkubwa wa utambuzi na uchunguzi wa magonjwa.

“Tayari kupitia Wakala wa Maabara ya Vetenari Tanzania tumetoa vifaa  sita vya QPCR vinavyohamishika kwa maabara zake za kanda ya Mwanza, Arusha na Iringa, Tutaendelea kutoa vifaa hivyo vya kisasa na vitenganishi pamoja na kuendelea kuwajengea uwezo wataalam wa maabara katika kipindi tutakachotekeleza mradi huu hadi 2023,” Amesisitiza Voutilainen.

Naye,  Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Uchunguzi, kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Alex Magesa, amefafanua kuwa katika kuhimarisha Huduma za uchunguzi imebainika kuwa usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni changamoto kubwa hivyo tayari serikali imeandaa mpango mkakati wa kukabiliana na changamoto hiyo ambapo wafamasia na wanafuzi  na jamii kwa ujumla wanahusishwa katika kukabili changamoto hiyo.

Mkutano huo ulioratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kupitia Dawati la Uratibu wa Afya moja, uliwakutanisha wataalam wa maabara hao kwa kuzingatia dhana ya Afya moja ambayo ni wataalam wa maabara kutoka sekta ya Afya ya binadamu, Afya ya wanyamapori na mifugo pamoja na mazingira.

No comments:

Post a Comment