NDITIYE ASHUHUDIA KUWASILI KWA VIFAA VYA UJENZI WA MELI MPYA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 2 October 2019

NDITIYE ASHUHUDIA KUWASILI KWA VIFAA VYA UJENZI WA MELI MPYA

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akiwashukuru madereva wanajeshi wa Tanzania na wakandarasi wa Korea walioleta shehena ya kontena 17 (zinazoonekana nyuma yake) za vifaa vya kujenga meli mpya ya Ziwa Victoria baada ya kuwasili kutoka bandari ya Dar es Salaam. Wa tatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli, Erick Hamisi akitoa taarifa ya kuwasili kwa shehena ya kwanza ya vifaa vya ujenzi wa meli mpya ya Ziwa Victoria kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kulia mbele) wakati wakisubiri kupokea vifaa hivyo, Mwanza.

Na Prisca Ulomi, Mwanza
NAIBU Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye ameshuhudia kuwasili kwa shehena ya kwanza ya kontena 17 kati ya 300 zenye vifaa kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya ya Ziwa Victoria mkoani Mwanza itakayogharimu shilingi bilioni 89
Nditiye amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametimiza ahadi yake aliyoitoa miaka minne iliyopita kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa ya kuwajengea meli mpya baada ya kuzama kwa meli ya MV Bukoba miaka 23 iliyopita
Ameongeza kuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imeleta wataalamu watakaoshirikiana na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na mkandarasi kutoa Korea ambayo ni Kampuni ya Gasentec Ltd wanayojenga meli hiyo kuhakikisha kuwa ujenzi wa meli hiyo unakamilika kwa wakati ili watanzania watumie huduma ya usafiri huo katika kuhakikisha kuwa wanasimamia na kutekeleza malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwatumikia watanzania
Nditiye amempongeza Kanali A. Fuko, Mkuu wa Msafara wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa niaba ya madereva wanajeshi kwa kazi kubwa wanayoifanya siyo tu ya kulinda usalama wa nchi yetu bali hata ya kushiriki shughuli za maendeleo kwa kusafirisha shehena ya awali ya kontena 17 kati ya 300 kutoka banadari ya Dar es Salaam na kuleta Mwanza kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya ambapo wametumia siku tatu tu badala ya siku saba ambazo huwa zinatumika kusafirisha mizigo
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Erick Hamisi amesema kuwa ujenzi wa meli hiyo utagharimu shilingi bilioni 89 ambapo hadi sasa tayari Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelipa shilingi bilioni 30 kwa mkandarasi wa kujenga meli hiyo ambayo ni kampuni ya Gasentec Ltd kutoka Korea
Hamisi amefafanua kuwa mell hiyo itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 mizigo tani 400 na magari 20 ambapo itakuwa na urefu wa mita 92.6, urefu wa kwenda juu mita 11.2 ambazo ni sawa na ghorofa nne, upana wa mita 17 na itakuwa ni meli kubwa kwa ukanda wa Ziwa na itachukua muda wa miezi 24 kukamilika ambapo hadi sasa tayari miezi 12 imeisha na inatarajiwa kuajiri watanzania 250
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Gasentec Ltd, Donganyang Kwak amesema kuwa kila mwezi wanategemea kupokea shehena ya kontena 20 hadi 30 kwa ajili ya ujenzi wa meli hiyo na malengo yao ni kuhakikisha kuwa ujenzi unakamilika na watajitahidi kwa juhudi zao zote ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya meli hiyo itakapokamilika
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema kuwa ujenzi wa meli hiyo utakapokamilika na kuanza kutoa huduma kwenye kanda ya Ziwa utaongeza chachu ya maendeleo ya Mkoa wa Mwanza na utafungua fursa mbali mbali na kuchangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa letu
Katibu wa CCM wa Mkoa wa Mwanza, Salumu Mkalli amesema kuwa Chama cha Mapinduzi kimeamua kuwatumikia watanzania hivyo tumuunge mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwa ameamua na anatekeleza ambapo mradi huu wa ujenzi wa meli utakapokamilika hautanufaisha watu wa Mwanza tu bali na wa sehemu nyingine
Katika hatua nyingine, Nditiye amekagua maendeleo ya ukarabati wa meli ya MV. Victoria na ujenzi wa chelezo. Aidha, amewataka wakandarasi wanaohusika kuhakikisha kuwa wanakamilisha kazi hizo kwa wakati na wafanye kazi usiku na mchana ili kuendana na muda waliopewa na Serikali wa kukamilisha kazi

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments:

Post a Comment