Wanafunzi wa Shule ya Msingi Chem Chem mjini Sumbawanga. |
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Winnie Kijazi. |
Hayo yalianza kusemwa na Afisa Elimu Mkoa wa Rukwa Nestory Mloka baada ya kutoa taarifa ya matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019 pamoja na taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2020 katika Mkoa huo.
“ Mwalimu kutokuwepo shuleni, kutokuja kabisa shuleni, watoro wapo, pwngine hawaripotiwi ipasavyo katika vyombo vya maamuzi vyenye kutoa maamuzi kwa wakurugenzi hawajui na yawezekana hata maafisa elimu hawajui, wapo waalimu anatoroka yupo Mbeya anafanya mambo yake, lakini mwalimu Mkuu hasemi. Sasa hili ni tatizo,” Alisema
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Kalolo Ntila alisema kuwa waaalimu wengi wamekuwa wakifika shuleni na kufanya kazi ya ‘kuchati’ na sumu zao mpaka muda wa kazi unakwisha na kwenda nyumbani na hivyo kuutaka uongozi wa mkoa kutafuta mwarobaini wa tabia hizo za waalimu.
“Bado naendelea kujitafakari hivi hao waalimu wamesomea mbinguni, hao wanaofundisha shule za binafsi, nidhamu na uwajibikaji ni kubwa sana katika hizi shule binafsi, waalimu hawa watuambie ni mambo gani yanayowapelekea kutowajibika ili tuelewe,” Alisema.
Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Apolinary Macheta alisema kuwa shule ambazo waalimu hawana mahusiano na wazazi kitaaluma, shule hizo daima huwa chini sana kitaaluma na kuongeza kuwa waaalimu wanahitajika kufanya vikao na wazazi ili kutambua changamoto mbalimbali za shule na kuweza kushirikiana kuzitatua.
Ambapo katika kuunga mkono jambo hilo mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga John Msemakweli amezitupia lawama bodi za shule kushindwa kutatua matatizo ya utoro wa wanafunzi, waalimu pamoja na kuona namna ya wanafunzi hao kupata chakula mashuleni ili kuweza kuongeza ufaulu kwakuwa wanafunzi hao hushinda njaa jambo linalowafanya kushindwa kuwa makini na masomo.
Katika kulitafutia mwarobaini suala hilo la chakula masuleni mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Mazwi Godson Mwaibingila ameuomba uongozi wa mkoa kutoa maelekezo kwa halmashauri ili suala hilo la chakula liwekwe katika sheria ndogo za halmashauri na kuweza kuwalazimisha wazazi kuchangia chakula katika shule za msingi na sekondari ndani ya mkoa.
Aidha, Diwani wa Kata ya Chala, Wilayani Nkasi Michael Mwanalinze alisema kuwa sera ya elimu bure itolewe kwa upana wake ili kuhakikisha wazazi wanaielewa, tofauti na hali ilivyosasa kuwa wazazi hawachangii chochote wakisema kuwa elimu ni bure na kuonya kuwa endapo hali hiyo itaendelea basi ufaulu utaendelea kushuka.
Kwa upande wake kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Winnie Kijazi aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanashughulikia matatizo hayo kwani yapo chini ya mamlaka yao kama halmashauri pamoja na mabaraza yao na kuongeza kuwa mkoa umekuwa ukitoa ushirikiano katika kuhakikisha wanafunzi wanaodhulumu haki za kusoma za wanafunzi wanafikishwa katika vyombo husika kwa taratibu za kisheria.
Jumla ya Watahiniwa 16,069 sawa na asilimia 81.01 wakiwemo wavulana 7,953 na wasichana 8,116 wamefaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019. Huku ufaulu huo ukipanda kwa asilimia 8.01 ukilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2018 uliokuwa asilimia 73.00 na kupelekea kushika nafasi ya 13 kitaifa kati ya mikoa 26.
No comments:
Post a Comment