TFS YATOA GAWIO LA SHILINGI BILIONI 24.891 KWA SERIKALI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 25 November 2019

TFS YATOA GAWIO LA SHILINGI BILIONI 24.891 KWA SERIKALI


 WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imetoa gawio la kiasi cha shilingi bilioni 24.891 kwa Serikali ikiwa ni makusanyo ya Wakala kwa mwaka 2018/2019.

 Akizungumza na mwandishi wetu jijini Dodoma mara baada ya makabidhiano ya hundi ya gawio hilo, Kamishna Mhifadhi wa Misitu Prof. Dos Santos Silayo (pichani akikabidhi juu) alisema yeye pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri TFS Br. Jenerali Mkeremy walimkabidhi mfano wa hundi Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa hafla ya upokeaji gawio, michango na ziada kutoka Mashirika na Taasisi za Umma iliyofanyika Ikulu Chamwino, Dodoma.

 Prof. Silayo anasema mchango huu unatokana na makusanyo ya TFS kwa mwaka 2018/19 ambapo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ulipanga kuchangia bilioni 18.39 kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma na. 6 ya mwaka 2001 na marekebisho yake ya mwaka 2015 na kufanikiwa kuchangia shilingi bilioni 24.891 ikiwa ni ziada ya shilingi bilioni 6.5.

 “Tumetoa gawio la shilingi bilioni 24.891 mwaka huu, gawio hili limeifanya TFS kuwa miongoni mwa taasisi 6 bora kati ya Taasisi 79 zilizochangia na kutunukiwa cheti cha uchangiaji bora kwenye mfuko Mkuu wa Serikali,” alisema Prof. Silayo.

 Prof. Silayo anawashukuru wafanyakazi wote wa TFS kwa kila mmoja na nafasi yake, uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Waziri ya Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, Bodi ya Ushauri ya TFS iliyo chini ya mwenyekiti wake Br. Jenerali Mkeremy na wajumbe wote kwa uchapakazi na uongozi thabiti uliowezesha TFS kukusanya na hatimaye kuwasilisha sehemu ya mapato yake kwa serikali.

 “Niwatake wafanyakazi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kuendela kuwa kielelezo bora katika usimamizi endelevu wa rasilimali za kitaifa za misitu na nyuki ili kuchangia mahitaji ya kijamii, kiuchumi, ki-ikolojia na kiutamaduni kwa kizazi cha sasa na kijacho, “Prof. Silayo.

 Hii ni mara ya pili kwa TFS kuchangia gawio la Serikali ambapo katika mwaka wa fedha uliopita jumla ya shilingi bilioni 22.41 ilikabidhiwa kwa Serikali kama gawio.

No comments:

Post a Comment